Editha Karlo – Kibondo
SHIRIKA la Madaktari wasiyokuwa na Mipaka la Umoja wa Mataifa (MSF), linalotoa huduma katika makambi ya wakimbizi ya Nduta na Mtendeli mkoani Kigoma, limejipanga kupambana na maambukizi ya virusi vya ugonjwa corona ili kuhakikisha havisambai.
Mratibu wa shirika hilo ofisi ya Kigoma, Maclle Homme aliyasema hayo jana, wakati wa kikao cha kamati ya afya ya msingi wilayani Kibondo.
Alisema wanayo timu ya dharula iliyopewa mafunzo maalumu, iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa ebora,sasa iko tayari kwa ajili ya kudhibiti corona
‘’Wote tunafahamu hali halisi inayoikabili dunia, virusi vya corona,tunaendeleza nguvu huko na tuko tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kusaidia kuzuia maambukizi kuanzia kwa wakimbizi na jamii inayozunguka maeneo haya,”alisema
baadhi ya wadau wengine Shirika la Chakula Duniani (WFP), lililowakilishwa na Said Johari,na Oxfam Josephat Joseph ambao nao wanahudumia wakimbizi, walisema wanafanya kazi kuhakikisha wakimbizi wanafuata maelekezo yote ya wataalamu wa afya, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kutosalimiana kwa kushikana mikono na mikusanyiko yasiyokuwa yalazima ambayo yanaweza kusababisha maambukizi
“Tunagawa chakula cha zaidi ya siku 30 kwa wakimbizi ili kupunguza makusanyiko ya mara kwa mara kwa wakimbizi maana awali walikuwa wanapewa kwa siku saba, tumewagawa katika makundi wanaopokea jioni na wengine asubuhi ili kupunguza muda wa kuwa pamoja na muda mrefu na tunataraji kutoa chakula cha zaidi ya muda huo ili wakimbizi wakae pamoja kwa muda mrefu ili yasije yakatokea maambukizi,’’ alisema Saidi
Ofisa Afya Wilaya ya Kibondo, Steven Janks alisema kamati ya dharula ya wilaya imejipanga kuhakikisha ndoa zote zitakazofanyika kipindi hizi lazima zitolewe taarifa kwa kuombewa kibali kabla ya kufungwa ili wataalamu watoe ushauri na haitafungwa ndoa itakayokusanya idadi kubwa ya watu na sherehe zote zifanyike nje ya kumbi na kwa kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake mita mija na nusu hadi mbili
Alisema sasa wanawapima joto abiria wote wanaoshuka kwenye mabasi kituo cha Kibondo ili kuhakikisha maambukizi yanazuiliwa kuingia.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Luisi Bura alisema ni vizuri kuwapo uzingatiaji na utekelezaji wa kila kinacho amriwa akisisitiza watu wanaohitaji kufunga ndoa na sherehe zingine kuhakikisha wanaomba kibali toka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kibondo ili wataalamu wa afya wahusishwe na kushauri ili kutotoa mianya ya kuwepo maambukizi