26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi: Lissu legeza ‘kamzizi’ Ukawa warudi bungeni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi

Gabriel Mushi na Aziza Masoud

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi, amesema anayekwamisha mjadala wa Katiba Mpya ni mmoja wa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tundu Lissu.

Amesema kwamba, kama Lissu ataamua kubadili msimamo uwezekano wa Ukawa kushiriki Bunge Maalumu la Katiba ni mkubwa kwa vile ana uwezo mkubwa wa kushawishi, kujieleza na kujenga hoja.

Kutokana na hali hiyo, amemuomba Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alegeze kamba ili Ukawa warudi bungeni.

Lukuvi alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza katika mdahalo wa Katiba Mpya ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA).

“Namuomba Tundu Lissu awashawishi wenzake warudi bungeni, huyu ndiye kimzizi kikubwa cha Ukawa, yaani kama kuna mchawi namba moja ni Lissu.

“Huyu akilegeza tu kamzizi kake, nawaambia tutaendelea na Bunge kama kawaida. Tundu Lissu namfahamu sana na kwa muda mrefu ana uwezo mkubwa wa kushawishi, ni mtaalamu wa sheria na ana uwezo wa kujifungia ndani akaandaa kitu ili ashawishi watu hata kwa muda wa saa 12.

“Uncle, legeza kidogo kwa sababu wewe ndiye unayewaendesha hawa Ukawa,” alisema Lukuvi huku akimnyooshea kidole Lissu aliyekuwa amekaa jirani naye.

Pamoja na hayo Lukuvi alionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Ukawa kususia Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa walikuwa wakielewa kilichokuwa kikiendelea wakati wa mijadala ya Bunge hilo.

Kutokana na hali hiyo, alisema Ukawa hawana haja ya kuendelea kukaa nje ya Bunge hilo linalotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma.

“Nawaomba mrudi bungeni, utaratibu tulioweka katika kanuni utaenda vizuri na kama kutakuwa na tatizo, tutatafuta njia ya kutatua kwa makubaliano,” alisema.

Naye Lissu alipokuwa akichangia, alisema Ukawa hawataweza kushiriki tena Bunge  hilo kwa kuwa kanuni za kuliendesha zimekiukwa.

Kwa mujibu wa Lissu, kinachotarajiwa kufanyika baada ya Bunge hilo kuanza kesho ni CCM kuandaa rasimu ya Katiba wanayotaka kuliko wanavyotaka wananchi.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha mjini Iringa, Profesa Gaudence Mpangala, alisema wajumbe wa Bunge la Katiba wanatakiwa kuheshimu rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi.

Wakati hayo yakiendelea, mjadala huo ulitawaliwa na zomea zomea baada ya baadhi ya washiriki kuzomewa.

Pamoja na wachangiaji kadhaa kuzomewa, aliyekumbwa na hali hiyo pia ni Lukuvi ambaye alizomewa dakika chache kabla ya kuanza kuchangia. Wakati akizomewa, baadhi ya washiriki waliondoka ukumbini wakionyesha kutotaka kusikiliza alichokuwa akitaka kukichangia.

“Kama ni kuzomea, zomeeni kwa sababu mimi ni mzoefu wa kuzomewa,” alisema Lukuvi.

Wengine waliozomewa ni George Kinde ambaye alichangia kwa kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Katika mchango wake, Kinde alimshutumu Jaji Warioba kwa kusema kuwa kitendo cha tume aliyoiongoza kupendekeza muundo wa Serikali tatu, hakiwezi kukubalika kwa kuwa kitaliingiza taifa katika machafuko.

Kinde alipokuwa akiendelea kuchangia, baadhi ya washiriki wa mdahalo huo walichachamaa na kumzomea huku wakitaka anyang’anywe kipaza sauti.

Baada ya kelele kuzidi, muongozaji wa mdahalo alilazimika kuchukua kipaza sauti na kumfanya Kinde asiendelee kuchangia.

Mwingine aliyezomewa alikuwa ni Dk. Emmanuel Makaidi ambaye alianza kuchangia kwa kupiga vita muundo wa Serikali mbili.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa tume hiyo, wanatarajiwa kushiriki mdahalo wa Katiba Mpya ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Mbali na Jaji Warioba, wengine watakaoshiriki mdahalo huo ni pamoja na wajumbe wa tume hiyo, Joseph Butiku, Dk. Salim Ahmed Salim, Profesa Palamagamba Kabudi na Mwantumu Malale.

Taarifa iliyotolewa jana katika mitandao ya kijamii na mmoja wa waliokuwa wajumbe wa tume hiyo, Hamphrey Polepole iliwataja wajumbe wengine watakaoshiriki mdahalo huo ni Polepole mwenyewe pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria  Zanzibar, Awadh Ali Salim.

Taarifa hiyo ilisema mdahalo huo utarushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha ITV na Redio One.

- Advertisement -

Related Articles

6 COMMENTS

  1. Waswahili husema” maji yakimwagika…”. Serikaliya CCM inavuna ilichopanda…yaani chuki, fitina, majivuno, ubabe, kiburi, manyanyaso, vurugi, mayowe nakadhalika.Tulipokuwa tunawaeleza wananchi CCM imepoteza mwelekeo watu walisema tunafanya siasa hasa sisi mapadre na wachungaji. leo yako wapi, hakuna kitu kibaya kuwa na mavijuno, na kujifanya unajua yote, unaweza yote na huna woga wa kitu chochiote. Hayo yanayotokea kwa CCM sasa ni matokeo ya kuwadharau watanzania wakifikiri bado ni wale wale wa kukandamizwa, kumbe wameamka zamani. Treini imeanza safari haiwezi kurudi nyuma…tusubiri tutaona matokeo yake. Wale wanaoendelea kuwashurutisha UKAWA warudi ungeni, hivi watarudi wakajadili nini na katika mazingira yepi? mazingira ya matusi, kejeli, madharu, na vitisho? Nani yupo tayari kwa hilo? Mimi nawaunga mkono UKAWA kususia Bunge la katiba kwa sababu hakuna kilichorekebishwa. Nadhani Ukawa wana busara nawapongezeeni, kurudi huko mtakaonekana hamna msimamo, itakuwa ni kuwasaliti Watanzania ambao maoni yao yanataka kuchakachukuliwa. UKawa ni mkombozi wa wananchi Tanzania, bakini na msimamo huo. ngoja CCM wajadili rassimu waandike katiba mpya, halafu wailete kwa wananchi, halafu wataona wananchi wataifanya nini. Kibusara, Rais avunje bunge, pesa ziokolewe, zipelekwe kununua madawatu shuleni, walipwe walimu, na zingine mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.UKawa hongereni sana kwa msimamo wenu huo, na hii ni lama ya nyakati toka kwa Mungu kwamba muda wa mabadiliko nchini Tanzania umefika. Hatuwezi kutumia maneo ya Mungu ati kwa sababu watu watasema ni udini, kwanza siasa bila dini ni wendawazimu, na ndipo tulipofikiria. Wanasiasa wa Tanzania wanajidai hawataki kusikia maneno ya Mungu lakini wanasahau wanachama wengi wa CCM ni wale ambao ni waumini katika madhehebu mbali mbali. CCM ijitathimini imeboronga wapi? Narudia tena kusema ” CCM inavuna ilichopanda….fitina,chuki,uwongo, ubabe, jeuri,….”

    • Fr. Baptiste ameongea vizuri mno tena bila woga. Ni kweli kabisa kwamba CCM ni wababe na kiburi cha hali ya juu. Mambo hayawezi yakabakia hivihivi miaka yote. Lazima kutakuwa na mabadiliko. CCM hawako tayari kuachia serikali kwa njia ya kura. Ndio maana wanapambana na rasimu ya katiba maana imewakalia vibaya. Hawataki uwajibikaji. Wanataka serikali isioulizwa maswali.

  2. Bwana Lukuvi, kama umeona kuwa bwana Tundu Lisu ni mwongeaji mzuri na kwamba anajua sheria, basi kumbe anayo busara na hekima tunayoihitaji wengi, hivyo anayoyazungumza uyafanyie kazi kwa sababu ndiyo busara yenyewe ambayo kimsingi wananchi tuliowengi ndivyo tunavyotaka.

    Kifupi, Tundu Lisu anao upeo mkubwa na uelewa mkubwa na ndani mwake hana ubinafsi kabisa pamoja na wenzake wote katika kundi la UKAWA. Mimi nawapongeza tu UKAWA pamoja na timu nzima iliyopo. CCM mjitathmini, yatakayotokea ambayo ni mabaya, lawama zooooote tutazielekeza kwenu ninyi ndiyo mtakaozibeba. Mnasema Waryoba ameanzisha suala ambalo litaleta mgogoro, mgogoro huo atauanzisha nani kama si ninyi wenyewe CCM ambao tayari mmeuanza? Ubinafsi haufai, wananchi tunataka ijadiliwe rasimu ya katiba ambayo Waryoba na timu yake walikusanya maoni kwetu, ijadiliwe si vinginevyo!. Mnayoyaendekeza CCM ndiyo fujo zenyewe na pia ndicho chanzo cha machafuko, jadilini rasimu muone kama kutatokea hayo ambayo yatatokea kwa kukosa kuijadili rasimu ya katiba.

  3. ccm wanazomewa sawa ila naomba dunia na watanzania waelewe jambo moja kuwa moja ya dhambi na fedheha kubwa ni pale utakapogungua kuwa upiye mzomea alikuwa na hoja ambayo ungemsikiliza ingekusaidia na unaanza kumuunga mkono.swala hili la muundo wa serikali hakuna mwenye majibu sahihi ila majadiliano na muuno wa mbali vitatoa jibu sahihi.kumbukeni warioba anqsema walitazamq uzito wa hoja ili usahihi au kutokuwa sahihi hakuna mwenye jibu kamili.ahsant

  4. Bunge la katiba halina wana CCM peke yao wapo wajumbe kutoka asasi nyingine mbalmbali kwanini hao wanafikiriwa ni wana CCM tu? Acheni fikra potofu hivi CHADEMA wangekuwa wameshika nchi na wakawa na wabunge wengi wangewakataa? kUMBUKENI KUWA CCM kuwa na wabunge wengi ni chaguo la wananchi hamwezi kuzuia, wananchi gani hao mnaowatetea ambao walipenda wenyewe kuchagua CCM? wINGI WA ccm KWENYE BUNGE LA KATIBA hauepukiki hata kama wewe utakuwa unaichukia CCM Jambo la msingi ni kukubaliana katika mambo ya msingi ya kitaifa sio kukaa na kuionea wivu CCM. mBONA aFRIKA KUSINI BADO WANAITHAMINI ANC? Wananchi kama wataichukia CCM wataiondoa madarakani kwenye kura sio maneno ya mtaani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles