Nora Damian -Dar Es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kwani si kila kifo kinachotokea kwa sasa kinasababishwa na corona na kuiiagiza wizara ya afya kutangaza takwimu za waliopona ugonjwa huo ili wananchi wajue.
Rais Magufuli pia alisema kuna baadhi ya watu wanashauri Jiji la Dar es Salaam lifungwe kwa kukataza watu kutoka nje ya nyumba zao, suala alilosema kamwe haliwezekani kwani jiji hilo ndilo kitovu cha biashara nchini.
Akizungumza na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama Chato mkoani Geita jana, Rais Magufuli alisema kumekuwa na upotoshaji mwingi uliosababisha Watanzania kuingiwa na hofu na kuitaka Wizara ya Afya kutoa ufafanuzi wa vifo vinavyotokea.
“Si kila anayekufa ni corona ina maana malaria yameacha kuua, kuna upotoshaji mwingi umekuwa ukifanyika kwa ajili ya kuwatisha wananchi, kikubwa nawaomba Watanzania tuiondoe hofu kwa sababu hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko corona.
“Wanaotumia vibaya mitandao wajizuie katika kuandika uongo wa masuala ambayo hayapo, niwaombe pia wananchi muipuuze baadhi ya mitandao.
“Niviombe vyombo vya ulinzi na usalama IGP uko hapa shughulika nao hao ni saizi yako, shirikiana na TCRA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” alisema Rais Magufuli.
DAR KUTOFUNGWA
Rais Magufuli alisema Jiji la Dar es Salaam halitafungwa na kusisitiza watu waendelee kufanya kazi huku wakizingatia tahadhari zinazotolewa na wataalam.
“Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam hili haliwezekani, Dar es Salaam ndio ‘center’ pekee ambako collection ya revenue (makusanyo ya mapato) inapatikana.
“Sasa unapofunga ina maana wasipelekewe mchele, ndizi kutoka Bukoba, wasifanye biashara ya vitenge kupeleka vijijini, madereva wasibebe mafuta kupeleka mikoani.
“Unawazuia watu milioni sita ikitokea Mwanza, Mbeya nao utawafungia, utawafungia mikoa mingapi?” alihoji Rais Magufuli.
Pia alikemea dhana potofu iliyoanza kujitokeza kwa baadhi ya wananchi hasa waishio mikoani ya kuwatenga watu wanaotoka Dar es Salaam na kutaka ikomeshwe mara moja.
“Si kila anayetoka Dar es Salaam ana corona, dhana ya Watanzania kuwaogopa watu wa Dar es Salaama lazima iondoke, corona tutaishinda kwa ushirkiano, kwa kumaliza hofu, kwa kumtanguliza Mungu, kama tulivyoweza kushinda vita vingine,” alisema.
UCHUNGUZI WA BARAKOA
Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa misaada mbalimbali inayotolewa kukabili corona zikiwemo barakoa.
“Tusiamini kila kitu tunacholetewa, vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiiana na wizara ya afya waanze kushughulikia vitu tunavyoletewa kama zawadi.
“Tunapoletewa mask za kujikinga puani ni lazima tujue huyo aliyezitengeneza, aliyezi – supply’ bado Watanzania wanaweza kujishonea wenyewe,” alisema Rais Magufuli.
Alisema hata upuliziaji dawa ambao umekuwa ukifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hakuna uthibitisho kwamba unaangamiza virusi vya corona.
“Nimeowaona viongozi wanazungumza tunafanya fumigation kuua corona ni uongo mtupu, labda vitoto vya mbu. Lazima tujiulize hizo ‘fumigation’ ambazo zimekazaniwa sasa hivi je, kukiwa na virusi vya corona mle ndani
“Hakuna fumigation yoyote inayoweza kuzuia corona, ni lazima tuambizane ukweli, kama kungekuwa panafanyika ‘fumigation’ corona wanakufa basi kwenye nchi zinazoendelea wasingekuwa wanaendelea kufa.
“Fumigation ambayo imekuwa ikifanyika Dar es Salaam ni upuuzi mtupu kwa sababu wataalamu wote wanaojua virusi vya corona huwezi ukaua kwa ‘fumigation’, vinapasuka kwa kutumia sabuni au alcohol,” alisema.
Pia aliiagiza wizara ya afya kuangalia upya utaratibu wa kuwaweka watu karantini na kama mtu hana tatizo aondolewe kuokoa rasilimali za Serikali.
“Hakuna sababu ya mtu kukaa siku 20 wakati anaonekana hana tatizo, tunapoteza resources (rasilimali) zetu,” alisema Rais Magufuli.
TAASISI ZA FEDHA
Rais Magufuli aliziomba taasisi za fedha za kimataifa kuzisamehe nchi zenye madeni ili fedha zitakazookolewa zielekezwe kukabili janga la corona.
Alitoa mfano wa Tanzania kwamba kila mwezi huwa inalipa karibu Sh bilioni 700 kwa madeni yaliyokopwa na nchi kwa taasisi mbalimbali za kimataifa na karibu Sh bilioni 203 zinalipwa kwa Benki ya Dunia.
“Napenda nishauri na kuwaomba vyombo vya kimataifa kama Benki ya Dunia, najua wanatoa ofa ya nchi zinazosumbuliwa na corona kukopa fedha, ni ofa nzuri lakini ningeomba badala ya kutoa ofa ya kukopesha tena kwa ajili ya kupambana na corona watusamehe madeni waliyokopesha hizi nchi.
“Watusamehe madeni hata ‘by percentage’ ili kusudi hizi fedha tunazolipa na ‘interest’ zikatumike sasa kama mbadala wa ‘relief’ katika kupambana na janga hili la corona, nchi zetu za Afrika tusimamie katika hili kuwaomba wakubwa hawa watusamehe madeni katika kipindi hiki kigumu cha kupambana na corona badala ya kutuongezea mzigo mwingine wa kukopa na huku wanataka ‘interest’,” alisema Rais Magufuli.
NJIA ZA ASILI
Rais Magufuli pia alishauri Watanzania kutumia njia nyinine za asili za kupambana na ugonjwa huo kama njia ya kujifukiza.
“Wizara ya afya iendelee kufafanua ni namna gani suala la kujifukiza linasaidia kudhibiti corona, ‘it is a scientific treatment’,” alisema.