28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Madudu elimu ya msingi

Pg 1Na Mariam Mkumbaru, Dar es Salaam
KATIKA hali isiyo ya kawaida, zaidi ya wanafunzi 459 wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Saku iliyopo Chamazi, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wanasoma katika darasa moja.
Hali hiyo ya wanafunzi kusoma katika darasa moja na wengine chini ya miti inayozunguka shule hiyo, inachangiwa na upungufu wa majengo ya shule hiyo ambayo ina vyumba saba vya madarasa huku ikiwa na zaidi ya wanafunzi 2,038.
Akizungumza na MTANZANIA ambayo ilifika shuleni hapo na kuona hali halisi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Saku, Salome Munisi, alisema shule yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa madarasa pamoja na wingi wa wanafunzi kuliko uwezo wa vyumba vya madarasa walivyonavyo.
Munisi alisema idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka huu ni kubwa kuliko darasa la pili ambalo lina wanafunzi 436, wakiwamo wanaume 217 na wasichana 219.
“Darasa la tatu wako 372, darasa lenye wanafunzi wachache ni darasa la saba ambalo kuna wanafunzi 225 kwa darasa moja.
“Kipindi cha mitihani inabidi wanafunzi wafanye mtihani chini ya mti kwa sababu wako wengi darasani, huwezi mwalimu kuwapa mtihani watatizamiana na itakuwa ngumu kupima kiwango cha elimu kwa wanafunzi kwa sababu watajaza majibu yote yanayofanana,” alisema mwalimu Munisi.
Aidha alisema kwa sasa kuna walimu 30 ambao hawatoshi kufundisha wanafunzi wote hao, na kwamba wanahitaji walimu 52, huku madawati yaliyopo kwa sasa ni 193 wakati mahitaji ya madawati ni 1,845 na vyumba sita vya madarasa vya haraka vijengwe ili kipindi hiki cha mvua wanafunzi wasiache kusoma.
Akizungumzia hali hiyo, mwalimu Rose Mabina ambaye anafundisha darasa la awali shuleni hapo, alisema shule hiyo ilianza mwaka 2008, lakini tangu kipindi hicho amekuwa akifundisha chini ya miti.
“Mvua zikianza nakwenda likizo bila ya malipo kwa sababu hakuna mahali pa kukaa kujificha na mvua na watoto wakaweza kusoma na kuelewa kwa umakini, hata mvua zilizoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana wanafunzi wameshindwa kufika shuleni kwa sababu ya hofu ya kunyesha mvua tena wakiwa hapa shuleni,” alisema Mwalimu Mabina
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Manispaa ya Temeke, Honorina Mumba, alikiri kuwapo kwa changamoto kwa shule hiyo.
“Pamoja na hali hiyo, lakini pia changamoto hizo sio kwa Shule ya Saku tu, kuna shule za Mkundi, Kijaka na Bohari nazo hali yake ni mbaya sana,” alisema Mumba.
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda, ambaye alisema ili kuinua ubora wa elimu nchini ni lazima Serikali ijipange vizuri ili kuweka mazingira sawa katika kupata elimu bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles