HARRIETH MANDARI-GEITA
KATIBU wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga amewataka wakuu wa mikoa kuchapa kazi na kuachana na vitendo vya rushwa.
Alitoa kauli hiyo juzi kwenye kikao cha wakuu wa mikoa 10 wa kanda ya ziwa na magharibi ambao walikutana mkoani Geita katika kikao cha ujirani mwema kujadili hali ya usalama katika mikoa hiyo na kuweka mikakati utendaji.
Mikoa hiyo ni Tabora, Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida, Kagera, Rukwa, Katavi, Mara na Geita.
Vilevile walipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali iliyojengwa kupitia fedha za miradi ya jamii ( CSR), ikiwamo zahanati ya Nyamalembo, Shule ya Msingi Bombambili, kiwanda cha kuchakata dhahabu cha Magambo na mgodi wa GGML.
Alisema umefika wakati wa kuchapa kazi na kuhakikisha wanawajibika kwa ufanisi katika majukumu yao ikiwamo kutunza siri za Serikali.
“Tuwajibike kwa ukamilifu kwa kuhakikisha mnasimamia migogoro iliyopo maeneo yetu.
“Epukeni rushwa kuna watu wanatumia nafasi zao vibaya wanashidwa kusimamia ipasavyo wanapokea rushwa.
“Mkuu wetu wa nchi anapenda watu watendewe haki na imani yake ataka tuishi mazingira ya amani,”alisema.
Aliwashukuru kuanzisha ushirikiano wa ujirani mwema, kwa sababu unaleta chachu ya maendeleo katika mikoa yao.
Aliwataka kuendelea kusimamia ilani ya CCM, na pia kuwatumikia wananchi kwa ukamilifu.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alisema lengo la kikao hicho lilikuwa kujifunza na kubadilishana uzoefu wa mbinu mbalimbali za utendaji katika nyanja za uchumi na utawala bora.
Alisema haiwezekani nchi tajiri kama Tanzania wageni waingie na kusomba mazao kama vile alizeti ambyo huisafirisha kwenda kuiboresha nchini mwao kwa manufaa yao, badala ya kuongeza thamani hapa nchini.