Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
MABONDIA watakaopanda ulingoni katika pambano la Safari ya Beach, leo Oktoba 13,2023, wamejitokeza kwa wingi kupima afya zao, huku daktari Hadija Hamisi akiweka bayana kuwa wanachoangalia zaidi ni magonjwa ya kuambukiza kama homa ya ini na HIV.
Zaidi ya mabondia 30 watapanda ulingoni katika mtanange huo utakaofanyika Oktoba 22,2023 kwenye fukwe za Rongoni, Kigamboni, Dar es Salaam ambapo pambano kubwa litamkutanisha Hassan Ndonga dhidi ya Oscar Richard.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kupima afya, Hadija amesema endapo bondia atabainika kuwa na HIV, haruhusiwi kupanda ulingoni maisha lakini homa ya ini na mengine yanayotibika akipona anarudi kazini.
Ameeleza kuwa tofauti na hayo pia yapo magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza wanaangalia ili kuhakikisha bondia anapopanda ulingoni anakuwa na afya njema kuepuka madhara kama ya kuzimia na kupoteza maisha.
“Leo ni siku ya kupima afya mabondia kama kawaida yetu, hapa tunawapima magonjwa yote kwa kuzingatia mikanda ya dunia ambayo ni homa ya ini, HIV, magonjwa ya zinaa na mengine ya kuambukiza.
“Mtu atakayekutwa na tatizo mfano HIV, tunasema ngumi ‘bye bye, lakini magonjwa ya zinaa na homa ya ini yanatibika mtu akiwa mgonjwa tunamuanzishia kliniki.
“Kwa wasichana kitu kingine tunachoangalia ni ujauzito. Lakini mimi kama daktari wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, huwa ninajiongeza kuangalia magonjwa mengine ambayo hayapo kikanuni kama sukari na malaria,” amefafanua daktari huyo.
Ameeleza kuwa ameamua kuongeza vipimo vingine ambavyo havipo kwenye sheria kutokana na hali za mabondia wengi kutokuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara.
“Katika sheria za mkanda wa dunia hakuna kupima maralia lakini mimi najiongeza ili kuzuia madhara kwa sababu nishakutana na kesi nyingi kama bondia kuanguka na kuzimia,” amesema Dk. Hadija.
Kwa upande wake Mratibu wa Habari wa Peaktime Sports Agency, Victor Denis amesema wamejiwekea utaratibu wa kuwapima afya mabondia kabla ya pambano ili kujiridhisha kuwa kila mmoja yuko fiti.