24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

LUGOLA APIGA MARUFUKU POLISI KUKAMATA WATU KWA AMRI ZA WAKUU WA MIKOA, WILAYA

 

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepiga marufuku polisi kuwaweka watu ndani kwa saa 48 kutokana na maagizo ya wakuu wa wilaya na mikoa.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, alisema imekuwapo  tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia mamlaka  waliyopewa katika sheria ya kuwaweka watu mahabusu kwa saa 48 hata kama wamezozana katika jambo lisilo katika msingi ya kazi.

Aliwataka polisi kuhakikisha wanahoji wakuu wa mikoa na wilaya sababu za kuwaweka watu wanaoelekezwa kuwakamata na kujiridhisha kama kuna sababu za msingi za kufanya hivyo na endapo watabaini hakuna, wawaachie huru.

“Nimeshamweleza Mkuu wa Jeshi la Polisi mahabusu zile ni za jeshi la polisi na wao ndiyo wanaotekeleza kumweka mtu ndani mtu uliyempeleka.

“Wale askari walio kwenye chumba cha mashtaka wanapokea na kusikiliza ‘huyu na huyu’ kwa hiyo pale wanapoona aliyeletwa hakuna sababu za msingi za kumweka ndani, wanaweza kumwachia.

“Kumekuwa na wananchi na wengine ni viongozi na baadhi ya wakuu wa wilaya wanatumia mianya ya mamlaka waliyopewa kuweka watu mahabusu saa 48  hata pale ambako mmezozana (kiongozi na mwananchi) huko nje katika masuala ambayo si ya kazi.

“Mmekorofishana huko kwenye mawindo nayo unakuja huku na kumkamata mtu na kumwambia utanitambua mimi ndiyo DC, hilo ndilo hata mimi waziri mwenye dhamana nasema hapana,” alisema.

Lugola pia alisema ameanza kutembelea vituo vya polisi na atahakikisha anavifikia popote vilipo  kujionea utendaji na ufanisi wa askari katika kuwahudumia wananchi.

Alisema atakapofika katika kituo cha polisi na kukuta mwananchi ameonewa au kubambikiwa kesi, atamweka mahabusu askari aliyehusika  aone hasara ya kulichafua jeshi hilo.

“Nimesema hakuna kituo cha polisi kiwe kikubwa au kidogo ambacho sitafika, nitapita huko   kuona wananchi ambao inadaiwa wanabambikiziwa kesi na polisi wasiokuwa waaminifu wanaoshirikiana na baadhi ya Watanzania wenzetu wasiokuwa waaminifu.

“Popote nitakapokuta hawa askari wachache wanaotuharibia sifa nzuri na utendaji wa jeshi la polisi na kuwachukulia hatua.

“Nimekukuta wewe askari umemtesa mwananchi kwa sababu za rushwa, umembambikiza kesi, umemweka mahabusu pasipo sababu na wewe papo kwa papo nakuingiza humo humo  ili uone hatari na hasara ya kulichafua jeshi la polisi,” alisema Lugola.

Alisema kama  Biblia ilivyoandika kuwa mwanadamu hajui siku wala saa atakayokuja mwana wa Adamu (Yesu), pia askari katika vituo vyote nchini hawajui siku wala saa watakayoibukiwa na Ninja (Lugola).

Wakati huo huo Waziri Lugola, amemwagiza  IGP Simon Sirro, kuwashughulikia askari wanaokamata magari ya abiria na kuyapeleka katika vituo vya polisi huku yakiwa na abiria hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi.

Lugola alisema imekuwapo tabia ya baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutotumia busara wanapokuwa kazini  gari linapokamatwa kwa kosa la dereva likiwa na abiria.

Alisema baadhi hupeleka gari hilo polisi hali inayosababisha abiria kukaa muda mrefu licha ya kutohusika na kosa hilo.

Waziri alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha kero kwa wananchi na kukwamisha kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa ufanisi ikiwamo kuchelewa kesi zinazowakabili na usaili kwa wale wanaotafuta ajira.

“Nimemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha vitendo hivyo havitokei tena. Kwa mfano leo nimepigiwa simu na baadhi ya abiria wakilalamika kutendewa kitendo hicho na askari aliyewakamata  amewaacha kituoni na yeye kuondoka” alisema Lugola.

Waziri Lugola aliwataka askari kutumia busara  wanapolikamata basi kwa kuliacha liwafikishe abiria sehemu wanayokwenda kisha kutoa taarifa kwa askari walio karibu na kituo linapoenda basi husika  likamatiwe huko.

Kuhusu makosa yanayohusu ubovu wa gari, alisema anaamini hakuna abiria aliye tayari kuendelea na safari na basi bovu litakalohatarisha usalama wa maisha yake.

Lugola pia ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama  chini ya wizara yake kuainisha maeneo  yanayomilikiwa na vyombo hivyo na yale yaliyopimwa na yana hati miliki.

“Nimewaelekeza wakuu hawa wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanaainisha maeneo yote ambayo yamevamiwa na wananchi ama taasisi au mfanyabiashara yeyote yule. Nimewaeleza pia kuainisha mahitaji ya ardhi kwa matumizi ya baadaye kwa ajili ya shughuli mbalimbali za vyombo hivi.

“Kuanzia sasa ni marufuku kwa mwananchi, kampuni ama shirika lolote lile kuvamia ardhi ama maeneo yanayamilikiwa na vyombo hivi na mtu yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za sheria,” alisema.

Imeandaliwa na Meza Fride (SJMC), Edwin Mkenda (Saut), Frank Kagumisa (Saut) na leonard Mang’oha.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles