NA ARODIA PETER, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amezitaka taasisi, mashirika ya haki za binadamu pamoja na vyama vya siasa nchini kuelekeza nguvu katika kujadili na kudai Katiba mpya itakayozingatia masilahi ya umma.
Amesema kwamba mjadala huo unapaswa kujielekeza katika kupata tume huru ya uchaguzi itakayokuwa haifungamani na upande wowote katika utawala, ikiwa ni pamoja na kuondoa nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia masilahi ya chama kilichoko madarakani.
Akizungumza na wazee wa Chadema kutoka Jimbo la Ubungo, waliokwenda ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam kumpongeza kwa kumaliza uchaguzi salama, Lowassa alisema anashangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, aliyesema tume hiyo ni huru na haina upendeleo wowote.
Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, alisema kauli ya Jaji Lubuva ni ya uongo, upotoshaji na kupoteza muda, huku akisisitiza kuwa NEC haifai na wajumbe wake walipaswa kufukuzwa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka jana.
“Natamani mjadala mpya kuhusu Tume ya Uchaguzi kupitia Katiba mpya uanze sasa ili tuweze kupata chombo cha kusimamia uchaguzi ambacho hakina ushawishi na Serikali au rais aliyepo madarakani, kwa sababu kauli ya mzee Lubuva ni ya uongo na asitupotezee muda.
“Katiba isiyozingatia utawala bora na haki za binadamu inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko na uvunjifu wa amani.
“Watanzania walio wengi wana hasira na tume hii ya uchaguzi kwa sababu iliboronga na kuchakachua kura zao, haifai na wajumbe wake walipaswa kufukuzwa baada ya uchaguzi kumalizika,” alisema Lowassa.
Aidha kiongozi huyo alitumia mkutano huo wa wazee kuzungumzia mgogoro wa Zanzibar ambapo alionya na kusema kama usiposhughulikiwa kwa hekima na busara, mambo yanaweza kuharibika.
“Kama CCM na CUF walikubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa maana ya kila upande kuongozwa na mwenzake aliyeshinda, kwa nini chama tawala kione ugumu kukiachia CUF ambacho inadaiwa kilishinda?
“Suluhisho la mgogoro wa Zanzibar si kurudia uchaguzi, bali ni kukabidhi madaraka kwa walioshinda ili nchi iweze kutawalika, vinginevyo nchi inaelekea kuzalisha makaburi.
“Mgogoro wa Zanzibar unapaswa kushughulikiwa kwa umakini chini ya meza ya mazungumzo, tumalize suala hili na kuvuka salama kama ilivyofanyika miaka mitano iliyopita ambapo vyama hivyo viliongoza pamoja chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
“Waroho wa madaraka wanaweza kudhani mgogoro huo ni wa Wazanzibari pekee, ingawa matatizo yatakayotokana na mgogoro huo yanatuhusu wote. Naomba tumalize suala hili kwa kukabidhi madaraka hata kama kuna upande utakaopoteza,” alisema Lowassa.
BARAZA LA WAZEE
Akielezea sababu za kwenda kwa Lowassa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Jimbo la Ubungo, Enock Ngombale, alisema walikwenda kumpongeza kiongozi huyo kwa kumaliza uchaguzi salama pamoja na kusimamia amani na utulivu licha ya kura zake kuchezewa na NEC.
Alisema wazee wa Ubungo wanamwomba aendeleze vuguvugu la kupata Katiba mpya itakayotoa dira ya Tanzania itakayopigania mabadiliko na uhuru wa kweli wanaoutaka Watanzania.
“Kwa niaba ya wazee wa Ubungo, tunakupongeza kwa dhati kwa uamuzi wako wa busara kuongoza upinzani kwa kufanya kampeni za kistaarabu hadi kumalizika kwa uchaguzi.
“Tunakushukuru kwa kuwezesha vyama vya Ukawa kupata kura nyingi za urais, ubunge na madiwani nchi nzima.
“Hicho ni kielelezo cha ushawishi wako mkubwa na kampeni ya nguvu uliyoifanya” alisema Ngombale.