Fransic Godwin -Iringa
MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa, wamemuondoa meya halmashauri hiyo, Alex Kimbe, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kura za kutokuwa na imani naye 14 kati ya 26 .
Kikao hicho cha kumuodoa kilifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo wajumbe walikuwa wakiingia kwa barua maalumu ya mwaliko.
Mwenyekiti wa kikao hicho Joseph Ryata ambae ni Naibu Meya akitangaza matokeo ya kura, alisema kura zilizopigwa ni 26 ambapo 12 ziliharibika na 14 zilimtaka Kimbe kuondolewa katika nafasi yake .
“Ndugu wajumbe zoezi letu la mchakato wa kupiga kura za kumwondoa Meya Kimbe madarakani limekwenda vizuri baada ya wajumbe wote 26 kushiriki kupiga kura za kutokuwa na imani na meya na matokeo kura zilizoharibika ni 12 na kura za hapana hakuna na za ndio ni 14.
“Hivyo natangaza rasmi matokeo ya kura zilizopigwa waliosema ndio meya aondoke madarakani wameshinda hivyo natangaza rasmi kuwa Alex Kimbe kuanzia leo (jana) Machi 28 mwaka 2020 sio msitahiki meya tena wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa hadi kufikia hapa kikao kimefungwa,” alisema Ryata.
Akizungumza baada ya kutangawa kuondolewa madarakani Kimbe alisema yeye bado ni meya wa kwani kikao hicho kimeshindwa kuffikisha mbili ya tatu ya wajumbe wote wote 26 waliopaswa kupiga kura.
“Wameshindwa kunitoa katika nafasi yangu kwa sababu wameshindwa kufikisha mbili ya tatu ya wajumbe wote kama ambavyo kanuni inasema, theluthi mbili wajumbe wote katika Halmashauri ni 17 leo tulikuwa madiwani 26 lakini ili meya ama mwenyekiti wa Halmashaurti aweze kuondoka kanuni ipo wazi kuwa wajumbe mbili ya tatu ndio wanapaswa kumwondoa na waliopiga kura za kuniondoa ni 14 ilipaswa wawe 17 hivyo mimi bado meya “
Aidha alisema katika kikao hicho wakati ikisomwa taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake alinyimwa haki ya kujieleza.
Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema mbinu ambayo waliitumia kupiga kura ni mbinu kabambe ya kubaini wasaliti ndani ya Chadema baada ya kupata taarifa za ndani kutoka CCM kuwa kuna mbinu ya kuwanunua madiwani watatu ama zaidi ili wapige kura za kumwondoa meya.
” Tulitaka kura zetu 12 kuwa salama bila kununuliwa lakini wakati huo huo sio kwamba hizo kura kura 12 hazijapigwa zimepigwa hivyo kura zilizopigwa ndani ya ukumbi ni kura 26 na zilizomtaka meya aondoke ni kura 14 za CCM na 12 ni kura zilizoharibika.
“Kanuni ipo wazi inamtaka meya kuondoka kwa theluthi mbili ya kura zilizopigwa si vinginevyo, walihitaji kura nyingine tatu ambazo hawajazipata ” alisema Msigwa .
Kwa upande wa diwani wa CCM, Nguvu Chengula na Ibrahim Ngwada, alisema Chadema walikuwa wametengeneza mbinu ya kutopiga kura imekwama baada ya zoezi hilo kufanyika kwa mafanikio.
Alisema kitendo cha madiwani kutopiga kabisa kura kimetoa nafasi ya meya kuondolewa kwani walipaswa kupiga kura za hapana na sio kutopiga.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Nicholaus Mwwakasungura, alisema kitendo ambacho wamekifanyha Chadema kutopiga kura ya hapana ama ya ndio, kimetengeneza mazingira ya kuonesha kura za hapana zimeshinda katika mchakato huo.
“Kwa matokeo haya ni wazi
kuanzia Machi 28 Meya Kimbe
ameondolewa madarakani na sio meya tena wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na anapaswa kukabidhi
ofisi.
“Imebainika Kimbe anamiliki mali ambazo haziendani na kipato chake kwani kipato chake kwa mwaka ni Sh milioni 15 fedha
inayohusisha posho za
vikao, posho ya madaraka, takrimu
na posho za vikao na shughuli za kilimo, duka la vipuri na biashara
ya wakala wa voda ni vyanzo
hafifu vya mapato ya meya huyo kuweza
kumiliki mali hizo,” alisema.
Alisema timu ya uchunguzi ilibaini kuwa anamiliki shamba lenye ekari 30 lililopo katika mataa wa Chautinde Kata ya Isakalilo, shamba la ekari 35 lililopo Pawaga ambalo analitumia katika kilimo cha Mpunga na Shamba la ekari tisa lililopo Pawaga ambalo analima mpunga.
Pia alisema anamiliki shamba ekari sita mtaa wa Kitasengwa kata ya Isakalilo na mashamba mengine yaliyopo Kilolo na nje ya mkoa wa Iringa, nyumba tatu, gari aina ya Nadia ambavyo vyote hivyo alipata kati ya mwaka 2015 na 2020 kipindi akiwa Meya
Alisema walibaini pia kuwa ana eneo jingine la Chautinde lenye ekari 25 maeneo hayo yapo ndani ya kata anayoiongoza ya Isakalilo Manispaa ya Iringa.
” Imebainika kuwa meya Kimbe anamiliki mali ambazo haziendani na kipato chake kwani kipato chake kwa mwaka ni wastani wa shilingi milioni 15 fedha inayohusisha na posho za vikao, posho ya madaraka,takrimu pamoja na posho za vikao na shughuli za kilimo ,fuka la vipuri na biashara ya wakala wa VODA ni vyanzo hafifu vya mapato ya meya huyo kuweza kumiliki mali hizo .