33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Mawaziri wangu watafanya kazi usiku na mchana

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

Na Bakari Kimwanga, Tunduma

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akifanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, atakuwa na baraza dogo la mawaziri litakalofanya kazi usiku na mchana.

Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni mkoani Rukwa juzi, Dk. Mgufuli alisema mawaziri wake watahudumia wananchi kwa wakati na si kukaa ofisini na kusubiri kuletewa taarifa.

“Nitateua mawaziri wachache na wenye uadilifu, kama kuna waziri nitakayemteua na akaona hawezi kazi akae pembeni, kwa sasa Watanzania wanataka huduma kwa wakati.

“Haiwezekani mnatuchagua bure kisha na nyinyi mkose huduma, hili hapana ni lazima muhudumiwe bure na kwa wakati,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema Serikali atakayoiunda itakuwa na watu waadilifu na haitakuwa na ngojangoja katika kuwahudumia wananchi.

“Ninajua hapa Laela kuna mradi wa maji unasuasu, najiuliza nikiwa Waziri wa Ujenzi nilifukuza wakandarasi 3,200, sasa kwa nini huyo wa maji yupo? Sasa naomba nafasi ya urais na hawa makandarasi wamaji wajiandae.

“Ninafahamu Watanzania wanataka mabadiliko, wamechoshwa na uonevu na wanataka maendeleo ya haki. Katika uongozi wangu sijawahi kukemewa wala kujiuzulu, siri kubwa ya hilo ni kwamba nilikuwa namtanguliza Mungu,” alisema.

Akizungumzia masilahi ya wafanyakazi na Polisi, alisema katika uongozi wake atahakikisha anaweka mazingira bora ya kazi.

“Katika utawala wangu polisi watapata masilahi bora ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.

“Tunahitaji kuwa na Jeshi la Polisi bora na imara na hatuhitaji kuwa na jeshi la uonevu. Leo mtu anakamatwa na askari kwa kosa la kuwa na bodaboda kisha anabambikiwa kesi nyingine, hii hapana,”alisema.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema  hana kinyongo na Dk. Magufuli na kwamba anashirikiana naye tofauti na baadhi ya watu wanavyodai.

Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), alisema licha ya yeye kuwa miongoni mwa makada 38 waliorudisha fomu kuomba kuteuliwa katika nafasi ya urais, ameridhika na mchakato wa ndani ya chama.

“Leo (jana) nipo hapa kwa ajili ya kushiriki kampeni za Magufuli, nimeridhika na moyo wangu mweupe kabisa sina kinyongo na mgombea wetu.

“Na nimekuja mwenyewe sitaki kusemewa maana kuna watu walishaanza ohooo mara hajaonekana katika uzinduzi wa kampeni … nimekuja sasa nilianza na ndugu Magufuli Katavi na sasa nipo Sumbawanga.

“Mmeona barabara zetu za lami pamoja na mimi kuwa kiranja wa Serikali mtendaji wa hizi barabara ni Magufuli, ujenzi huu alikuwa waziri je akiwa rais ni lazima atamaliza zote na zawadi yetu kubwa ni Oktoba 25 kura zote kwa Magufuli,” alisema Pinda huku akishangiliwa na mamia ya wananchi.

Kwa upande wake Dk. Magufuli, alisema anaomba kura kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania na kuhakikisha anawaletea maendeleo ya kweli.

Alisema hakuamini kama CCM ingemteua ila ni uwezo wa Mungu ndio umemfikisha mahali hapo kutokana na dua za Watanzania na wana CCM.

“Ninajua hapa Sumbawanga kura zote mtanipa mimi lakini siwezi kufanyakazi peke yangu ninawaomba mnichagulie mbunge Aeshi Hilal, ninamuamini maana alikuwa kila siku ananisumbua ndani ya Bunge na ofisini kwangu kutaka pesa za kukamilisha barabara.

“Kubwa mkituchagua mimi na Aeshi mbunge wenu, nitahakikisha namaliza ujenzi wa barabara zote pamoja na Uwanja wa Ndege Sumbawanga kwa kuujenga kwa kiwango cha lami.

“…lakini pia Serikali yangu itakuwa na kazi ya kutoa huduma zenye staha kwa Watanzania nitahakikisha tunatoa elimu bure kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia tatizo la rushwa nchini alisema amejipanga kupambana kwa vitendo na watendaji wabovu ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za maendeleo.

Alisema kutokana na kukithiri kwa hali hiyo anajua wala rushwa na watendaji wanaomchukia kwa usimamizi wake hawatampa kura ila wananchi wengi ambao ndio watetezi wake ndio watamchagua kwa wingi.

“Wale watendaji wazembe mjiandae nimekuwa waziri kwa miaka 20 ninajua kuwa kuna fedha nyingi zinaliwa na wachache sasa wajiandae. Hatutakuwa na mchezo katika hili tutapambana nao kwa vitendo,” alisema.

Alisema anajua Tanzania ina rasilimali nyingi ikiwemo madini, hifadhi za Taifa lakini bado kuna watu wamekuwa wakwepa kodi za Serikali.

“Leo mfanyabiashara mdogo anaonewa kwa kulundikiwa kodi huku wafanyabishara wakubwa wanakwepa kodi hawa ndio nataka kupambana nao katika Serikali ya awamu ya tano.

“Machinga, mama lishe wanaanzisha biashara zao wanaonewa na hata kusumbuliwa kwa kila aina ya kodi jambo ambalo sitakubali uonevu wa aina hii,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles