30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Maagizo nane mifuko ya plastiki

  • Zikiwa zimebaki siku tatu, Makamu wa Rais asema hakuna kuongeza muda

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimebaki siku tatu kufikia Mei 31 ambayo ni siku ya mwisho wa matumizi ya mifuko ya plasitiki nchini, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo manane ikiwa ni pamoja na marufuku ya maji ya kunywa yaliyokuwa yakifungwa kwenye mifuko, maarufu kama Kandoro na barafu.

Akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Samia alisema kuanzia Juni Mosi hakutakuwa na kubembelezana juu ya kuendelea kutumia mifuko hiyo inayotajwa kuwa ni hatari kwa mazingira.

Marufuku ya mifuko ya plastiki pia itahusu mifuko inayotumika kutengenezea barafu na maji maarufu kama ya Kandoro na Ice cream.

“Hayo ‘maji ya Kandoro’ mimi niko kinyume nayo, kwanza hatujui usalama wake, hivyo hakuna Kandoro wala hakuna koni,” alisema.

Bidhaa nyingine ambazo hazikutajwa na Makamu wa Rais lakini hufungwa kwa kutumia mifuko sawa na ile ambayo hufungia maji ya Kandoro, ni karanga ambazo huuzwa mitaani ama madukani na wajasiriamali wadogo, korosho, sambusa na chapati kwa mama ntilie na pilipili ama kachumbari kutoka kwenye vibanda vya chipsi. 

Pia aliwatahadharisha viongozi kuacha siasa katika utekelezaji wa marufuku ya mifuko hiyo, huku akisema kwa kiongozi atakayesimamia vizuri zoezi hilo, inaweza kuwa kigezo cha kumpandisha.

“Mameya niwaombe sana, hapa hakuna siasa, ni utekelezaji wa kuondoa mifuko ya plastiki nchini. Kosa umeya lakini simamia mifuko iondoke.

“Hili zoezi hatuwezi kurudi nyuma na haliwezi kushindwa, lazima kila mmoja awajibike. Nataka ijulikane kwamba ikifika Juni Mosi hakuna kuongeza muda wala kutazamana, hapa hakuna kubembelezana, nataka Watanzania waelewe hivyo,” alisema Samia.

Alisema pia katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira mwakani, mikoa na wilaya itapimwa kwa kuondosha mifuko ya plastiki katika maeneo yao na watakaofanya vizuri watazawadiwa.

Kuhusu mpango kazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema ni mzuri na kama ukifanya vizuri utatumika nchi nzima.

“Dar es Salaam ndio kigezo, tukifanya vizuri nchi yote itafanya vizuri kwa sababu ndio msambazaji mkubwa,” alisema.

MAPENDEKEZO

Makamu wa Rais alipendekeza maeneo yaliyotengwa kukusanyia mifuko hiyo yasimamiwe vizuri ili isiharibu mazingira.

Maonesho ya mifuko mbadala yafanywe kwa wingi, wananchi waijue na kuhamasisha wafanyabiashara kuzalisha kwa wingi.

Fedha nyingi zielekezwe katika utoaji elimu na taarifa na kuepuka kupeleka mahali ambako hakutaleta matokeo makubwa.

“Asilimia 80 ya wananchi hawasomi mabango, wako ‘busy’ kujitafutia riziki, tunaweza kutumia fedha nyingi kuweka mabango lakini yasilete ‘impact’ (matokeo),” alisema Samia.

Alilitaka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutafsiri mpango kazi wao kwa Kiswahili na kuusambaza sambamba na kuharakisha kutoa leseni kwa wawekezaji wanaotaka kuzalisha mifuko mbadala.

Pendekezo lingine ni kutolewa kwa elimu ya sheria na kanuni kwa vyombo vya habari na viongozi wa dini waweze kufanya uchambuzi na  kuelimisha umma.

WAZIRI WA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alisema hadi sasa nchi 127 zimechukua hatua kadhaa za kudhibiti matumizi ya plastiki na 60 zimepiga marufuku ya moja kwa moja.

Alisema kila mwaka zaidi ya mifuko bilioni tatu inaingia katika mazingira na inachukua miaka kati ya 400 hadi 1,000 kuondoka.

“Tulikokuwa tunaelekea kulikuwa ni kubaya sana na hatua kama hii ilikuwa ni lazima kuchukuliwa,” alisema Makamba.

Alisema kanuni za utekelezaji agizo hilo zimeshatungwa na zitachapishwa kwa lugha ya Kiswahili na kugawiwa kwa wadau wote nchini ili ziweze kueleweka vizuri.

Hata hivyo, alisema licha ya sheria kutoa adhabu mbalimbali, watahakikisha wanaelimisha wananchi waone umuhimu wa jambo hilo na kuzuia hatari ya kutumia nguvu.

Alifafanua kuwa kinachokatazwa ni mifuko ya plastiki, lakini vifungashio vingine vya vyakula, vifaa vya ujenzi na mifuko mikubwa ya taka haijakatazwa.

“Safari ya kuondoa mifuko ya plastiki nchini lazima iwe kwa hatua, bidhaa zingine zinazofungwa kutoka viwandani hazijakatazwa bali kinachopigwa marufuku ni mifuko ya plastiki,” alisema.

Alisema pia Dar es Salaam ndiko ambako mifuko mingi inazalishwa, kutumika na kutupwa sehemu mbalimbali na madhara yake yanaonekana kila wakati, hasa katika rasilimali za bahari.

Makamba pia alitahadharisha katazo hilo lisitumike kubughudhi wageni wanaoingia nchini na kwamba katika wiki ya kwanza ya utekelezaji, mifuko mbadala itatolewa bure kwa wageni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

“Kutakuwa na dawati maalumu Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, lakini ‘hatutasachi’ wageni kutafuta kwenye mabegi yao kama wana mifuko ya plastiki.

“Kama atakutwa nayo kwa utaratibu mwingine ataelekezwa sehemu ya kuiweka na kupewa bure mifuko mbadala,” alisema.

MIFUKO MBADALA

Makamba alisema hadi sasa viwanda 70 na wajasiriamali wengi zaidi wako tayari kuzalisha mifuko mbadala.

Alisema pia mwezi uliopita kulikuwa na ongezeko la asilimia 300 ya malighafi katika kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Mufindi.

“Watakaoanzisha viwanda vya kutengeneza mifuko mbadala, ‘fee’ ya mazingira itaondolewa katika kipindi cha miezi sita.

“Tunaamini uchumi wa mifuko mbadala ni mpana, shirikishi na utatoa ajira kwa watu wengi na kuiongezea Serikali mapato,” alisema Makamba.

UTEKEKEZAJI DAR ES SALAAM

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Omar Kunenge, alisema wamejipanga kutekeleza agizo hilo bila kuleta kero kwa wananchi.

Alisema wamejipanga kutoa elimu kwa umma, kuwa na mfumo wa ufuatiliaji na usimamizi katika maeneo ambapo mifuko itawekwa na kushirikiana na wadau kuhakikisha kunakuwa na mifuko mbadala.

“Kuacha kutumia mifuko ya plastiki ni suala la tabia, hivyo tunataka mabadiliko ya tabia na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili utekekezaji wetu uwe ni rahisi zaidi,” alisema Kunenge.

Alisema pia wameunda kamati za vikosi kazi katika ngazi ya mkoa na halmashauri zote na kwamba wana maeneo 137 ya kukusanyia mifuko ya plastiki.

Nao wakuu wa wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni walisema wamejipanga kutekeleza kampeni hiyo kikamilifu sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.

TBS, SUMATRA

Mwakilishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Heri Msuya, alisema tangu mwaka 2016 walisitisha utoaji wa leseni za uzalishaji wa mifuko ya plastiki.

Alisema mwaka jana walitengeneza kiwango cha kitaifa kitakachotumika kutoa leseni za uzalishaji kwa watengenezaji wa mifuko ya karatasi.

“Tutaanza kuandaa viwango vya kitaifa kwa ajili ya mifuko mbadala inayotumika katika vifaa tiba, kilimo na viwandani,” alisema Msuya.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Gilliard Gewe, alisema wameanza kutoa matangazo katika vituo vyote vya mabasi Tanzania Bara tangu Mei 23 mwaka huu na sehemu kubwa ya Watanzania wamesikia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles