BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, limewafukuza kazi watumishi wawili wa Idara ya Fedha na biashara pamoja na ofisa mipango, ufuatiliaji na takwimu kwa makosa mbalimbali.
Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Juma Kimisha alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kikao cha Baraza la Madiwani kujigeuza kamati na kujadili mienendo ya watumishi hao wa kazini ikiwa ni pamoja na nidhamu yao kutokana na kutuhumiwa kuhusika tuhuma mbalimbali ambazo hakuzitaja.
Kimisha aliwataja watumishi hao kuwa ni Stephano Fanuel Nyeliga ambaye alikuwa mkuu wa idara ya fedha na biashara, aliyekuwa akikabiliwa na makosa sita baada ya kusikilizwa alipatikana na hatiya ya makosa matano.
Mtumishi mwingine, ni  Mkuu wa Idara ya Mipango, Ufuatiliaji na Takwimu, Fredrick Summa ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa sita na kutia hatiani na makosa matano kati yake hivyo kwa pamoja walifukuzwa kazi na baraza hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Michael Matomola akizungumzia uamuzi huo, alisema Serikali inataka watumishi wadilifu, haina utani na mtumishi yeyote katika utekelezaji wajibu wake na kuwaonya wazembe.
Alisema wamefikia hatua hiyo kwa watumishi hao ili kujenga uwajibikaji wa kazi na kuwahakikishia watumishi hao waliofukuzwa kazi kuwa watalipwa stahiki zao wanazostahili katika muda wote walipokuwa kazini.