23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Nchi inahitaji mabadiliko

pombeNa Bakari Kimwanga, Mbeya

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema taifa linahitaji mabadiliko ya kiuongozi chini yake na siyo kwa kubadili chama kilichopo madarakani.

Amesema pamoja na kuwa kuna wimbi la watu wanaotaka mabadiliko, ni vema wakatambua kwamba yatapatikana kupitia CCM na si nje ya chama hicho.

Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbalizi, Mbeya Vijijini na Wilaya ya Chunya mkoani hapa kwa nyakati tofauti.

Dk. Magufuli alisema hata nchi ya China imefanikiwa kufanya mabadiliko na kuwa nchi ya daraja la kwanza kiuchumi ikiwa chini ya chama tawala cha CPC.

Alisema ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano, atahakikisha anaharakisha maendeleo ya nchi kwa kudhibiti mianya ya rushwa, hasa katika ngazi za juu serikalini.

“Nchi yetu inahitaji mabadiliko lakini si ya kukiondoa chama madarakani, hata nchi ya China ambayo inaongozwa kijamaa ilifanya mabadiliko. Lakini hawakukiondoa chama tawala madarakani.

“Ila wamejipanga na kubadili mfumo wao, nasi hapa Tanzania kwetu tunaweza kuleta mabadiliko ya kimfumo na kuimarisha uchumi. Leo nchi ya China chini ya chama tawala wameweza kuwa nchi ya daraja la kwanza na sasa imekuwa ikiogopwa na nchi kubwa kama Marekani.

“Kubadili chama sio suluhisho na hakuna wa kuleta mabadiliko ila ni mimi Magufuli, nayaweza haya. Maana haraka haraka haina baraka, zipo nchi tumeona leo zilipo, mfano nchi ya Libya walimwondoa na kumuua Gadafi (Muhamar), nchi ilikuwa na utaratibu wa kijana akitaka kuona anapewa pesa na nyumba na Serikali, leo wako wapi?” alisema Dk. Magufuli.

Alisema anaomba Watanzania wamchague ili aweze kusimamia Serikali na kuharakisha maendeleo ya kasi kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, dini na ukabila.

Mgombea huyo wa urais wa CCM, alisema Tanzania ilipofika sasa watu wake hawatakiwi kugomba kwa vyama ila wanachotakiwa ni kuheshimiana na kujenga hoja kwa amani na utulivu.

Alisema anashangazwa na baadhi ya watu kuhangaika na hata kufikia kuchomeana moto bendera za vyama hali ya kuwa vitendo hivyo havisaidii kuleta maendeleo ya nchi.

“Ninataka kuwaambia kuchoma bendera za vyama haisaidii kuleta maendeleo, ndiyo maana mimi nataka kuwa rais wa Watanzania wote, na nitakuwa rais wa Chadema, CUF, ACT, CCM na hata wasiokuwa na vyama.

“Leo kuna kiu ya mabadiliko kubwa, na kubwa ikiwa mtanichagua elimu ya msingi hadi kidato cha nne itakuwa bure. Najua watu watasema wapi nitatoa hela, nchi yetu ina mapato mengi sana ila kuna wajanja kule juu serikalini wanafanya tofauti, sasa nataka nikapambane nao hukohuko,”  alisema.

Alisema pamoja na hayo yeye si mwanasiasa ila mtendaji ambaye amejipanga kuwatumikia Watanzania.

“Ninaomba kura mnichague watu wa Chadema, CUF na wengine wote, maana kuna wengine wanasemaga ‘Peoples power’, sasa nipeni hiyo power nikawe rais wa vitendo.

“Ninataka kuijenga nchi na kuleta mabadiliko bora kwa Watanzania wote pamoja na maendeleo kwa wote,” alisema.

 

KUFUTA WIKI YA MAJI

Akiwa Chunya, Dk. Magufuli, alisema ikiwa atachaguliwa kuwa rais, katika Serikali yake hakutakuwa na maadhimisho ya Wiki ya Maji.

Alisema inashangaza watu kufanya maadhimisho hayo huku wakitafuta fedha na wananchi wakiendelea kukosa maji mijini na vijijini.

“Mimi nimeomba urais sio kwa majaribio, ninajua matatizo ya Watanzania, ndiyo maana nasema na ninajua hapa Makongolosi hakuna maji, lakini kule juu wanatafuta fedha kwa maadhimisho ya Wiki ya Maji hali ya kuwa watu hawana maji.

“Ikiwa mtanichagua, Serikali yangu ya awamu ya tano itafuta maadhimisho ya Wiki ya Maji ambayo fedha nyingi hutumika huku gharama za kuchimba kisima haizidi shilingi milioni 25. Na Waziri wa Maji nitakayemteua atakuwa na kazi ya kuleta maji na sio kila siku tuko kwenye mchakato.

“Na akiwa na lugha hii itabidi akae pembeni ili akajichakatue mwenyewe, hili sikubali hata kidogo. Kikubwa nawaomba mniamini na mnichague ili nianze kazi hii kwa kasi ili niwatumikie,” alisema Magufuli.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles