26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Haukuwa uamuzi rahisi

Na Faraja Masinde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema uamuzi wa kuingia katika Serikali, Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi.

Maalim Seif ameyasema hayo leo Jumanne Desemba 8, kwenye hafla ya kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika Ikulu Visiwani Zanzibar.

“Kwa upande wetu, uamuzi wa kuingia katika Serikali, Baraza la Uwakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi. Ulikuwa ni uamuzi uliotufikirisha sana, tumejadili sana na tumepishana sana. Hatimaye tukafikia uamuzi.

“Moja ya sababu zilizotufanya kufikia uamuzi huo ni imani yetu kwako wewe binafsi, maneno yako, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawishi kuwa unayo nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote.

“Tumeona wewe ni mtu tunayeweza kufanya naye kazi, tunayeweza kusikilizana na tunayeweza kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema. Nia yako ambayo ndiyo iliyotufanya na sisi tutangulize nchi kwanza licha ya madhila yote yaliyojitokeza katika Uchaguzi uliopita,” amesema Maalim Seif.

Aidha ameongeza kuwa;

“Wenzangu walipokuja na wazo hili la sisi kuungana na wewe, na baada ya kushauriana na wanachama wetu, niliwashauri kuwa sasa ni wakati wangu mimi kupumzika na kupeleka jina la damu mpya. Hawakunikubalia. Waliniambia, wewe ndiye uliyeongoza maridhiano na Rais Amani Karume mwaka 2009 na wewe ndiyo uliyeshiriki Serikali ya Kwanza ya Umoja wa Kitaifa na Rais wa wakati huo Dk. Mohamed Ali Shein. Wakaniambia maadam wewe ndio umelianza, basi ulimalizie.

“Wakasema wewe mtu mzima na utu uzima dawa. Wakanitaka nikubali ili nije kusaidia azma hii ya kutibu majeraha ya Zanzibar na kuyastawisha maridhiano. Sikuweza kuwakatalia. Niliwakubalia na ndio maana leo niko hapa,”amesema Maalim Seif.

Amesema serikali ya Umoja wa Kitaifa ni sawa na chombo cha usafiri, kwa msafiri yeyote awe wa baharini, angani au nchi kavu, lengo lake sio kuingia katika meli, ndege au gari. Lengo lake ni kufika safari aliyopanga. Safari ya Wazanzibari ni Maridhiano ya Kweli, Mshikamano na Umoja wa Kitaifa. Chombo chetu cha kufika safari hiyo kwa wakati ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo, ni wajibu wa viongozi sote ambao tumepewa jukumu la kuongoza Serikali kuhakikisha kwamba tunaelekeza chombo hichi katika safari hiyo.

Aidha amesema kuwa kwenda kwao serikalini ni nia njema ya kutaka kushirikiana kutafuta majibu ya kudumuya changamoto.

 “Kuja ketu serikalini na kuingia kule barazani na bungeni ni nia yetu njema ya kutaka kushirikiana kutafuta majibu ya kudumu ya changamoto, ni imani yangu binafsi na chama changu kuwa wajibu wa serikali hii ya awamu ya nane itakuwa ni kuwaunganisha Wazanzibar yaliyotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi hayajirudii tena.

“Niwaombe Wazanzibar wote walipo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa maridhiano, tumeze machungu yaliyotokana na uchaguzi, tushikamane kuijenga Zanzibar yetu,” amesema.

Upande wake, Rais wa Zaznibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema; “Katiba yetu inatuelekeza muundo wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa wa umoja wa kitaifa.

“Hapana shaka kwamba kwa uteuzi huu nilioufanya umezingatia matakwa ya katiba yetu, mbali na kuwa ni takwa la kikatiba binafsi, mimi ni muumini wa umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na maridhiano, naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa maridhiano ni njia nzuri ya kujenga umoja wa kijamii na ustawi wa nchi na wananchi wake,” amesema Rais Mwinyi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles