27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Maendeleo yanaibua changamoto mpya za malezi

CHRISTIAN BWAYA

KAMA kuna wakati tumeshuhudia upatikanaji wa maarifa na utaalamu mwingi kuhusu malezi ya watoto, ni sasa. Suala la malezi limekuwa likipewa uzito mkubwa kuliko ilivyowahi kuwa katika kipindi cha nyuma.

Sambamba na ongezeko la mijadala ya malezi katika majukwaa mbalimbali, eneo la malezi limevuta hisia za watafiti wengi kuliko ilivyopata kuwa. Kila siku, kwa mfano, zinachapishwa tafiti nyingi kujadili masuala yanayohusu malezi ya watoto.

Jambo hili linaweza kumtia wasiwasi mfuatiliaji makini wa mambo. Kwamba, iweje kuwe na msisitizo huu mkubwa katika malezi? Iweje wazazi wetu ambao ‘hawakufundishwa’ namna ya kulea waliweza kutulea vizuri? Kwanini sasa hivi pamoja na kuwapo kwa kila namna ya maarifa ya kimalezi kwa wazazi wa kisasa bado changamoto za malezi zimeendelea kuongezeka kuliko ilivyokuwa hapo zamani?


Jibu la swali haliwezi kuwa jepesi. Hata hivyo, kuna ukweli kuwa mfumo wa maisha tunayoishi katika siku za leo unaathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyolea watoto wetu. Kwa mfano, leo hii ni jambo la kawaida kwa wazazi kutumia muda mrefu kuwa mbali na familia zao.

Kazi zinachukua muda mrefu wa wazazi kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.
Wakati zamani katika familia nyingi za kawaida baba na mama waliishi sehemu moja, siku hizi mambo yamebadilika. Huwezi kushangaa, ukisikia mume anaishi Mwanza, wakati mama anafanya kazi mkoani Lindi.

Katika mazingira haya, wazazi hawa wanaweza kukutana kwa nadra na hata kuchukua miezi kadhaa kabla mzazi mmoja hajapata muda wa kwenda kusalimia familia yake inayoishi mbali naye. Jambo hili halikuwahi kuwa sehemu ya maisha katika siku za nyuma.


Kadhalika, katika familia nyingi za kawaida, mama alitarajiwa kuwa nyumbani muda mwingi kulea watoto. Wanawake wengi, kwa kawaida, hawakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuwatunza watoto. Kazi ya kutafuta mkate wa familia ilikuwa ni ya wanaume.

Watoto walilelewa kwa karibu na mama tangu wakiwa wadogo hadi walipofikia umri wa kuondoka nyumbani na kujitegemea.
Siku hizi mambo yamebadilika, akina mama wameondoka nyumbani kuungana na wanaume kuongeza kipato cha familia.

Dhana kuwa mwanamke ni mama wa nyumbani inafutika. Si wanawake wengi walio tayari kuwa ‘mama wa nyumbani’ kulea watoto kama ilivyopata kuwa katika siku za nyuma.


Mwanamke kufanya kazi, kwa hakika si jambo baya. Jitihada za kubadili mitazamo ya wanajamii ili waweze kuwasomesha watoto wa kike zinaenda sambamba na fursa ya ajira sawa na mwanamume. Ndio kusema, kama mwanamume anaweza kuajiriwa, haileti maana kufikiri kuwa mwanamke anapaswa kubaki nyumbani kufanya kazi za ndani kama ilivyokuwa imezoeleka hapo zamani.


Katika ajira, wanawake wameonesha uwezo wa kumudu majukumu yao sawa na wanaume. Karibu kila sekta hivi sasa wapo akina mama. Wanawake wanaonesha uwezo mkubwa. Wanashika madaraka makubwa makazini na wanafanya vyema, tena wakati mwingine kuliko wanaume.


Hata hivyo, mafanikio haya ya akina mama kikazi yametikisa maeneo mengine ya kijamii. Malezi ni eneo moja wapo kubwa lililokumbwa na tetemeko kubwa tangu akina mama walipoanza kuondoka nyumbani kuelekea makazini.


Kuanzia juma lijalo tunakusudia kujadili changamoto hizo katika safu hii na kujaribu kuangalia kile kinachoweza kufanyika.
Itaendelea…

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles