Veronica Romwald, Kenya
Magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu imetajwa kuwa tishio kwa maendeleo ya ustawi wa jamii na uchumi wa mataifa mengi Barani Afrika hasa yaliyopo Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.
Aidha, pamoja na magonjwa hayo, nchi zilizopo katika ukanda huo zinakabiliwa pia na majanga mengine ya kiasili kama vile ukame, mafuriko na migogoro.
Hayo yameelezwa jijini Nairobi na Ofisa Mfuatiliaji wa Masuala ya Majanga na Dharura wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO-Kenya), Dk. James Kojo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari za afya kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Cameroon, Ghana, Zambia, Ethiopia na Mozambique.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wa jinsi ya kukusanya taarifa kutoka kwa vyanzo sahihi ili kutoa taarifa sahihi kwa jamii kuhusu magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
“Kati ya majanga ya dharura 100 yanayotajwa kila mwaka katika Ukanda huu, mengi huhusisha masuala ya mlipuko ambayo huhitaji ufumbuzi wa haraka.
“Serikali pekee kupitia Wizara ya Afya haziwezi kufanya kazi peke yake kukabili magonjwa na kwamba waandishi wa habari wana nafasi kubwa kushirikiana nao kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi ili kusaidia jamii.
“Naamini semina hii itawasaidia kupata maarifa namna gani mtazidi kutoa habari sahihi kwa umma ili kwa pamoja tuweze kuokoa maisha kwa sababu sisi WHO kazi yetu ni kutoa takwimu lakini hatuwezi kusimulia habari lakini ninyi mnao uwezo huo ni muhimu kuhakikisha mnakusanya taarifa kutoka kwa vyanzo sahihi ili kuisaidia jamii hasa jinsi ya kuepuka magonjwa haya,” amesema.
Hivi karibuni Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema visa vya watu kupata maambukizi ya kipindupindu vimeendelea kuripotiwa katika baadhi ya mikoa.