Na Mwandishi Wetu, Kigoma
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Lameck Michael Mlacha ameongoza kikao cha Menejimenti katika Kanda hiyo kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa robo mwaka ya Januari hadi Machi, 2023 lengo likiwa ni kuboresha zaidi huduma ya utoaji haki katika Kanda hiyo.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Jaji Mlacha aliwataka wajumbe pamoja na watumishi wote wa Mahakama katika Kanda hiyo kujitathmini na kuchukua hatua za mabadiliko chanya ya kuboresha utendaji kazi.
“Siku chache zilizopita niliwaletea maelekezo ya Jaji Kiongozi ambayo kwa ufupi yanahusu kuboresha mikakati ya kumaliza mashauri ya mlundikano. Maelekeo hayo yanatakiwa yatekelezwe na kutolewa taarifa kama tulivyoagizana” amesema Jaji Mlacha.
Jaji Mfawidhi huyo amewakumbusha viongozi na watendaji kushiriki kikamilifu katika kutekeleza yale yote yanayoazimiwa na kikao ikiwa ni pamoja na maelekezo mbalimbali ya Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Tanzania ambayo yanatolewa siku hadi siku.
Amesema tathmini hiyo ya utendaji kazi ilionesha kuwa Kanda ya Kigoma inaendelea kufanya vizuri katika usimamizi wa jukumu kuu la utoaji haki ambapo matumizi ya TEHAMA yameendelea kuimarika katika kusajili mashauri na kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao.