NA GURIAN ADOLF, NKASI
MAHAKAMA wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, imewataka mashahidi wanaofika mahakamani hapo kutoa ushahidi wa kesi za wanafunzi waliopewa ujauzito kuacha kuhofia gharama ya nauli, kwani mahakama itawarejeshea.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, Ramadhani Rugemalila, aliyasema hayo jana, alipokutana na wasemaji wa vijiji katika mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Plan International, kupitia mradi wa kukabiliana na ndoa na mimba za utotoni wilayani humo.
Alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwa mashahidi kutohudhuria mahakamani wakidai kuwa hawana fedha za kusafiri na kujikimu kila wanapohudhuria mahakamani, hali ambayo imekuwa ikisababisha kutokamilika kwa ushahidi na hivyo watuhumiwa wa mimba za wanafunzi kutotiwa hatiani.
“Hivi sasa mahakama kupitia kitengo cha uhasibu kinarejesha gharama ili mradi tu kuwepo kwa vithibitisho kama stakabadhi watakuwa wakirudishiwa fedha zao, hivyo hakuna sababu za kukwepa kuhudhuria,” alisema.
Alisema kuwa, hivi sasa serikali inapambana na watu wanaowapa mimba wanafunzi, hivyo ni lazima mashahidi washiriki kikamilifu katika vita hiyo kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi ili waipe nguvu mahakama kuwashughulikia watu hao, kwani hakuna mwanya wa kuwaacha waendelee kutamba kwa vitendo vyao viovu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo kutoka Shirika la Plan International, Nestory Frank, alisema Shirika hilo linajitahidi kutoa elimu, lakini ni lazima jamii ishiriki kwa hali na mali katika kukabiliana na vitendo hivyo.