Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Cha cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka marafiki zake waliobaki CCM waendelee kumuunga mkono na kushirikiana kwa kumpatia taarifa kwa ajili ya hatima ya nchi.
Aamesema Watanzania bado wanataka mabadiliko na imezidi kuthibitika kuwa hawawezi kuyapata ndani ya CCM .
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema kwa sasa Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza mabadiliko hayo na suala hilo linapatikana ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Nina furaha kutimiza mwaka mmoja tangu nilipojitoa CCM na kujiunga na Chadema. Uamuzi ule haukuwa rahisi, lakini kwa ushupavu, ujasiri na mwongozo wa Mungu nilifanya hivyo. Nilifanya uamuzi wa historia katika nchi yetu.
“…kwa wale wenzangu waliobaki CCM na wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatma ya nchi yetu. Nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema,” alisema Lowassa.
Alisema anajivunia uamuzi wake ambao alisema umewafungua macho Watanzania wengi na kuimarisha demokrasia.
“Nimeingia Chadema nimewakuta viongozi na wanachama waliyo na moyo wa dhati wa kuliletea maendeleo taifa lao kwa vitendo. Najihisi mwenye furaha kubwa na raha kuwa upande huu.
“Watanzania bado wanataka mabadiliko na hali hiyo imezidi kuthibitika kuwa hawawezi kuyapata ndani ya CCM. Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza mabadiliko hayo, vyote hivyo watavipata ndani ya Chadema na Ukawa kwa jumla.
“…nawahakikishia Watanzania na wana Ukawa kwa jumla kuwa hivi sasa nina ari, nguvu na hamasa kubwa kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Lowassa katika taarifa yake.