27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atoa maagizo kwa mawaziri watatu

NORA DAMIAN-UVINZA

RAIS John Magufuli ametoa maagizo kwa mawaziri watatu akitaka yatekelezwe haraka ili Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma itoe huduma kwa ufanisi na kutatua kero za wananchi.

Mawaziri hao ni Seleman Jafo (Ofisi ya Rais – Tamisemi), Dk. Medard Kalemani (Nishati) na Inocent Bashungwa (Wizara ya Viwanda na Biashara).

Katika maagizo hayo, mawaziri hao wametakiwa kutekeleza kila mmoja kulingana na wigo wa wizara yake, huku wakiagizwa kuharakisha utekelezaji huo.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana akiwa njiani kuelekea mkoani Tabora akitokea Kigoma ambapo alisimama katika maeneo mbalimbali yakiwemo Kazuramimba, Uvinza, Mpeta, Nguruka, Kaliua na kuzungumza na wananchi.

Miongoni mwa changamoto kubwa katika maeneo hayo ni ubovu wa barabara, ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji, maji na uendelezaji wa kiwanda cha chumvi cha Uvinza.

Akizungumza na wananchi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea, Rais Magufuli alisema hajaridhika na kasi ya usambazaji umeme katika wilaya hiyo na kuahidi kuwa vijiji 61 ambavyo bado havijapata umeme vitapelekewa.

“Naseme kwa uwazi kwamba suala la umeme katika vijiji na wilaya ya Uvinza hatujafanya vizuri sana, nitawabana watu wangu na waziri wangu wa umeme kama anasikia aanze kutekeleza kwa sababu bado ni waziri.

“Mheshimiwa Waziri Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia) nataka ukamweleze Waziri Kalemani (Nishati) kwenye suala la umeme Uvinza sijafurahia, lakini nawaambia hivi vijiji 61 nitalibeba.

“Hatuwezi tukapeleka kwa miaka mitano vijiji 17 tu, tulitakiwa tuwe tumepeleka kwenye vijiji 61 vibaki 17 tu, hii ni kero lazima nibebe mimi mwenyewe,” alisema Rais Magufuli.

Kwenye miundombinu alisema barabara ya Uvinza – Malagarasi kilomita 150 itatengenezwa kwa kiwango cha lami na kwamba mwezi ujao zabuni itatangazwa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli zaidi ya Sh bilioni 51 ambazo zinatarajiwa kutatumika katika ujenzi huo zimetolewa na Quwait Fund na Opec Fund.

Pia alisema katika barabara ya Uvinza – Mjini ambayo awali ilipangwa kutengenezwa kilimota moja, aliagiza ziongezwe kilometa nyingine 9 na kumtaka Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais – Tamisemi), Seleman Jafo kutafuta Sh bilioni 5 za ujenzi huo.

“Nataka siku moja nikija kuweka jiwe la msingi niikute lami mpaka Uvinza, natoa maagizo Jafo uwaletee bilioni tano kuanzia Jumatatu ziwe zimeshafika Uvinza,” alisema Rais Magufuli wakati akizungumza kwa njia ya simu na Jafo.

Aidha alimuagiza Waziri Bashungwa (Viwanda na Biashara) kufuatilia kiwanda cha chumvi ili kiweze kuendelezwa kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Tuna kiwanda cha chumvi kikubwa sana tunataka tuki – promote kiwe kinauza mpaka Burundi, DRC na kwingine na vijana wetu wapate ajira, kwa hiyo, Waziri wa Viwanda naye hili akalibebe,” alisema.

MIRADI MINGINE

Rais Magufuli alisema pia bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh milioni 420.3 hadi Sh bilioni 4 sambamba na kutolewa Sh milioni 400 zilozowezesha ujenzi wa Kituo cha Afya Nguruka.

Kwenye sekta ya elimu alisema Sh bilioni 7.63 zimetolewa kwenye elimu bure wakati Sh bilioni 5.04 zimetumika kujenga mabweni, maabara, chuo cha Veta na miundombinu mingine ya elimu.

Aidha alisema Sh bilioni 11.06 zimetumika kwenye miradi ya maji ambapo mingine imekamilika na mingine inaendelea.

Aliyataja baadhi ya maeneo yaliyonufaika na miradi ya maji kuwa ni Nguruka, Ndagala, Lukoma, Kalia, Lubufu, Katete, Kazanza, Mwanila, Mugambazi, Kalenge, Mwakizenga na Kazuramimba.

Akiwa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, aliahidi kufufua reli ya kutoka Kaliua – Mpanda ili kuwezesha wananchi wafanye biashara vizuri.

Kwa upande wa maji alisema upo mpango wa kuyavuta kutoka Tabora – Urambo – Kaliua ili kumaliza changamoto ya uhaba wa maji wilayani hapo.

Kero nyingine ambazo aliahidi kuzishughulikia ni barabara ya lami Kaliua Mjini, mahakama ya wilaya, ofisi ya TRA, magereza ya wilaya, uhaba wa watumishi wa afya na barabara za vijijini ambazo nyingi huwa hazipitiki hasa wakati wa mvua.

Nyingine ni ujenzi wa barabara inayounganisha Kaliua – Katavi kilomita 423, uhaba wa masoko ya pamba na tumbaku na pembejeo za kilimo.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana, akiwa njiani kuelekea Tabora baada ya kufanya kampeni zake kwenye Mkoa wa Kigoma na kufanya shughuli za kiserikali, ambapo alikutana na Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimye.

Akiwa mkoani kigoma juzi, Rais Magufuli alisimamia makubaliano baina ya Tanzania na Burundi ambapo walikubaliana kushirikiana katika maeneo sita ya biashara, madini, nishati, ufugaji, usafirishaji na ulinzi na usalama kwa manufaa ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo baina ya Rais Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Burundi, Ndaishmiye yaliyofanyika Ikulu ndogo iliyopo mkoani Kigoma.

Alisema Tanzania imekuwa rafiki wa kweli na Burundi na kumshukuru Rais Ndaishmiye kwa heshima kubwa aliyoipa Tanzania kwa kuamua kuja kuitembelea tangu alipochaguliwa.

“Mazungumzo yetu yamekuwa mazuri sana, tumetoa maagizo tume ya kudumu ya mawaziri ianze kukutana kujadili masuala ambayo yako ‘pending’,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema biashara kati ya Tanzania na Burundi zimeongezeka kutoka Sh bilioni 115.15 (2016) hadi Sh bilioni 201.

Alisema pia Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 16 kutoka Burundi yenye thamani ya Dola milioni 29.42 ambayo imetoa ajira kwa zaidi ya watu 544.

Rais Magufuli alisema zaidi ya kampuni 10 kutoka Tanzania zimewekeza Burundi zikiwemo za Azam, Maxicom na Benki ya CRDB na kwamba asilimia 95 ya mizigo yote ya nchi hiyo husafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli mizigo ya Burundi inayosafirishwa kupitia bandari hiyo imeongezeka kutoka tani 379,704 hadi 481,081.

MAENEO SITA

Rais Magufuli alisema kupitia makubaliano hayo Burundi sasa itaweza kuuza madini yake ya Nico katika soko la madini lililopo mkoani Kigoma sambamba na kushirikiana kujenga mtambo wa pamoja wa uchenjuaji madini hayo.

Aidha kwenye eneo la miundombinu walikubaliana kuimarisha usafiri wa barabara, reli na bandari ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo.

“Tunaweza kujenga ‘narrow gaje’ kutoka Uvinza – Vitega ikaanza kutumika kusafirisha Nico, wataalam wa Tanzania wameweza kufufua reli karibu kilomita 1,000 hawawezi kushindwa kilomita 200.

“Tunataka tutengeneze ‘hub’ ya hapa Kigoma ili tuwasaidie wananchi wa Burundi waweze kufanya biashara na wenzao wa Tanzania, tumeiweka ‘centre’ ya biashara ambayo itaunganisha Burundi, Rwanda na DRC, hata bandari tutaipanua ili kubeba mizigo ya kutosha,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia suala la ombi la Burundi kujiunga SADC nalo litashghulikiwa.

Aidha marais hao waliagiza uhitishwe mkutano wa wataalam wa nchi hizo kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

“Wataalam wa wizara zinazohusika wakae na kujadili, tunakaribisha wafanyabiashara wa Burundi walete dhahabu yao wauze, huu ni wakati wa kujenga uchumi wa nchi zetu hizi mbili,” alisema Rais Magufuli.

RAIS NDAISHMIYE

Kwa upande wake Rais Ndaishmiye alisema anafurahishwa na ushirikiano uliopo wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ambao umekuwepo tangu enzi za baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Burundi tunasema kwamba Watanzania ni wazazi kwa sababu tangu zamani katika kupambania uhuru baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitusaidia.

“Wakati wa machafuko ya Burundi, Tanzania ilikubali kubeba msalaba, walipokea Warundi wengi wakimbizi na wale waliokimbia zamani walipata uraia. Mheshimiwa rais mimi nakuona kama baba yangu ndiyo sababu nimekuja kujifunza kwako ili nijue nafanya nini,” alisema Ndaishmiye.

Rais huyo alisema Burundi sasa kuna amani na kuwaomba raia wake waliopo hapa nchini kurudi wakajenge nchi yao.

“Warundi wote tulikaa pamoja tukazungumza tukagundua kwamba ni wazungu walitugawa, hatutarudia tena machafuko ya zamani, najua tukiwa na amani Burundi na Kigoma wana furaha kwa sababu tulikuwa tunawasumbua sana na wakimbizi,” alisema.

Pia alimualika Rais Magufuli kutembelea nchi hiyo pale atakapopata muda.

“Umeijenga Tanzania, umeibadilisha nina uhakika kwamba utashinda uchaguzi na Warundi wote wanakutakia kila la kheri kwa uchaguzi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles