25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Madereva wa daladala Moshi wagoma

daladala MoshiNa UPENDO MOSHA, MOSHI

MADEREVA wa daladala zinazosafiri maeneo ya Kiboriloni, Soweto, Majengo, KCMC na Pasua katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimegoma kwa muda usio julikana.

Madereva wa daladala hizo waligoma kuanzia jana asubuhi ili kuishinikiza Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kuondoa usafiri wa bajaji katika barabara wanazotumia.

Pia, madereva hao wanalalamikia uamuzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kuzuia uegeshaji wa magari katika Kituo cha Mbuyuni walichokuwa wakikitumia bila kuwaonyesha kituo kingine mbadala.

Kutokana na mgomo huo, mamia ya wakazi wa Manispaa ya Moshi, walikuwa na wakati mgumu wa kusafiri na hivyo baadhi yao kulazimika kutumia bodaboda na wengine kutembea kwa miguu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya madereva hao walisema wameamua kugoma baada ya kutoridhishwa na uamuzi uliochukuliwa.

“Tumegoma kwa sababu mamlaka haziwezi kuruhusu bajaji zitumie njia tunaoztumia wakati zikijua zinaathiri biashara zetu.

“Pia tunapinga uamuzi wa Halmashauri ya Manisapaa ya Moshi, kutuondoa katika kituo chetu cha kuegesha mabasi kwa ajili ya kupisha wateja wa Benki ya CRDB na kibaya zaidi hawajatuonyesha kituo kingine mbadala,” alisema mmoja wa madereva hao bila kutaja jina lake.

Naye Abdallah Juma ambaye ni dereva wa dalala za KCMC, alisema usafiri wa bajaji umekuwa ni kero kwao kwa sababu zinabeba abiria wao.

William Shakaza, alisema bajaji katika njia ya KCMC ni zaidi ya 40 na kwamba zimekuwa zikivunja sheria za barabarani ingawa polisi hawawachukulii hatua wahusika.

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkoa wa Kilimanjaro, Thadei Mwita, alisema malalamiko ya madereva hao ni ya msingi na kwamba wanaangalia jinsi ya kuyatatua.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa, alithibitisha uwepo wa mgomo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles