25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

LOLOTE LINAWEZEKANA NUSU FAINALI ASFC

Na ZAINAB IDDY

MICHUANO ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama Kombe la Azam (ASFC), imezidi kunoga, baada ya miamba minne kutinga hatua ya nusu fainali, huku bingwa mtetezi, Mtibwa Sugar, akitimuliwa na KMC hatua ya robo fainali.

Timu zilizoingia nusu fainali ni Yanga, KMC, Lipuli FC na Azam FC, ambazo kila moja kama itachanga karata zake vizuri inaweza kufuzu fainali na hata kutwaa ubingwa, licha ya kwamba watu wengi wanatupa karata zao kwa Azam FC na  Yanga.

Makala haya yanakuletea tathmini ya miamba hiyo minne itakayopigana vita hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa wake ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hapo mwakani.

Lipuli FC Vs Yanga

Timu hizi zitakutana kwa mara ya tatu ndani ya msimu mmoja, kwani tayari zimekutana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili.

Mara ya kwanza Yanga ilikuwa ya kwanza kuialika Lipuli katika dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilizoka sare, kabla ya Yanga kukubali kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili Uwanja wa Samora, Iringa.

Lakini safari hii Lipuli ndiyo itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye uwanja wao ule ule wa Samora, ambao awali waliutumia kuiadhibu, huku makocha wote wakijinasibu kufika fainali na hivyo kuufanya mchezo huo kutabiriwa kuwa mgumu.

Msimu uliopita Yanga ilipoteza nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa na kuziachia Simba iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Mtibwa Sugar, hivyo ni wazi watakuwa wamejifunza kutokana na makosa.

Katika hilo, Yanga imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha inatwaa taji hili, ikianza na kuwaondoa wapinzani wao, ikianzia kwa Tukuyu Stars, Biashara United, Namungo FC na Alliance.

Kwa upande wa Lipuli, nao wana nafasi ya kufanya makubwa  na hii inatokana na kupata nguvu na imani kuwa taji hili si la timu kubwa pekee, baada ya Mtibwa Sugar kulinyakua mara ya mwisho.

Lipuli wamefika nusu fainali baada ya kuwaondoa Leha ya Rukwa, wakipata ushindi mnono wa mabao 9-0.

Kabla ya hapo ilizitandika Dodoma FC, Polisi Tanzania na Singida United.

KMC vs Azam FC 

Hii itakuwa mara ya pili kwa timu hizo kukutana, baada ya awali kukipiga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

KMC ikiwa chini ya kocha Ettiene Ndayiragije, imeonekana kuwa bora tangu mwanzo wa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitokea kushiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Chini ya wachezaji wake wakongwe wa Ligi Kuu, kama kipa Juma Kaseja, ni wazi KMC haitakuwa tayari kuona inapoteza nafasi hii adimu kwao, na hiyo ni baada ya kuwatoa mabingwa watetezi wa kombe hili, Mtibwa Sugar.

KMC imefika hatua hiyo baada ya kuzifungashia virago Pan African, Tanzania Prisons na African Lyons.

Azam kwa upande wake, nayo haina matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kimahesabu, hivyo nguvu zake imezielekeza ASFC, ambako inatakiwa ishinde mechi mbili tu, ili ipate nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho hapo mwakani.

Silaha kubwa ya Azam ni kuwa na wachezaji wazoefu na walio kwenye kiwango bora, lakini mabadiliko yaliyofanywa katika benchi la ufundi kwa kumtema Hans van der Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi na majukumu yao kupewa Meja Mstaafu Abdul Mingange na Iddi Cheche, yameongeza morali ya kufanya kazi kwa vijana wao wa Chamazi. 

Azam FC ilianza safari yake kwa kuwaondoa katika mashindano hayo timu za Pan African, Rhino Ranges, Pamba FC na Kagera Sugar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles