27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA KUTOA UAMUZI LEO JUU YA DHAMANA YA LEMA  

Na JANETH MUSHI -ARUSHA


pg-1

UAMUZI wa kusikilizwa maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema utajulikana leo mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Sekela Moshi.

Jaji Moshi anatarajiwa kutoa uamuzi huo baada ya  Mawakili wa Serikali kuweka pingamizi za awali wakipinga Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa mshitakiwa Alhamisi iliyopita.

,Jaji Moshi alisikiliza hoja za sheria za pande zote mbili na  baada ya  mabishano ya sheria aliahidi atatoa uamuzi wa maombi hayo leo.

Uamuzi wa pingamizi hizo unatarajiwa kueleza endapo Mahakama hiyo itasikiliza maombi hayo au kuyatupilia mbali.

Katika maombi hayo namba sita ya mwaka huu, Mawakili Waandamizi wa serikali,  Matenus Marandu na Paul Kadushi, waliwasilisha maombi hayo huku upande wa wajibu maombi (Lema) ukiwakilishwa na  jopo la mawakili sita wakiongozwa na Peter Kibatala, John Mallya, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, Faraji Mangula na Charles Adiel.

Akiwasilisha pingamizi hizo, Wakili Kadushi, aliiomba Mahakama  kuwaruhusu kuwasilisha pingamizi moja na mahakama ikishindwa kuridhia pingamizi hiyo wawasilishe pingamizi la pili.

Alidai  maombi hayo yaliyosainiwa na Wakili Kibatala,   walitumia kifungu cha 372 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinaipa Mahakama Kuu kufanya mapitio ya mashauri ya kesi za mahakama za chini.

Kadushi alidai   hoja ya sheria ni kuwa baada ya mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2002 yaliondoa haki za pande zozote katika kesi za jinai kuomba rufaa au mapitio ya uamuzi mdogo uliofanywa katika mahakama zinazoongozwa na mahakimu nchini.

Hoja ya pili iliyowasilishwa mahakamani hapo ni kuwa maombi ya Lema hayajakidhi matakwa yasheria kifungu cha 359(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu asiporidhika na uamuzi wa mahakama ya chini, anatakiwa kukata rufaa mahakama kuu.

Kwa upande wake, Kibatala ambaye alikuwa akiwawakilisha mawakili wenzake watano, alidai hoja za sheria zilizowasilishwa   na upande wa Jamhuri hazina mashiko  katika sheria na akaiomba mahakama izitupilie mbali.

Aliiambia mahakama kwamba hakimu aliyeruhusu wakili wa Serikali kusimama kabla hajafikia mwisho wa uamuzi aliokuwa akiusoma ni ishara kuwa mahakama hiyo haikuongozwa vizuri jambo ambalo linaifanya Mahakama Kuu iingilie kati na kutoa maelekezo.

“Hoja walizoleta Serikali hazijakidhi matakwa ya sheria, kwanza pingamizi hiyo haijasema inakuja kwetu au inaenda kwa mahakama.

“Kwa sababu  sisi na Serikali tumeitwa hapa mahakamani na hii ni kama mwananchi wa kawaida kwenda kwa msajili kulalamika. Jaji akawaita pande zote mahakamani huwezi kuweka pingamizi,”alidai Wakili Kibatala.

Alidai kifungu cha 373 cha Sheria hiyo ya Makosa ya Jinai kianaeleza namna gani  mahakama kuu inaweza kupata taarifa ya upungufu wa mwenendo katika mashauri yanayoendelea mahakama za chini na ina uhuru wa kuitisha majalasda na kusikiliza maombi upande wowote kati ya serikali au utetezi.

“Mahakama ilijivua mamlaka ambayo inayo, ikiwa ni pamoja na kazi yake ya sheria.  Hakimu alikosea hata kumruhusu Wakili wa Serikali kusimama
wakati wa uamuzi.

“Nasema hivyo kwa sababu kifungu cha 148(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema Mahakama ikitoa dhamana kwa mshitakiwa ni lazima ifikie mwisho wa hatua ya uamuzi wake kwa kuweka  masharti ya dhamana.

“Lakini mahakama iliishia njiani baada ya  Wakili wa Serikali kusimama, kueleza kusudio la kukata rufaa,” alidai Wakili huyo.

Wakili Kibatala aliomba mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi hizo kwa gharama na kusikiliza maombi hayo ya dhamana ya mteja wao.

Katika maombi hayo, Lema kupitia mawakili wake, anaiomba mahakama hiyo  ifanye mapitio ya majalada ya kesi za jinai namba 440 na 441 mwaka huu, ambako anakabiliwa na makosa ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Mawakili hao wa Lema wanaomba ombi hilo kwa sababu wakati Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,Desderi Kamugisha akisoma uamuzi huo uliokuwa na kurasa 22 hivi karibuni, alisema Mahakama inamwachia Lema kwa dhamana kwa masharti atakayopewa na mahakama hiyo.

Hata hivyo, kabla hajakamilisha uamuzi huo akiwa katika ukurasa wa 21 kati ya 22, mawakili wa serikali walisema Serikali inakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles