26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Ngumi na michezo mingine inahitajika uwekezaji

GLORY MLAY

MCHEZO wa ngumi ni kati ya michezo yenye mashabiki wengi hapa nchini na nje ya nchi, lakini bado umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine hasa soka na mpira wa kikapu.

Wadau wa michezo hasa wale wa masumbwi, mara kadhaa wamekuwa wakiwashambulia na kuwalaumu mabondia pale inapotokea wamepoteza mapambano yao nje ya nchi.

Wanaolaumu wamekuwa wakidai kwamba mabondia wa Tanzania wamekuwa na tabia ya kuuza mapambano kwa wapinzani wao ili wapigwe kwa makusudi kwa makubaliano ya kulipwa fedha.

Miongoni mwa waliowahi kuandamwa na kashfa za kuuza pambano ni bondia mahiri nchini, Francis Cheka na hili lilitokea baada ya kupoteza pambano lake kwa ‘TKO’ dhidi ya bondia wa India.

Hata hivyo, hakuna yeyote kati ya wale wanaolaumu ambaye amewahi kuanika ushahidi usiokuwa na mashaka kwamba kuna mabondia wanauza mapambano.

Ombi langu kwa wadau wa michezo hapa nchini ni kwamba, tuache tabia ya kusubiri kuwalaumu mabondia wetu pale wanapofanya vibaya na badala yake kujitokeza kuwasaidia hasa wakati wa maandalizi ya mapambano hayo.

Ukweli ni kwamba mara kadhaa mabondia wamekuwa wakilalamika kukosa msaada wa wadau wakati wanapojiandaa na mapambano hasa dhidi ya mabondia wa nje ya Tanzania.

Tunaamini hakuna njia ya mkato katika kufikia mafanikio, hivyo basi ni wajibu wa viongozi wenye mamlaka ya kusimamia mchezo wa ngumi kuhakikisha mnatoa msaada unaokidhi kwa mabondia, badala ya kuwaachia wenyewe wafanye maandalizi ya zimamoto ambayo mwisho wa siku ni aibu kwa taifa zima.

Ifike kipindi tuache kufanya maandalizi ya mazoea kama kweli tunataka kusonga mbele katika mchezo wa ngumi ambao kila kukicha thamani yake imekuwa ikishuka hapa nchini, jambo ambalo ni kinyume na mataifa mengine ambayo yamekuwa yakiwekeza kwa kiasi kikubwa katika mchezo huu unaopendwa na watu wengi duniani.

Nachukua fursa hii kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye aliunda kamati maalumu ambayo jukumu lake ni kuhakikisha mabondia wanafaidika na jasho lao badala ya kutumika kuwanufaisha wale wanaojiita mapromota.

Ni jukumu la kila mpenda maendeleo ya michezo kuendelea kuunga mkono nia nzuri ya Waziri Mwakyembe ili mwisho wa siku mabondia wasiweze kujilaumu kuwa walipoteza muda wao kwa kujihusisha na mchezo huo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,608FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles