19.8 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Nitapambana na wala rushwa

magufuliNa Bakari Kimwanga, Rukwa

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema ikiwa atachaguliwa kuongoza Serikali ya awamu ya tano atahakikisha anapambana na watendaji wala rushwa serikalini.

Amesema watendaji hao ndiyo wamekuwa wakikwamisha juhudi za Serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi hali inayosababisha malalamiko ya wananchi.

Kauli hiyo aliitoa jana kwa nyakati tofauti alipohutubia wananchi katika mikutano ya kampeni  katika mikoa ya Katavi na Rukwa.

Dk. Magufuli pia aliahidi kufuta utaratibu wa wakulima kukopwa mazao yao na serikali.
Alisema utaratibu huo umekuwa hauleti tija kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakirudi nyuma kwa maendeleo badala ya kusonga mbele.
“Hakuna jambo linaloniudhi kama wakulima kukopwa mazao yao, ninajua mikoa ya Katavi hasa Majimoto   na Nkasi ni wakulima wazuri wa mahindi na mpunga ila nimekuwa siridhiki na namna watu wanavyokopwa mazao yao.

Mgombea huyo wa urais aliwaahidi wananchi kuwa ikiwa atafanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu wa tano, kuanzia Februari mwaka kesho elimu ya msingi hadi sekondari itakuwa bure kwa watoto wote.

“Fedha zipo lakini kuna wala rushwa wachache ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali, mimi ninasema nichagueni nikapambane na watendaji wabovu ambao hawafai kwa sasa.

“Ninajua wazi kero kubwa ni barabara na ninachopenda kuwaambia wakandarasi waliposikia nimeteuliwa kuwania urais hivi sasa wote wamerudi kazini licha ya wengine hawaidai serikali, na ni lazima barabara ya Nkasi-Mpanda ikamilike kwa wakati.

“Kubwa ninachowaomba mniamini ndugu zangu na mnichague mimi   na wabunge, madiwani wa CCM,” alisema.
Dk. Magufuli alisema ingawa Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa  changamoto zimebaki na akaahidi kuzikamilisha kwa wakati.

“Ninashangazwa sana leo tuna kero ya maji sasa inafanyika wiki ya maji wakati maji yenyewe hayapo, wiki ya Ukimwi dawa hakuna, wiki ya maziwa lakini viwanda na maziwa hakuna, kwangu ninataka kurekebisha hili kwa vitendo,” alisema.

Alisema moja ya ahadi yake kupitia ilani ni kuhakikisha ujenzi wa zahanati na huduma ya umeme kwa kila kijiji katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake.

“Ilikuwa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere (Julius), mzee Mwinyi, Mkapa, Rais Kikwete na awamu ya tano ninawaomba mnikabidhi mimi kwani
ni zamu yangu kuwatumikia Watanzania,” alisema.

Wakati huohuo, mgombea mwenza wa Dk. Magufuli, Samia Suluhu Hassan aliwataka wananchi wa Vunjo mkoani Kilimanjaro kushughulikia bei ya kahawa   wakulima waweze kunufaika na zao hilo, anaripoti Patricia Kimelemeta kutoka Moshi.

Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Marangu Mtoni, Samia alisema bei ndogo iliyopo inasababisha wakulima wa zao hilo kutafuta masoko nje ya nchi.

Alisema  lengo la CCM ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, hivyo  atashughulikia suala hilo na kuhakikisha bei ya zao hilo inapanda.

“Serikali ya awamu ya tano imepanga kushughulikia mambo mbalimbali yakiwamo kupanda kwa bei ya kahawa   iweze kuwasaidia wakulima wa zao hilo,”alisema Samia.

Alisema  licha ya kushughulikia suala hilo,   pia CCM imepanga kujenga soko la Himo  liweze kuwanufaisha wakulima wa mazao mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles