NA JESSCA NANGAWE
BEKI wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, Hamis Yusuph, amemtaka Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, kumpa nafasi beki wake chipukizi, Hajji Shaibu ‘Ninja’, ili kumjengea kujiamini na kuonyesha kipaji chake na si kumuweka benchi.
Yanga leo itashuka dimbani kuvaana na Njombe Mji, iliyopanda daraja katika Uwanja wa Sabasaba, uliopo Njombe.
Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, beki huyo alisema Ninja amekuwa mchezaji mwenye bidii sana, endapo atapata nafasi ana uwezo mkubwa wa kuja kuwa zao bora kwa timu yake ya Yanga.
“Ninja ni beki mzuri na akubali kukabiliana na changamoto akiwa kwenye timu kubwa, suala la kuzomewa ni kawaida kwa wachezaji, pia kikubwa kocha angekuwa anamtumia katika mechi nyingi ili kumpa kujiamini ili aweze kukabiliana na timu mbalimbali,” alisema Yusuph.
Alisema kuwa, Ninja anapaswa kuiga mfano wa beki wa sasa wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ambaye alianza kama yeye kwa kuzomewa, lakini alijifunza kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali hadi kufika hapa alipo.
Ninja alisajiliwa na Yanga akitokea katika timu ya Taifa Jang’ombe ya Visiwani Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili, lakini ameonekana kutoaminiwa sana na kocha Lwandamina, huku akimuweka benchi katika baadhi ya michezo.