30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Nachukia mauaji ya Kiteto

g jpg*Asema hayupo tayari kuongoza Serikali inayovuja damu

 

Na Bakari Kimwanga, Kongwa

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema amechoka kusikia mauaji ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto.

Mgombea huyo alisema akichaguliwa kuwa rais atashughulika na Mkuu wa Mkoa (RC) na Mkuu wa Wilaya (DC), atakaowateua iwapo mauaji hayo yataendelea.

Alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) atakayeteuliwa anapaswa kujipanga vizuri kusimamia amani katika eneo hilo la sivyo hatamwonea haya.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo jana wilayani Kongwa mkoani Dodoma, wakati akihutubia mkutano wa hadhara.

Alisema hayupo tayari kuongoza Serikali inayovuja damu, hasa kwa mapigano ya wakulima na wafugaji.

Kutokana na hali hiyo, alisema kama atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha anatumia sheria namba 4 ya ardhi na namba 5 ya vijiji, ili kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo.

Alisema anatambua changamoto kubwa inayowakabili Watanzania, ikiwamo udogo wa ardhi, wakati idadi ya watu ikiongozeka.

“Katika mambo yanayoniumiza ni mauaji ya kila mara ya wakulima na wafugaji, tumechoka kuzika ndugu zetu wanaouana kwa ajili ya ardhi…siwezi kuvumilia jambo hili.

“Ninasema  kiongozi nitakayemteua hasa mkuu wa mkoa na OCD, nitaondoka nao katika jambo hili.

“…haiwezekani watu wanauana halafu viongozi niliowateua wanakula upepo, nasema hawa ndiyo nitaanza nao kwa vitendo. Nahitaji kuongoza nchi kwa misingi ya haki na amani,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema anashangazwa na baadhi ya viongozi hasa wa Serikali kushindwa kukomesha mauaji hayo na badala yake kugeuka kuwa sehemu ya migogoro hiyo.

Alisema tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 haijawahi kushuhudia mapigano ya kutisha kama yaliyotokea Kiteto na kusema sasa tiba ya mapigano hayo ipo mbioni kupatikana.

“Ninajua hivi sasa Watanzania wameamua kuwa Ikulu ni ya Magufuli na CCM, kikubwa ninachoahidi ni utumishi mzuri uliotukuka.

“Nasema hapa kati ya watu ambao walipambana ndani ya Bunge kuhusu mapigano haya, alikuwa mgombea wenu Job Ndugai, hadi mkuu wa wilaya akaondolewa.

“Sasa maadui wake wa kisiasa hawaoni haya, jamani mti mzuri wenye maembe ndio unaopigwa mawe. Ilani ya uchaguzi ya CCM imeweka wazi kuhusu matumizi ya ardhi, nami ninakuja kuyatekeleza kwa vitendo,” alisema.

 

Baa la njaa

Alisema anatambua baadhi ya maeneo nchini yamekuwa yanakabiliwa na ukame, ikiwemo Mkoa wa Dodoma hali inayosabisha mazao kukauka na kusababisha njaa.

Alisema Serikali yake ya awamu ya tano, itaandaa utaratibu maalumu wa kuwawezesha wananchi kulima mazao yanayostahamili ukame na kuahidi kupeleka chakula maeneo hayo.

“Najua changamoto ya ukame hapa Dodoma  ila hakuna mwananchi atakayekufa njaa katika Serikali ya Magufuli, jamani nichagueni muone, hapa kwangu ni kazi tu.

“Ninataka Watanzania waje wanihukumu kwa kufanya kazi na si vinginevyo, narudia kusema hapa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, sitaki kuahidi jambo ambalo sitaweza kulitekeleza mbele yenu na kwa Mungu,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles