23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI 2, JK 13

Magufuli BarazaPATRICIA KIMELEMETA NA ELIZABETH HOMBO

RAIS Dk. John Magufuli ametangaza Baraza la Mawaziri ambalo lina jumla ya wizara 18 zenye mawaziri 19, huku wizara moja ikiwa na mawaziri wawili.

Katika uteuzi huo, mawaziri wateule 13 walikuwamo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, huku wapya wakiwa wawili ambao ni Balozi Dk. Augustine Mahiga na Nape Nnauye.

Kwa upande wa manaibu waziri, wengi ni sura mpya ambazo hazikuwamo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli, kutangaza baraza lake la mawaziri, sasa unavunja ukimya na maswali ya muda mrefu kuhusu uundwaji wa baraza hilo.

Rais Magufuli, amesema pamoja na hali hiyo hata akikamilisha uteuzi wa wizara nne zilizobaki, baraza lake la mawaziri litakuwa na mawaziri 34 tu tofauti na Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, iliyokuwa na mawaziri na manaibu waziri 60.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Magufuli, alisema uamuzi wa kupunguza baraza hilo ni pamoja na kupanga safu ambayo itafanya kazi kwa uadilifu, nidhamu na uwajibikaji kwa wananchi ili kuhakikisha wanapata maendeleo.

Alisema kitendo cha kuchelewa kutangaza baraza hilo ni kutaka kujiridhisha uadilifu wa viongozi waliochaguliwa ambao watafanya kazi kwa mujibu wa sheria ili waweze kuwatumikia wananchi.

“Nimetumia siku 30 kwa ajili ya kuwafuatilia, kuwachunguza na kujiridhisha kuwa watu niliowachagulia ni waadilifu kiasi gani, ndiyo maana nimechelewa…lakini nilitakiwa kuwatangaza mapema. Nilishindwa kufanya hivyo kwa sababu nilikuwa nataka nihakikishe kama ni kweli wanaweza kufanya kazi nasi,” alisema Dk. Magufuli.

Pamoja na hali hiyo, Rais Magufuli, alisema amelazimika kuunganisha baadhi ya wizara kama njia ya kuleta ufanisi kwa mawaziri wake.

Alitaja wizara hizo pamoja na mawaziri wake kuwa ni Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, ambayo itaongozwa na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene na Angela Kairuki, huku Seleman Jaffo, akiteuliwa kuwa naibu waziri.

Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) aliyeteuliwa ni January Makamba, huku naibu wake akiwa Mbunge wa Kisesa, mkoani Simiyu, Luhaga Mpina.

Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) itaongozwa na Jenister Mhagama akiwa na naibu mawaziri wawili ambao ni Mbunge mteule Dk. Abdallah Possi na Anthony Mavunde.

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,  itaongozwa na Mbunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba, huku naibu wake ni William Ole Nasha, wakati Wizara ya Nishati na Madini itaongozwa na Waziri wa zamani wa wizara hiyo ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya Escrow, Profesa Sospeter Muhongo na naibu wake ni Dk. Merdard Kaleman.

Wizara ya Katiba na Sheria itaongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, wakati Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ikiongozwa na Mbunge mteule, Dk. Augustine Mahiga huku naibu wake akiwa ni Dk. Susan Kolimba.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (TPDF) itaongozwa na Dk. Hussein Mwinyi, huku Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikiongozwa na Naibu Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaongozwa na William Lukuvi na naibu wake ni Angelina Mabula.

Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto,  itaongozwa na Ummy Mwalimu na naibu wake ni Dk. Hamis Kigwangallah.

Katika uteuzi huo wa Rais Magufuli, amemteua Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, ambaye pia ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye, kuongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, huku naibu wake akiwa Anastasia Wambura.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itaongozwa na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage.

Wizara ya Maji na Umwagiliaji aliyeteuliwa kuiongoza ni Mbunge mteule Profesa Makame Mbarawa Mnyaa na naibu wake ni Mhandisi Isack Kamwela.

 

WIZARA NNE ZAKOSA MAWAZIRI

Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo jambo ambalo limemfanya kuteua manaibu waziri huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye.

Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo Naibu ni Dk. Ashatu Kijaji.

Wizara nyingine ambazo hazina mawaziri ila zina manaibu waziri ni Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo aliyeteuliwa ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa jimbo jipya la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.

 

PANGA LA MAKATIBU WAKUU

Rais Magufuli alisema kupunguzwa kwa wizara katika Serikali ya awamu ya tano kutasaidia kupunguza idadi ya makatibu wakuu wa wizara.

 

SEMINA ELEKEZI ‘STOP’

Alisema viongozi waliochaguliwa wanapaswa kufanya kazi bila ya kuwapo kwa semina elekezi ili waweze kuleta tija kwa wananchi.

Alisema kutokana na hali hiyo, Sh bilioni 2 zilizotengwa na Utumishi kwa ajili ya semina hiyo, zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine ikiwamo ya ununuzi wa madawati.

Rais Magufuli alisema viongozi hao watakapoapishwa wanapaswa kuanza kazi mara moja ili kuhakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi.

“Si wakati wa kufanya sherehe, anayetaka kufanya hivyo ajiandae na siku ya kufukuzwa akafanye sherehe…naendelea kusema kuwa mkakati wangu ni kazi tu, na si mchezo, tufanye kazi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kutokana na hali hiyo, mawaziri hao watakapoapishwa moja kwa moja wanapaswa kwenda kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya kuwajibika.

Akitolea mfano wa yeye pamoja na makamu wake, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kuwa walipoapishwa walianza kufanya kazi bila ya kupewa semina elekezi.

“Hakuna umuhimu wa kuwapo kwa semina elekezi, hayo mambo watajifundisha wenyewe uko kazini, kwani nilivyomteua Waziri Mkuu alijielekeza mwenyewe kwenda kwenye makontena na Makamu wa Rais, alijieleza kwenye usafi,” alisema.

Dk. Magufuli alisema mkakati wake ni kuhakikisha kuwa fedha zinazookolewa baada ya kupunguzwa kwa baraza hilo zinatumika kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.

 

MASWALI NA MAJIBU KWA DK. MAGUFULI

Yafuatayo ni maswali na majibu, ambayo aliulizwa Rais Magufuli na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutangaza baraza hilo.

Swali: Kuna baadhi ya wizara haukutaja mawaziri wake, tatizo ni nini kwa mawaziri hao kutowateua? Je, wabunge wa chama chako hawana sifa? Na baadhi ya wizara zinatakiwa kuhamia Dodoma ukiondoa TAMISEMI je, utekelezaji wake ukoje?

Magufuli: Nilitegemea ungeniuliza kwanini sikuteua siku niliyoapishwa, subira yavuta heri, hawa wameanza na wengine watafuata. Ninawaambia msiwe na haraka. Kuhusu Dodoma tutatekeleza yaliyoko kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Swali: Umesema hakutakuwa na semina elekezi, utafanya nini ili mawaziri wapya waweze kwenda na kasi ya hapa kazi tu?

Magufuli: Niliowachagua wote ni wana CCM na wengi wao ni wabunge, walinadi sera ya CCM na hapa kazi, ndiyo maana hakuna haja ya kuwapa semina elekezi, watakwenda kujifundisha wenyewe kwenye ofisi zao, spidi ni hiyo hiyo, hatutatumia semina elekezi ya Sh bilioni mbili, fedha hizo bora zikatumike kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo.

Swali: Kwa kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri na kwa kulinganisha na tulipotoka, Serikali itakuwa imepunguza kiasi gani cha fedha?

Magufuli: Wewe ndio utapiga hesabu, kwa vile ni mmiliki wa gazeti huwa unapiga hesabu unapata kiasi gani. Utanisaidia katika kupunguza baraza tutakuwa tumeokoa kiasi gani na zile tulizookoa za semina elekezi, kuchelewa kutangaza baraza na wale ambao sijawataja na bahati nzuri nyie waandishi mnaweza kupiga hesabu vizuri.

Zipo nchi zina mawaziri wengi mpaka kufikia hata 70, wizara 44, manaibu na mawaziri. Nilijua ungeniuliza hilo swali maana nimekuja na kitabu hiki ningekupa ukasome, ila tutakapomaliza tutakuwa na baraza la watu 34 tu.

Wakienda kule mawaziri wakafanye kazi, tena kazi kweli kweli ndiyo maana sisi tulipochaguliwa tulifanya kazi kweli na hatukwenda kwenye semina elekezi na tulijielekeza, wakajielekeze wenyewe kwenye maeneo yao.

Wasihangaike kufanya sherehe kwa sababu ni kazi ngumu na hapa wamepata kazi wanatakiwa kufanya kazi, kama wapo wanaopenda kufanya sherehe wajiandae kufanya sherehe siku wakifukuzwa, contract (mkataba) ni miaka mitano ya kuwatumikia wananchi.

Wakawafanyie kazi Watanzania bila kuwabagua kikanda wala kikabila bali wanapaswa kufanya kazi kwa bidii.

Baraza hili la wizara 18 tumejiridhisha linaweza kufanya kazi tunayowatarajia kuifanya effectively. Ngoja tukimaliza uteuzi wote tutajua tume-save (tumeokoa), kiasi gani ili ziweze kwenda kwa wananchi.

Swali: Siku saba zimetimia, wafanyabiashara wamesharudisha zile fedha kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)?

Magufuli: Swali hilo kamuulize Kamishna wa Kodi TRA.

Swali: Kuna wizara ina mawaziri wawili, kuna kazi gani ngumu?

Magufuli: Kafanye utafiti hiyo wizara utapata jibu, tena unaona imeunganisha wizara ngapi.

Swali: Katika baraza, kuna mawaziri wa baraza lililopita, ulizingatia nini wakati wa uteuzi?

Magufuli: Umekosea hata kupiga hesabu, kafanye hesabu vizuri, waliorudi ni saba na sio kumi, ukipiga utaelewa ni vigezo gani nilivyotumia.

KUAPISHWA KESHO

Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya Rais ikulu na kaimu mkurugenzi, Gerson Msigwa, ilisema kuwa Mawaziri na manaibu waziri wataapishwa kesho ikulu jijini Dar es salaam kuanzia saa tano asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles