Kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini kimepungua kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/12 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/17 huku wanawake wakiongoza kwa asilimia 6.5 na wanaume asilimia 3.5.
Akizindua matokeo ya Utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi nchini kwa mwaka 2016/17, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na janga la ugonjwa huo.
Amesema kwa mujibu wa utafiti huu wa mwaka 2016/17, inakadiriwa kuwa Watanzania milioni 1.4 wanaishi na VVU.
“Lakini kupungua kwa kiwango cha maambukizi hakumaniishi kuwa ukimwi umekwisha bali ni matokeo ya jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo wananchi katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.
“Pia utafiti huu umeonyesha kupungua kwa kasi ya maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia 5.1 mwaka hadi asilimia 4.7, inatokana na juhudi za pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau mbalimbali waliojikita katika kutoa elimu na huduma za masuala ya Ukimwi,” amesema.
Awali akitoa maelezo kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk. Albina Chuwa amesema huo ni utafiti wa nne kufanyika nchini, ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2003/04 ambao ulionesha kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 7.0 na kufuatiwa na tafiti nyingine za miaka ya 2007/08 na 2011/12 iliyoonesha maambukizi ya asilimia 5.1.
Kuhusu utafiti huu amesema umekuwa wa kipekee kwani unatoa makadirio ya kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote ikiwa ni pamoja na maambukizi mapya ya VVU, kiasi cha VVU mwilini kwa wanaoishi na VVU, na kiwango cha kufubazwa kwa VVU mwilini.
Amesema utafiti huu ulihusisha kaya 16,198 na kujumuisha wanakaya wote waliokuwa kwenye kaya wakilishi zilizochaguliwa na umegharimu kiasi cha Sh bilioni 7.4 ambazo zimetolewa na Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na Ukimwi.
Aidha, ametaja mikoa ambayo kiwango cha maambukizi ya VVU ni zaidi ya asilimia 10 ni Iringa yenye maambukizi ya asilimia 11.3 na Njombe yenye asilimia 11.4 huku mikoa yote ya Tanzania Zanzibar ikiwa na maambukizi ya ukimwi ni chini ya asilimia moja.