Na Yohana Paul, Geita
Madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wanatarajiwa kuwasili kwa mara nyingine katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kuendelea kutoa huduma kwa wenye uhitaji.
“Ujio wa madaktari hao katika hospitali ya CZRH unakusudia kutoa vipimo na matibabu kwa wenye dalili na changamoto ya presha, sukari na magonjwa ya moyo kutoka mkoa wa Geita na mikoa jirani,” amesema Husna Karamagi, Mkuu wa Idara ya Habari kutoka hospitali ya kanda Chato, katika taarifa yake kwa waandishi wa habari. Kambi ya madaktari itaanza Julai 15 hadi 17, 2024.
Husna amebainisha kuwa madaktari hao bingwa na wabobezi wa kitengo cha moyo kutoka JKCI wanawasili Chato kuendeleza vita dhidi ya magonjwa na viashiria vingine vya magonjwa ya moyo, sukari na presha. “Huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zilianzishwa rasmi Novemba 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ambapo mwaka 2022/23 zaidi ya wananchi 2,000 walipimwa,” amesema.
“Mwaka 2023/24, wananchi waliojitokeza kupata huduma hii imeongezeka ambapo zaidi ya wananchi 3,400 wamepimwa na kati yao 576 waligundulika kuwa na matatizo ya presha, kisukari na moyo,” ameongeza.
Amesema wagonjwa waliobainika kuwa na changamoto hizo walipatiwa matibabu na wengine kuendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa na bobezi kutoka JKCI kwa kliniki maalum. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imenuwia kuwanusuru wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na nchi jirani kutokana na vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukizwa.
“Uwepo wa kituo hiki kunawapunguzia wananchi gharama za maisha ambazo mwanzo walizitumia kusafiri umbali mrefu kwenda kutibiwa magonjwa haya jijini Dar es Salaam,” amesema Husna.
Aidha, ifikapo 2025, serikali inatarajia kuanza ujenzi wa jengo kubwa la upasuaji wa moyo na mishipa ya damu ambapo huduma zote za upasuaji zinazotolewa na JKCI zitaanza kutolewa katika hospitali ya kanda Chato.