ACCRA, Ghana
MELFU ya waombolezaji na viongozi mbalimbali wa serikali wa nchi za nje na wa hapa na wa jadi, walijitokeza kuuaga mwili wa Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan ambaye alizikwa jana.
Shughuli hizo za mazishi zilifanywa na ndugu na jamaa wa karibu na kwa heshima zote za kijeshi.
Mwili wa kiongozi huyo, uliwasili mwanzoni mwa wiki nchini hapa ukitokea Uswisi tayari kwa mazishi.
Annan ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ambaye pia ni kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kushika wadhifa huo, alifariki Agosti 18, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 80, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kabla ya mazishi hayo, jeneza lililohifadhi mwili huo, likiwa limefunikwa kwa Bendera ya Taifa ya Ghana, lilipelekwa katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano nchini hapa ambapo viongozi na wananchi waliweza kutoka heshima zao za mwisho.
Kwa muda wa siku mbili zilizopita, mwili wa kiongozi huyo ulikuwa ukiagwa na watu mbalimbali, wakiwamo watu maarufu.
Viongozi kadhaa wa nchi walihuduria mazishi hayo yaliyofanyika katika makaburi ya jeshi ya Kambi ya Burma, mjini Accra.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) aliyeko mjini hapa, alisema kwamba ngoma za maombolezo zilisikika mfululizo kwa muda wa siku mbili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Accra, sehemu ambayo mwili wake ulikuwa ukiagwa na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa waombolezaji viongozi ambao walihudhuria mazishi hayo ni Graca Machel aliyewahi kuwa mke wa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Marais na viongozi kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika, ikiwamo Ivory Coast, Ethiopia na Zimbabwe, walihudhuria shughuli hizo za mazishi, wakiwamo pia marais wa zamani kutoka nchi za Ujerumani, Finland na Uswizi.