Na JANETH MUSHI, ARUSHA
MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Arusha, imefuta maombi ya jinai namba 56 ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na mawakili wanaomtetea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).
Maombi hayo yalifutwa jana baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani mwanzoni mwa wiki hii, baada ya kushikiliwa na polisi kwa siku kadhaa bila kufikishwa mahakamani.
Novemba 7 mwaka huu, Wakili John Mallya na Sheck Mfinanga walifungua maombi mahakamani hapo wakiiomba mahakama hiyo iamuru mteja wao apelekwe mahakamani baada ya Jeshi la Polisi kumshikilia Lema kwa zaidi ya saa 175 bila kumfikisha mahakamani.
Maombi hayo yaliyofunguliwa chini ya hati ya dharura, yalipangwa kusikilizwa Novemba 8, mwaka huu na Jaji Salma Maghimbi wa mahakama hiyo, lakini wakati yanaanza kusikilizwa, jaji huyo alilazimika kuahirisha kesi baada ya mawakili wa Lema kuitaarifu mahakama hiyo, kuwa mteja wao tayari alikuwa amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Arusha.
Kutokana na hatua hiyo, Jaji Maghimbi aliahirisha kusikiliza maombi hayo na kuwalazimu mawakili wa Lema kutoka mbio mahakamani wakielekea alipokuwa mteja wao akisomewa mashtaka ya uchochezi.
Akitoa uamuzi wa maombi hayo juzi, Jaji Maghimbi alisema baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa Lema amepelekwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayomkabili, mahakama hiyo inafuta maombi hayo.
Upande wa utetezi ulikuwa umeomba mahakama hiyo pia iamuru upande wa Jamhuri ulipe gharama za kesi ambapo jaji huyo aliagiza kila upande ugharamie gharama za maombi hayo.
“Kila upande ubebe gharama za maombi kwa sababu maombi hayakuwa yamesikilizwa kwa kina.
“Lakini, kama yangekuwa yamesikilizwa kwa kina, upande wa Jamhuri ungewalipa gharama za maombi haya,” alieleza Jaji Maghimbi.
Novemba 8 mwaka huu, Lema alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Arusha, akikabiliwa na kesi mbili za uchochezi.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa na Lema kurudishwa mahabusu, leo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Desderi Kamugisha, anatarajia kutoa uamuzi kama Lema anastahili dhamana au hastahili kama mawakili wa Serikali walivyokuwa wameomba.