24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI: AJALI IMEZIMA NDOTO

RAIS Dk. John Magufuli

 

 

Na AZIZA MASOUD,

RAIS Dk. John Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi wa darasa la saba, walimu wawili na dereva wa gari la Shule ya Lucky Vincent.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa, Rais Dk. Magufuli amesema ajali hiyo imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.

“Ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa …Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kwa sasa ni muhimu kuwaombea marehemu wote wapumzike mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huo wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nacho kimetuma salamu za rambirambi kwa familia na uongozi wa shule hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itikadi,  Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, ilieleza kuwa, chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali hiyo.

“Kwa majonzi makubwa tunatoa salamu za pole kwa wazazi, wanafunzi na uongozi wa shule hiyo pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa msiba huu mkubwa na wenye kutia simanzi na huzuni,” alisema Mrema.

Alisema chama hicho kitakuwa pamoja na familia za marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Mrema pia aliwataka wanachama wa chama hicho  na Watanzania bila kujali imani zao wawakumbuke wafiwa katika sala ama dua ili Mungu awatie ujasiri katika kipindi hiki kigumu.

“Hakika Taifa limepoteza watoto wake na vijana wa kesho ambao wangelitumikia siku zijazo,” alisema Mrema.

Mbali na hilo, chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo mbaya, ili matokeo ya uchunguzi huo yatumike katika kuzuia ajali nyingine kama hizo kutokea siku zijazo.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, akiitaja ajali hiyo kama pigo kwa Taifa.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Bunge Dodoma, ilieleza Spika Ndugai amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa  hiyo, iliyogharimu maisha ya watoto hao.

“Mkuu wa Mkoa nakupa pole sana, nimepokea kwa mshtuko taarifa hii ya ajali iliyogharimu maisha ya watoto wetu, hakika hili ni pigo kwa taifa zima, namuomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema Ndugai.

Ndugai pia alitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao, akiwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.

Kwa upande wa majeruhi, Ndugai pia amewaombea wapone haraka.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,  Edward Lowassa alisema alimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo.

 “Ni ajali mbaya iliyoifanya siku hii iwe mbaya katika historia ya nchi yetu.Nawapa pole wote waliopatwa na msiba huu mzito nawaomba Watanzania tukae pamoja na kusaidiana katika jambo lolote litakalopaswa kufanywa wakati huu mgumu kwetu sote,” alisema Lowassa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema), alisema, amepokea taarifa za kusitikisha kutoka kwa Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro juu ya kutokea kwa ajali hiyo iliyopoteza maisha ya watoto, walimu na dereva.

 “Taaraifa hizi zimenihuzusha sana ni taarifa mbaya kwa hakika sina lugha nyepesi ya kuzungumzia nimehuzunishwa sana kama kiongozi na Mbunge wao.

 “Natoa pole kwa walimu, wazazi walezi,  mmliki wa shule na wakazi wa Arusha jambo hili ni kubwa naomba Mungu awatie moyo na faraja hakuna maneno ya kibinadamu yanayoweza kuwatia faraja ndugu hawa zaidi ya Mungu mwenyewe.

“Niwape pole pia viongozi wenzangu waliokuwa Arusha kwa kufanya kazi ya ziada ya kuhakikisha miili ya wapendwa wetu inafikishwa Arusha. Watoto hawa wadogo walikuwa na mipango ya kuishi na malengo ya kufanya kazi siku zao za usoni,” alisema Lema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles