28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Kudekeza watoto ni kuwaharibia maisha yao baadae

MWANDISHI WETU

MALEZI ni suala gumu mno, kama mzazi hatokuwa makini anaweza kujikuta akimharibu mwenendo mzima wa mtoto.

Kuna watu wengi ambao watoto wao huharibika kutokana na kulelewa vibaya na wazazi wao.

Si jambo baya kwa mzazi kumpenda mtoto, lakini anapompenda kupita kiasi anaweza kujikuta akimharibu badala ya kumjenga.

Kuna watoto ambao katika makuzi yao walidekezwa kupita kiasi, na hivyo walipokuwa watu wazima wakajikuta wakishindwa kumudu kujitegemea.

Ninao mfano hai wa watoto wa aina hii.

Kuna familia moja ilikuwa ikidekeza mno watoto, walipofikisha umri wa kujitegemea walishindwa.

Unaweza kukuta mtoto hataki kuajiriwa wala hataki kuwa na familia inayoeleweka.

Kijana wa miaka 39 anaweza kuendelea kuishi kwa wazazi wake, na akajikuta akizalisha tu wanawake bila mpangilio maalum.

Kwa vyovyote vile, unapofikia umri wa utu uzima mzazi ungetamani kuona watoto wako wakifanikiwa. Wakifanya kazi na kuwa na familia yenye furaha. 

Unaweza kujiuliza, vijana wakubwa namna hii hakuna kitu wanafanya. Uwezo wa kufikiri kuhusu maisha hawana licha ya shahada walizonazo.

Mtu huwezi kuwa na amani kuwa na watoto wakubwa wasiojua kutafuta fedha na kujitegemea. Hata wanapokabidhiwa biashara waziendeshe, wanazifilisi.

Kwa ujumla, vijana wa aina hii huwa hawafahamu vema maisha, walitegemea kupata mahitaji yao mengi kwa wazazi, ambao kimsingi ni zamu yao sasa kutunzwa na watoto wake. Je, nini kimefanya watoto wawe na uzembe wa kiwango hiki?

Kuna ukweli kwamba watoto wanaokulia katika mazingira yenye kila kitu wanakuwa kwenye hatari ya kunyimwa changamoto. Wanakulia kwenye mazingira ambayo karibu kila wanachokipata kinapatikana. Mtoto akiomba fedha za matumizi, hakosi. Mzazi anaamini kwa kumpa kila anachokihitaji basi mtoto atakuwa na utulivu wa kujifunza maisha.

Hata hivyo, watoto hawa mara nyingi wanakuwa tofauti na wenzao wanaokulia kwenye maisha ya uhitaji. Shida ya kukosa mahitaji ya kila siku, shida zinazomfanya ajione mtu duni akilinganisha na wenzake wenye nafuu zinaweza kuwa motisha kubwa ya kumsukuma kijana kupanua ufahamu wake. Shida zinakuwa mwalimu wa maisha ya mtoto. 

Tunawafahamu watu wengi waliokulia kwenye familia duni lakini waliweza kufika mbali. Watu hawa walikosa ada ya shule, walibangaiza fedha za matumizi lakini kupitia changamoto hizi wakajifunza namna ya kupangilia matumizi, namna ya kuishi na watu ili kupata msaada na hata kujifunza uvumilivu mambo yanapokuwa magumu.

Ipo sababu ya mzazi mwenye mafanikio kumsaidia mtoto kutafuta maisha yake, badala ya kumpa kila senti anayohitaji, mathalani, ni vizuri kumtengenezea mtoto upungufu kidogo utakaomsaidia kujenga nidhamu ya kile alichonacho. Kwa kufanya hivi, mtoto atajifunza namna ya kukabiliana na upungufu, hali itakayomfunza upande wa pili wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles