29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli ataka haki itendeke Uchaguzi Serikali za Mitaa

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

WAKATI uandikishaji wa wapigakura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeanza rasmi jana, Rais Dk. John Magufuli amewataka wasimamizi wa uchaguzi huo kutenda haki ili wananchi wachague viongozi wanaowataka.

Alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kufika moja ya kituo cha kuandikisha wapigakura mkoani Rukwa.

Rais Magufuli ambaye yupo katika ziara ya kikazi mkoani humo, pamoja na kufika katika kituo hicho pia alizungumza na mawakala wa CCM na Chadema huku akiwapongeza.

 “Niwaombe wasimamizi wa uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, hakikisheni mnatenda haki kwa Watanzania wote bila kubagua vyama vyao kwa sababu uchaguzi huu ni wa kidemokrasia, ili watu wapate uhuru wao wa kuchagua mtu wanayemtaka katika viongozi wa Serikali za mita,” alisema Rais Magufuli.

Uandikishaji wapigakura ambao umeanza rasmi jana, utafanyika kwa siku saba katika mitaa yote hapa nchini, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Novemba 24.

WAKANDARASI WANAOHARIBU MIRADI YA MAJI

Akihutubia wananchi, Rais Magufuli pia alimtaka Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuwachukulia hatua wahandisi wanaoharibu miradi ya maji.

“Usiwahurumie wahandisi wanaoharibu miradi ya maji, kuwahurumia wahandisi wachache wanaoharibu miradi ni kuwahujumu wananchi wanyonge.

“Suala la umeme nasikia pia kuna matatizo naambiwa miradi wanapewa wakandarasi walewale, najua Mkuu wa Mkoa na Waziri wa Nishati mnanielewa,” alisema.

CHANGAMOTO YA UMEME

Aidha, alisema Serikali inatarajia kumaliza changamoto ya umeme kwa kila kijiji kupitia awamu ya tatu ya mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (Rea).

“Nia ya Serikali yangu ni kuleta maendeleo kwa kila mmoja, nataka watu watajirike, ukipata hela yako jenga na mimi hapa nimefurahi kila mahali pamejengwa nyumba.

“Nataka niwahakikishie kila mmoja atapata, nawaambia ukweli, najua kuna matatizo ya makandarasi na kuna mchezo mbaya unachezwa na baadhi ya watendaji wa Tanesco, watanikoma siku moja wataona,” alisema Rais Magufuli.

PORI LA AKIBA

Awali akizindua barabara ya Sumbawanga-Kanazi yenye urefu wa kilomita 75, Rais Magufuli alikataa ombi la wananchi wa kijiji cha Kanazi, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa la kutaka wapewe pori la akiba lililopo katika eneo hilo kwa shughuli zao za kilimo.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli ulitokana na mmoja wa wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo, kuinua bango lililoandikwa ‘ombi la eneo la kulima pori la akiba Lwafi Kakoma’.

Alisema hawezi kuruhusu wakalima kwenye pori la akiba kwa sababu mapori hayo ndiyo yanayoleta watalii nchini.

MIMBA ZA UTOTONI

Akizungumzia kuhusu mimba za utotoni ambazo mkoa huo unaongoza, aliwataka viongozi wote kulisimamia na kuwachukulia hatua wanaume ambao wanawapa mimba wanafunzi.

“Tumekuwa tukitoa fedha kila mwezi kwa ajili ya elimu bure. Tunafanya haya ndugu zangu kwa sababu tunatambua elimu ndio mkombozi wa maisha yetu, tatizo la mkoa huu inawezekana vyakula vipo mnashiba, mimba nazo zimeongezeka, watoto wetu 229 wamepata mimba.

“Lakini sijasikia wanaume 229 wamefungwa zaidi ya miaka 30, wakati sheria na mahakama ziko, polisi wapo, wakuu wa wilaya, mikoa, makatibu tarafa, madiwani na viongozi wengine wapo, hapo ndipo ninajiuliza maswali mengi kwamba hao waliowapa mimba ni hao viongozi?

“Kwa sababu kama sio wao walishindwa kitu gani kuwapeleka hao kwenye haki, niwaombe wananchi wa Nkasi tuwalee mabinti zetu, tusiwadanganye kwa fedha tunazozipata wakati hata kule nyumbani mkeo humnunuliagi nguo, niwaombe viongozi wa mkoa na wilaya mlisimamie hili, hii ni aibu,” alisema.

PONGEZI KWA MBUNGE

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimpongeza Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM), kwa utaratibu wake wa kutetea wananchi na kwamba ingewezekana wabunge wanabadilishwa majimbo, basi angempeleka katika Jimbo la Chato mkoani Geita.

“Ingekuwa inawezekana wabunge wanabadilishwa majimbo, basi ningesema Chato… sio kwamba kule hakuna mbunge mzuri, lakini wabunge wanaosema ukweli kama Keissy ni wachache.

“Niwaambie mna mbunge mzuri, mnamwona hapa anazungumza kwa dhati, ni wachache sana wa aina hii, amekuwa akiwakilisha mawazo ya wananchi waliomchagua kwenye Serikali,” alisema Rais Magufuli.

DC, RPC KULIPA NG’OMBE

Rais Magufuli ametoa siku tano kwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda na Kamanda wa Polisi wa Wilaya, kulipa Sh milioni 12.5 ya mama aliyeibiwa ng’ombe 25.

Alisema kwa kuwa walishindwa kulisimamia suala la mama huyo na kumsumbua hivyo wamlipe jumla Sh milioni 15 pamoja na fidia.

“Natoa maagizo wewe DC na RPC wilaya mzilipe hela kwa huyo mama na nawapa siku tano kwa sababu mmeshindwa kulisimamia hili, na naomba huyu mama alindwe,” alisema Rais Magufuli.

Awali mama huyo alisema aliibiwa ng’ombe 25 na baada ya mwizi kukamatwa na kufikishwa polisi, baadaye aliachiwa.

“Sisi tulibiwa ng’ombe, tukamkamata mwizi tukamfikisha polisi, wakampa siku mbili ili siku ya tatu tukalipane, ambayo kila ng’ombe walimpigia hesabu ni Sh 500,00 kila mmoja awe mkubwa au mdogo.

“Ikaonekana katika ng’ombe waliobiwa 25 jumla ikawa Sh milioni 12.5, tulivyoenda siku ya tatu tukakuta askari wamemwachia, wamemwekea dhamana, tukaanza kufuatilia, tumetembea sana hatukusaidiwa polisi, tukaenda kwa mkuu wa wilaya mara mbili hatukusaidiwa, tukaenda usalama hatukusaiwa,” alisema.

MBUNGE AFUNGUKA

Awali kabla ya uzinduzi huo, Keissy alisema wakandarasi wanashirikiana na baadhi ya watendaji na watumishi wa Wilaya ya Nkasi kutafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.

 “Mheshimiwa Rais, Serikali yako inaleta fedha, lakini makandarasi kwa kushirikiana na watumishi wako wanashirikiana kutuibia. Mkandarasi peke yake hawezi kuiba hela, ni watumishi wako ndio wanawasaidia,” alisema Keissy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles