24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Nasubiri kuapishwa

pic+seif*EU yataka mshindi Zanzibar atangazwe

Na Mwandishi Wetu, Pemba

MGOMBEA urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewata wananchi wa Kisiwa cha Pemba kutembea kifua mbele, kwani anachosubiri ni muda tu ili aweze kuapishwa kuwa rais wa awamu ya nane wa Zanzibar.

Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia katika mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya viongozi wa wilaya, majimbo na matawi kisiwani Pemba uliofanyika wilayani Chakechake.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema wanachofanya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivi sasa ni kuchelewesha muda, lakini kwa kuwa wananchi wa Zanzibar wamemchagua yeye kuwa rais na dunia nzima inajua hilo, hivyo muda ukifika wenyewe watamwita na kwenda kumwaapisha kuwa rais wa Zanzibar.

“Wananchi wa Pemba kuleni mshibe, laleni bila ya hofu na tembeeni kifua mbele, hawana njia lazima watakubali maamuzi ya wananchi wa Zanzibar walionichagua niwe rais wao,” alisema.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema jambo la muhimu kwa wananchi wa Pemba na Wazanzibari wote wasikubali kuchokozeka baada ya hali iliyojitokeza, kwa sababu kuna watu lazima watafanya vitimbi kwa tamaa ya kuvuruga amani ya nchi.

Katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi  kilichofanyika visiwani humo mwishoni mwa wiki, chama hicho kiliweka msimamo kwamba, hakikubaliani na suala la uchaguzi wa Zanzibar kurudiwa, kwa sababu wananchi wameshafanya maamuzi ya kidemokrasia.

Alisema hakuna muda wa kupoteza ila kinachoelendea sasa ni propaganda zisizokuwa na msingi kinachopaswa kufanyika hivi sasa ni Tume ya Uchaguzi Zanzibar  (ZEC), kumalizia kazi yake na kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25.

“Waache wapoteze muda wataniapisha tu, na wajue muda wangu wa urais utaanza siku nitakapoapishwa kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  alisema jambo linalowatia kiwewe CCM na kutoa visingizio kuhusiana na kura za Pemba ni kutokana na fedha nyingi walizotumia kwa tamaa ya kupata majimbo Pemba.

Alisema CCM wamesahau kuwa miaka yote hawapati majimbo kisiwani Pemba na hivyo si ajabu katika uchaguzi wa mwaka huu kukosa viti vyote vya ubunge, uwakilishi na udiwani.

Maalim Seif alisema hata mgombea urais wa Zanzibar kupitia ADC, Hamad Rashid Mohammed ambaye alitegemewa na CCM kupunguza kura za Maalim Seif kisiwani Pemba hakufua dafu  zaidi ya kuambulia kura 495 tu.

“Viongozi wa CCM maskini walimdanganya sana Dk. Shein kuwa watapata viti Pemba na kura za kutosha za rais, wametumia fedha nyingi katika uchaguzi huu, lakini walisahau hali halisi ya Pemba na sasa wanahangaika,” alisema Maalim Seif

Alieleza kuwa zipo taarifa kuwa kiasi cha Sh milioni 70 zilitumiwa na CCM katika jimbo moja la Mtambwe, jimbo ambalo katika uchaguzi uliowahi kufanyika huko nyuma, chama hicho hakijawahi kupata kura zaidi ya asilimia tano.

Maalim Seif aliwapongeza mawakala wa CUF katika majimbo yote 54 ya Zanzibar kwa namna walivyo jidhatiti kulinda kura za chama chao na hatimaye kukiwezesha kupata ushindi mkubwa ambao haujapata kutokea Zanzibar.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF  Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema Uchaguzi Mkuu uliofanyika kisiwani Pemba mwaka huu ni mfano mzuri wa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki katika nchi nzima.

Alisema kuwa wale wanaodai kuwa kura zimezidi kisiwani humo ni waongo wanaotapatapa kwasababu kuna watu waliojiandikishwa zaidi ya 20, 000 hawakupiga kura na waliojitokeza kupiga kura ni 119,000.

EU: Mshindi Z’bar atangazwe

JUMUIYA ya Ulaya (EU), imeishauri Tanzania kumaliza mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar kwa njia ya mazungumzo kwa kuheshimu uamuzi wa wananchi.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya wawakilishi wateule 27 wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar kuhoji uhalali wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta matokeo huku, wakisisitiza kuwa wao ni washindi halali na wanajiandaa kuwatumikia wananchi waliowachagua kwa mujibu wa sheria.

Tangu kutangazwa kufutwa kwa uchaguzi huo, jumuiya mbalimbali za kitaifa na kimataifa zimekuwa zikishinikiza kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, huku wakitaka waelezwe dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo ambazo waliamini si sababu ya kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Balozi wa EU anayemaliza muda wake, Filiberto Sebregondi katika sherehe ya kutimiza miaka 40 ya jumuiya hiyo, ambapo alisema kuwa pamoja na ushindani uliokuwepo katika uchaguzi uliomalizika karibuni, Watanzania wamedhihirisha kwa mara nyingine kuwa ni watu wa amani.

Alisema kwa miaka 40 EU imekuwa ikisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo, kiuchumi na kijamii lakini hakuna kitu ambacho kingefanyika kama hakuna uimara na amani ambayo wamekuwa wakiishuhudia kwa kipindi chote.

“Tanzania imekuwa ni nchi ya amani na hili limejidhihirisha wazi kwa watu wake kukamilisha uchaguzi kwa amani, ila kwa upande wa Zanzibar matumaini yetu mgogoro utamalizwa kwa njia ya mazungumzo na maamuzi ya wananchi yataheshimiwa kwa aliyeshinda atangazwe,” alisema Balozi Sebregondi.

Alisema katika kipindi chote uhusino kati ya Tanzania na nchi za EU ulizidi kukomaa hasa katika nyanja za uchumi, kisiasa na usalama katika ngazi za kimataifa.

“Mahusiano yetu yalizidi kukua na kukomaa, mwingiliano wa kiuchumi, kisiasa na usalama katika ngazi za kimataifa imekuwa ikipewa kipaumbele kwa kushirikiana,” alisema

Alisema katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020 Euro milioni 626 zilitengwa na Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (EDF) ukisimamiwa na muongozo wa EU na fedha hizo zimeelekezwa katika utekelezaji wa maendeleo ya kisiasa na kijamii.

“Imeelekezwa katika uongozi bora, kusaidia bajeti, nishati na kilimo, EDF itakuwa ikishirikiana na vyanzo vingine vya misaada katika kusaidia miundombinu na jamii za kiraia,” alisema Sebregondi.

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile alisema umoja wa EU  na Tanzania umeleta faida nyingi na kutaka misaada hiyo ije ilenge uchumi na kuleta maendeleo.

“Katika sherehe hizi pia tumezindua kitabu ambacho kitaelezea uhusiano huo na manufaa yake lakini pia kumuaga Balozi wa EU hapa nchini  na Afrika Mashariki kwa kuwa muda wake umekwisha na tunamkaribisha sana wakati mwingine,” alisema Likwelele.

Kauli za waangalizi

Oktoba 29 mwaka huu timu za waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola iliyoongozwa na Rais mstaafu wa Nigeria, Dk. Goodluck Jonathan, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoongozwa na Oldemiro Baloi, Waziri wa Masuala ya Kigeni na Ushirikisho wa Jamhuri ya Msumbiji, Umoja wa Afrika (UN) ulioongozwa na Mheshimiwa Armando Guebuza, Umoja wa Ulaya (EU) ulioongozwa na Judithi Sargentini, ulipitia mchakato wa upigaji na kuhesabu matokeo ya kura nchini kote.

Pamoja na hali hiyo walisema kuwa wameshtushwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ya kufuta uchaguzi wa Zanzibar.

Waangalizi hao walitoa taarifa ya awali Oktoba 27, ambapo tulithibitisha kufanyika kwa mchakato halali wa upigaji na kuhesabu kura.

Tunauhimiza uongozi wa kisiasa Zanzibar kuweka kando tofauti zao, kuweka kwanza maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar na kuungana pamoja kutafuta suluhu ya haraka kwa masuala ambayo yamesababisha mkwamo huu.

HABARI HII IMEANDALIWA NA MAULI MUYENJWA , ZAMDA BIWI (RCT), DAR ES SALAAM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles