31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAAMURU SETHI ATIBIWE MUHIMBILI

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeamuru kwa mara nyingine mfanyabiashara Harbinder Sing Sethi, akatibiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mahakama ilitoa amri hiyo kwa mara nyingine, baada ya Jamhuri kushindwa kutekeleza amri iliyotolewa na mahakama hiyo zaidi ya mara mbili ya kuwataka wafanye hivyo ili kunusuru uhai wa mshtakiwa.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya Wakili wa Sethi kuifahamisha mahakama kuwa mteja wake hajapatiwa matibabu.

Wakili huyo, Melchisedeck Lutema aliwasilisha malalamiko kuhusu tiba kwa mteja wake, baada ya Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai upelelezi haujakamilika anaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Wakili Lutema akijibu aliiomba mahakama kuiamuru Jamhuri, kueleza kwanini mshtakiwa namba moja hakupelekwa Hospitali ya Muhimbili kama mahakama ilivyoamuru.

“Tunaomba mahakama itumie busara baada ya kusikiliza maelezo ya Jamhuri kuhakikisha mshtakiwa anapelekwa hospitali kwa matibabu,”alidai.

Wakili wa mshtakiwa wa pili ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila, Pascal Kamala alidai washtakiwa wako rumande kwa siku 87 sasa tangu Juni 16, mwaka huu na makosa yao hayana dhamana, wanaambiwa upelelezi bado.

Wakili Kamala, aliomba Jamhuri wakamilishe upelelezi haraka ili haki ionekane inatendeka.

Akijibu hoja za utetezi, Wakili wa Swai alidai mshtakiwa Sethi alipatiwa matibabu Hospitali ya Magereza na mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Dotto Pakecha na kwamba mtaalamu huyo anafuatilia afya yake kwa kumuona kila siku.

“Mshtakiwa aliwahi kutibiwa katika Hospitali ya Amana na kuandikiwa vipimo vya MRI ambavyo vinapatikana Muhimbili, hata hivyo mshtakiwa hajawahi kuwasilisha ripoti yake ya matibabu ya awali gerezani.

“Washtakiwa wanakabiliwa na makosa ya kughushi, upelelezi bado unaendelea, makosa yao upelelezi wake unahusisha ofisi zaidi ya moja ndio maana unachukua muda mrefu,”alidai Swai.

Wakili Lutema alidai maelezo ya Jamhuri hayana uthibitisho hivyo aliiomba mahakama kumruhusu mshtakiwa kueleza kama anapatiwa matibabu au laa.

“Umetibiwa….?,Alihoji Hakimu Shaidi.

“Sijatibiwa….”alijibu Sethi.

Akitoa uamuzi, Hakimu Shaidi alisema amri za mahakama lazima zifuatwe kwani ilishaamuru apelekwe kwa wataalamu zaidi kutokana na tatizo lake la kuwekewa puto tumboni.

“Kila siku mahakama inatoa amri kwa kitu kimoja haifatwi…haina maana, kama hazifuatwi hakuna sababu ya kuja mahakamani.

“Hainifurahishi…nasisitiza mshtakiwa epelekwe hospitali,”alisema Hakimu Shaidi.

Awali, Wakili Joseph Mwakandege aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa  asipopelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu sahihi anaweza kupoteza maisha.

Washtakiwa katika kesi hiyo Seth na James Rugemarila, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwa na mashtaka 12 yakiwemo ya kughushi,kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 hivyo kuwafanya wakose dhamana.

Rugemarila ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na Sethi, mwenyekiti mtendaji wa kampuni hiyo, wanaendelea kushikiliwa gereza la Segerea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles