26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Nilivyoagana na Senga akiwa Dar, India

Marehemu Senga
Marehemu Senga

Na KULWA KAREDIA, DAR ES SALAAM

“MDOGO wangu Kulwa salama, nimefurahi sana kukuona leo, nimekuja hapa Muhimbili kukamilisha taratibu za kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa oparesheni ya moyo.

“Nimesumbuka sana na tatizo hili, nimekwenda hospitali nyingi hapa Dar es Salaam, wamenipatia dawa nimetumia muda mrefu, lakini matokeo yake si mazuri. Naamini kama nitakwenda India naweza kufanikiwa kumaliza tatizo hili kama Mungu akinisimamia vizuri.

“Baada ya kufanya mipango yote, leo nimekuja (Hospitali ya Muhimbili) kukamilisha nyaraka muhimu ambazo daktari wangu (jina ninalo), ataniandikia ili kesho nianze kushughulikia visa kwa pale ubalozi wa India.

“Mpaka nimefikia hatua hii mdogo wangu haikuwa kazi rahisi, kwa sababu gharama nilizoambiwa ni Sh milioni 26, mimi na ndugu zangu tumekaa tumechangishana mno. Sina cha kuwalipa kwa upendo wao kwangu.” Haya ni maneno ya kaka, rafiki yangu Joseph Senga, mpiga picha mkuu wa gazeti la Tanzania Daima nilipokutana naye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Julai 12, mwaka huu.

Baada ya kunieleza hayo, nami nikamwambia ‘kaka hapa nilipo na baba yangu mzazi ni mgonjwa, nahangaika na tiba’. Bila ajizi Senga akasema ‘twende nimsalimie baba’.

Ilimchukua karibu dakika 10 akiwa na baba yangu wanazungumzia mambo mbalimbali, huku mzee wangu akimsimulia namna alivyokuwa mkulima maarufu kuanzia miaka ya 60 hadi 2006 alipoacha shughuli za kilimo.

Senga hakusita, alimwambia baba yangu kuwa anaumwa, naye anahangaikia nyaraka za safari kwa ajili ya kwenda India kwa matibabu zaidi.

Baada ya hapo, Senga alirudi kwenye foleni, akakaa kwenye benchi na kusubiri kuonana na daktari wake. Muda si mrefu aliitwa akapewa barua zake, kisha akanifuata na kunionyesha, wote kwa pamoja tukafurahi tukiombeana heri.

Baada ya hapo tuliagana. Lakini jambo kubwa ambalo sitahau ni pale Senga aliponiita na kunipa namba yake ya simu ya kiganjani.

“Mdogo wangu, najua nitakwenda India, chukua namba hii tuwe tunawasiliana mara kwa mara,” aliniambia na kunipa namba yake ya simu ya mkononi. Nilichukua ile namba, sikujua alimaanisha nini.

Julai 15, saa nne asubuhi alinipigia simu na kuniambia amekamilisha nyaraka zake ikiwa ni pamoja na kupata visa yake na ya mdogo wake ambaye alimsindikiza huko. Kwa kweli nilifarijika sana na kumtakia kila la heri.

Baada ya hapo, kuanzia Julai 19, nilianza kumtafuta kupitia namba yake aliyonipa lakini sikumpata.

Sikukataa tamaa, Julai 22, saa 5 asubuhi nilifunga safari hadi nyumbani kwake Mtaa wa Sinza E na kumkuta mke wake, Frida Senga akiandaa chakula cha mchana, alinikaribisha kwa furaha mno, tukaongea kidogo. Nikamweleza kuwa jambo kubwa lililonipeleka pale ni kutaka kujua hali ya kaka Senga ambaye aliniambia anakwenda kutibiwa India.

“Oooh kweli amefika India na amefanyiwa upasuaji tayari,” alinieleza. Nikasema asante Mungu kwa hatua hii.

Kutokana na furaha aliyokuwa nayo Frida, akaniambia tangu Senga amekwenda India anatumia namba nyingine ya mtandao wa Zantel. Alinipatia na hapo hapo nikapiga, ikapokewa na mdogo wake aliyemsindikiza. Tukasamiliana na kujuliana hali ya mgonjwa, akanieleza kuwa yupo ICU, lakini anaendelea vizuri.

Kuanzia siku hiyo, kila siku ya Mungu tulikuwa tunawasiliana na mdogo wake akinipa maendeleo ya hali ya Senga, ambayo yalinipa moyo kuwa angerudi nyumbani akiwa mzima.

Juzi Julai 27 saa 6 mchana kwa saa za Tanzania, sawa na saa 9 alasiri India, nilipiga simu akapokea mdogo wake kama kawaida. Akaniambia kaka ameruhusiwa kutoka hospitali, hali yake ni nzuri. Akanitaka nisubiri kidogo anamalizia kulipa gharama za matibabu kisha ataniunganisha na Senga niongee nae.

Baadaye yapata saa 11 jiioni kwa saa za Tanzania, nikapiga simu na nikafanikiwa kuongea na Senga kwa dakika nane.

“Mdogo wangu, nafarijika kuona unanitafuta kila siku, huyu mdogo wangu aliyenisindikiza huku kila akija hospitali asubuhi kunijulia hali ananiambia umepiga simu, asante sana sana sana, naamini kweli unanipenda… Hivi sasa naendelea vizuri, leo (juzi) nimeruhusiwa kutoka hospitali nipo hotelini naendelea vizuri, upasuaji umekwenda salama, jambo la kushukuru Mungu, kama mambo yakienda vizuri, natarajia kurudia kabla ya Agosti 6, maana kuna dawa nimepewa za siku tano hivi nizitumie kwanza,” aliniambia Senga.

Baada ya maongezi mafupi, tukaagana kwa sababu alikuwa anahitaji kupumzika. Kumbe huo ndio ulikuwa mwisho wa mawasiliano yetu hapa duniani.

Nikiwa nimelala, usiku saa 7:10 simu yangu ikaita. Kuangalia naona jina la rafiki yangu Sitta Tuma. Niliamka nikaipokea, nikamuuliza ‘vipi usiku huu hii simu ina jambo la heri kweli?’

“Kaka! Kaka! Kaka! Unajua wewe ndiye uliyeniambia Senga yuko India kwa matibabu,” aliniambia, nikaitikia ‘ndiyo, kwani vipi?’

“Nasikitika kukwambia hatunaye tena duniani,” alinieleza.

Sikuamini, nikamwambia Sitta kata simu. Nikaamua kumpigia mdogo wake Senga aliyekuwa naye kule India. Ilikuwa karibu saa 10:15 za usiku. Akanithibitishia Senga amefariki dunia. Baada ya taarifa hizo, sikupata tena usingizi, maana sikuamini kilichotokea. Itoshe kusema Senga Mungu amekupenda zaidi.

Katika kitabu kitakatifu cha Biblia, Mtume Paul aliandika waraka kwa Wathesalonike 4:13-18 akisema: “Lakini ndugu, hatutaki mjue habari za waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na  hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti, kwa sababu bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu, nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki bwana hewani na hivyo tutakuwa pamoja na bwana milele, basi farijianeni kwa maneno hayo.”

Kwa maneno hayo, nasema Senga tangulia na sisi tunafuata maana hatujui siku yetu ni lini. Sitakusahau katika miaka minne na nusu tuliyofanya kazi pamoja pale Free Media. Nimezunguka na wewe Tanzania hii, tumesafiri usiku na mchana, tumepita maporini, tumenusurika kuuawa katika maeneo hatari kutokana na kazi zetu.

Nakumbuka siku tulipovamiwa na kundi la vijana wa chama fulani pale Igunga mkoani Tabora, lakini tulinusurika, sitasahahu siku tunapiga picha katika tukio la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario alipotekwa katika Kijiji cha Isakamaliwa. Sitasahau siku tulipofika Igoma mkoani Mwanza, jinsi mama yako mzazi alivyotupatia chakula, leo umemwacha mpweke, Mungu tusaidie.

Umeacha historia hapa duniani kwa kupiga picha za kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daud Mwangosi. Umekufa siku ambayo mtuhumiwa wa mauaji hayo amehukumiwa kwenda jela miaka 15. Kama si wewe, bila shaka polisi wangeficha ukweli wa tukio zima la Mwangosi. Ulivaa ujasiri bila kuogopa mitutu ya bunduki.

Senga umeniacha mpweke, sina la kusema, Mungu aipokee roho yako na aiweke mahali pema peponi – amina.

Kulwa Karedia ni Mhariri Mkuu wa Gazeti la Mtanzania – 0714 207 553

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles