Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
MAHAKAMA imekataa kutoa amri ya kumwachia huru kwa muda mfanyabiashara Yusuf Manji, badala yake imeamuru kusikiliza maombi yake ya kupinga kuwekwa kizuizini Jumatatu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kupokea maombi yaliyowasilishwa kwa njia ya mdomo na wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo mbele ya Jaji Ama–Isario Munisi.
Wakili Ndusyepo alisema walishangazwa na kitendo cha kumweka chini ya ulinzi Manji akiwa Hospitali ya Agha Khan.
Katika maombi yaliyowasilishwa mahakamani, inadaiwa kwamba Manji anashikiliwa isivyo halali, hivyo wanaiomba mahakama imwachie huru.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa jana, lakini upande wa Idara ya Uhamiaji ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomya, uliomba kuwasilisha majibu ya hati kinzani.
Jaji Munisi alikubali kuwapa muda hadi Jumatatu wiki ijayo, wawe wamewasilisha majibu hayo na kesi itaanza kusikilizwa saa nane mchana siku hiyo.
Wakili Ndusyepo aliwasilisha maombi kwa njia ya mdomo, akiomba mteja wake aachiwe huru kwa muda hadi maombi yaliyowasilishwa yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Jaji Munisi alikataa kutoa amri hiyo na kuamuru maombi ya kupinga kuendelea kuwapo kizuizini kusikilizwa Jumatatu ya wiki ijayo.
Katika hatua nyingine, kesi ya kudaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili Manji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, imeahirishwa hadi Aprili 18, mwaka huu.
Katika hati ya mashtaka, inadaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu, maeneo ya Upanga Sea View wilayani Ilala katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambako alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.