Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amewateua mabalozi watano kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, imewataja mabalozi walioteuliwa na vituo vyao vya kazi ni Balozi Mbelwa Kairuki (Beijing – China), Balozi George Madafa (Italia), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi (Brazil), Balozi Fatma Rajab (Qatar), Balozi Profesa Elizabeth Kiondo (Uturuki) na Balozi Dk. James Msekela (Umoja wa Mataifa-Uswisi).
Mabalozi hao wataapishwa leo saa 10:30 jioni Ikulu Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Muhidin Mboweto kuwa Balozi.
 JPM AKUTANA NA MKAPA
Pamoja na uteuzi huo, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa Ikulu, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Mkapa alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni kumpa taarifa juu ya kazi anayoendelea kuifanya ya kuwa mwezeshaji wa mazungumzo ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.