Mahakama yakusudia kumpa dhamana aliyemzushia Jenerali Mwamunyange

0
999

Davis MwamunyangeNA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inaangalia mwelekeo wa kumpa dhamana mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), Benedict Ngonyani, anayetuhumiwa kusambaza taarifa za uzushi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, amelishwa sumu.

Hayo yalidaiwa jana mahakamani hapo, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa na upande wa Jamhuri na kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

Hakimu Mkazi Respicius Mwijage, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, mwaka huu kwa ajili ya kuangalia mwelekeo wa kumpa dhamana mshtakiwa.

Wakili wa Serikali Mwandamkizi, Shadrack Kimaro, aliwasilisha mahakamani hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akidai kwa mamlaka aliyonayo amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa mshtakiwa kwa sababu kuna mambo ya taifa anayoyashughulikia.

Hakimu Mwijage, awali alikubali kumnyima dhamana mshtakiwa, lakini baada ya siku 14 alihoji akitaka Jamhuri itoe sababu za kuendelea kuwapo kwa zuio hilo.

Kutokana na kutokuwapo sababu za msingi, mahakama hiyo iliahirisha kesi hadi siku iliyopangwa kwa ajili ya kuangalia mwelekeo wa kumpa dhamana mwanafunzi huyo.

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kimaro kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungura, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa, Jackline Nyantori na Anastazia Wilson, walimsomea mshtakiwa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Mwijage.

Kimaro alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo, Septemba 25, mwaka huu, Dar es Salaam, ambapo alisambaza taarifa kupitia mtandao wa Facebook, kwamba Jenerali Mwamunyange amelishwa sumu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here