Na Asifiwe George, Dar es Salaam
TANZANIA inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Hadi sasa madaktari bingwa waliopo nchini ni watano hali inayowalazimu kufanya kazi kuliko uwezo wao, kwa mujibu wa taaluma ya upasuaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tiba ya Upasuaji wa Mifupa ya Fahamu (MOI), Dk. Othman Kiloloma, alisema hadi sasa kuna madaktari bingwa watano tu wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Dk. Kiloloma alisema hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inajiandaa kusomesha madaktari bingwa katika juhudi za kupunguza adha hiyo.
Alisema pamoja na gharama kuwa kubwa za kusomesha daktari bingwa ambaye hutakiwa kusoma kwa miaka 10, bado wanaamini watakabiliana na changamoto hiyo.
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na MOI, Wizara ya Afya na Taasisi ya African Relief Committee of Kuwait na Shirika la Kimataifa la Rahma, wameandaa kampeni ya afya na upasuaji kwa kuwatumia madaktari bingwa kutoka Misri, alisema.
Alisema madaktari bingwa hao watatoa huduma bure kwa wagonjwa wenye matatizo ya upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili na MOI.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampeni hiyo, Khamis Mkanachi, alisema lengo kubwa la kuendesha kampeni hiyo ya afya na upasuaji ni kukuza na kuendeleza uhusiano baina ya mashirika hayo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI.
“Kampeni hii ni kuongeza na kupanua wigo wa mashirika haya ya kimataifa katika kuhudumia jamii kupitia huduma za afya, hususan katika maeneo ya upasuaji ambayo kwa kawaida gharama zake ni kubwa na wananchi wengi wanashindwa kumudu.
“Pia ni kutengeneza fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa hawa madaktari bingwa kutoka Misri na madaktari wa Tanzania, kutakuwa na vikao vya pamoja kati ya madaktari hawa na uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika maeneo yao ya utendaji,” alisema Mkanachi.
Alisema kampeni hiyo ya upasuaji ilianza jana na itaendelea hadi Agosti 18 mwaka huu, kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kila siku.
Aliwataja madaktari bingwa watakaohusika na kampeni hiyo kuwa ni Profesa Mohamed Elbegermy, Profesa Ezzat Mohamed, Profesa Tamer Ahmed na Profesa Hussein Alsayed. Wote wanatoka Misri.