NEW YORK, MAREKANI
MAGAZETI ya Marekani jana yalijibu mashambulizi ya kila mara ya Rais Donald Trump dhidi ya vyombo vya habari, kwa kuzindua kampeni iliyoratibiwa ya kuchapisha tahariri zinazosisitiza umuhimu wa uhuru wa habari.
Gazeti la The Boston Globe ndilo liliongoza kampeni hiyo, likitumia kaulimbiu ya #EnemyofNone, yaani Sio Adui wa Yeyote, na kuungana na magazeti mengine 200 kote Marekani.
Tahariri ya gazeti hilo imesema Marekani kwa sasa ina rais ambaye amejenga dhana kuwa waandishi wa habari ambao hawaungi mkono sera za utawala wa sasa, ni maadui wa wananchi.
Gazeti hilo lilionya kuwa mbinu anayotumia Trump dhidi ya waandishi wa habari pia inawatia moyo viongozi aina ya Vladimir Putin wa Urusi na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, wanaofahamika kuwachukulia waandishi wa habari kuwa maadui.
Kwa hivyo Trump anaungana na viongozi wa kiafrika katika kupinga waandishi wa habari. Yawezekana si sahihi kwa kila habari kuchapishwa au kutangazwa ila kwa sababu ya hili neno ‘demokrasia’ dunia inaendelea kuhadaiwa kuwa demokrasia maana yake ni kumwaga hadharani kila kitu.