25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mabehewa feki yamponza mke wa Kafulila

Jesca KishoaNa Elias Msuya, Dodoma

MBUNGE  wa Viti maalumu, Jesca Kishoa (Chadema), jana alifukuzwa bungeni   Dodoma  na kutakiwa kutohudhuria vikao viwili vilivyobaki vya mkutano wa pili,   kikao cha tisa na 10.

Kishoa   pia ni mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi).

Alifukuzwa bungeni jana saa 7 mchana baada ya mjadala wa kikao cha kamati kilichokuwa kikijadili  Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.

Jesca alishindwa kutoa uthibitisho wa madai yake kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe kwamba alitumia Sh bilioni 238 kununua mabehewa mabovu alipokuwa Waziri wa Uchukuzi.

Madai hayo aliyatoa Februari mosi mwaka huu, ambako Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa, aliyeongoza kikao hicho alimpa siku tatu kutoa uthibitisho wake.

Mbunge huyo  hakuutoa  huku akimtaka Dk. Mwakyembe ndiye autoe.

Akitangaza uamuzi wa kumfukuza bungeni, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema jana kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 63(6), Mbunge anapaswa kusema ukweli juu ya jambo lolote kwa kutoa uthibitisho kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge kama alivyotakiwa na  Spika kufanya hivyo.

Alinukuu pia Kanuni ya 63(8) akisema   endapo hadi kufika mwisho wa muda ambao mbunge amepewa kuthibitisha jambo au kanuni au maeelezo yake atakataa, au atashindwa kuthibitisha na kuliabisha Bunge na kama atakataa kufuta kauli, usemi au maelezo yake, basi spika atamwadhibu Mbunge huyo asihudhurie vikao vya bunge visivyozidi vitano.

“Kwa maelezo hayo, namtaka Jesca Kishoa afute kauli yake aliyoiotoa Februari 1, 2016,” alisema Chenge.

Hata hivyo, Jesca  alisimama na kukataa kufuta kauli hiyo akisema:

“Ahsante Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba  sitafuta kauli yangu kwa sababu Mwakyembe hajathibitisha…” alisema.

Baada ya kukataa kufuta kauli hiyo, Chenge alitoa hukumu kwa mbunge huyo kwa kumtaka asihudhurie vikao viwili vya Bunge vilivyobaki.

“Kwa kuwa kanuni hii inanitaka kumsimamisha Mbunge kwa siku zisizozidi tano na kwa kuwa tumebakiwa na siku mbili tu kabla ya kumaliza mkutano wa Bunge;   namsimamisha Jesca Kishoa kutokuhudhuria vikao viwili vya Bunge kuanzia sasa hivi. Naomba utoke nje. Nakutaka utoke nje….” alisema Chenge.

Wakati Jeca anatoka nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani walimshangilia huku wa CCM wakimzomea na  kusikika wakisema “mwongo, mwongo…”

Mbali na Jesca, suala la mabehewa feki liliibuka pia Februari 2 mwaka huu,  ambako Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema),  alisema   aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi baada ya Dk. Mwakyembe, Samuel Sitta, aliunda kamati iliyobaini ubovu wa mabehewa hayo.

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alisimama na kuomba kutoa taarifa akisema baada ya kuona mabehewa hayo kugundulika kuwa mabovu mkataba wa ununuzi uliwaruhusu kumbana aliyekuwa na tenda kuyatengeneza kwanza.

Siku ya kwanza kutolewa madai hayo bungeni, Dk. Mwakyembe alipinga madai ya Jesca akisema Serikali haikutumia hata Sh bilioni 60 kununua mabehewa hayo.

Waziri alisema yuko tayari kujiuzulu hata ubunge kama madai hayo yatathibitika kuwa ya kweli.

KAULI YA JESCA

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Jesca alisema hatishiki kufukuzwa bungeni na ndiyo kwanza mapambano yameanza.

Alisema ushahidi wake ni ripoti iliyotolewa mwaka jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyofikishwa  kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara.

“Niliyoyoyasema bungeni ni ya kweli, Bunge kwa nafasi yake halikutakiwa kuilinda Serikali. Mwaka jana Bunge lenyewe ndilo lililoagiza ripoti ya mabehewa iletwe bungeni.

“Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara. Ndiyo kamati ambayo mwaka jana nikiwa nje ya Bunge ripoti hii ililetwa na kwenye kamati na PPRA. Imethibitisha kwamba mabehewa yaliyoletwa yalikuwa chini ya kiwango. Haya siyo maneno ya Jesca Kishoa, ni ya PPRA,” alisema.

Alisema PPRA ndiyo iliyothibitisha kwa asilimia 100 kuwa malipo ya mabehewa hayo yalishafanyika nje ya nchi kabla hayajafika Tanzania jambo ambalo ni kinyume na sheria na utaratibu wa ununuzi.

Alidai   hata kampuni iliyopewa tenda ya ununuzi huo ya Hindustan Company Ltd, haikufanyiwa uchunguzi wa kutosha (Due diligence),

“Leo hii nchi inaingia tenda na kampuni ambayo haina rekodi, hatuna taarifa nayo, kuna nini kinafichwa? Tujiulize; inakuwaje Serikali ipige dili yenyewe, ijichunguze, na ijiwajibishe yenyewe?” alisema Jesca na kuongeza:

“Kinachonisikitisha, badala ya bunge kuitaka Serikali ilete ripoti bungeni wanataka mambo yaishie gizani. Haya ndiyo madhara ya Bunge kutekwa. Watuambie kwa nini Takukuru waseme wanawapeleka watu watano mahakamani kwa ufisadi wa mabehewa?”

Januari 26, mwaka huu Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzui na Kudhibiti Rushwa Tanzania (Takukuru), Valentino Mlowola, alisema kutokana na uchunguzi  walioufanya tayari wameshampeleka Mkurugenzi wa Mashtaka   (DPP),  ili kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuniz za ununuzi wa umma kitolewe.

Mlowola alisema   shauri hilo linahusu ukiukwaji wa Sheria za Manunuzi ya Umma Namba 21 ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake kwenye ununuzi wa mabehewa 25 ya kokoto kutoka katika Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles