24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UN wampigia magoti Jenerali Haftar

NEW YORK, MAREKANI

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), limeyataka majeshi ya Jenerali Khalifa Haftar ambaye amefanya uasi, yasiendelee na msafara wake kuelekea katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Ombi hilo limetolewa na Balozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa, Christoph Heusgen, ambaye amelitaka jeshi la Jenerali Haftar kuacha mara moja harakati zake zote za kijeshi nchini humo na kueleza zinazidi kudhoofisha hali ya taifa hilo la kasakazini mwa Afrika. 

Balozi Heusgen amesema hayo baada ya kikao cha Baraza la Usalama mjini New York, ambako sasa Ujerumani ni Mwenyekiti wa Baraza hilo. Hapo awali mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za G7 pia walitaka kukomeshwa kwa mapambano hayo. Mawaziri hao wamesema mgogoro wa nchini Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi kama anavyofanya Jenerali Haftar.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya mapigano karibu na Tripoli, ambayo wamesema yanaweza kuvuruga utulivu na matarajio ya usuluhishi wa Umoja wa Mataifa wa kutatua mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.

Wanamgambo wanaounga mkono serikali magharibi mwa Libya walipambana na vikosi vya Jenerali Haftar juzi na kuwateka askari wake 100. Majeshi ya serikali yalitumia ndege kushambulia ngome za Jenerali Haftar muda mfupi baada ya kiongozi huyo kuyaamuru majeshi yake kuelekea mjini Tripoli.

Mapambano hayo yalitokea wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alipokuwa anamaliza ziara yake iliyokuwa na lengo la kuepusha kuongezeka kwa mgogoro. Guterres alikutana na Jenerali Haftar kwenye mji wa Benghazi.

Mkutano wa kimataifa juu ya kutatua mgogoro wa nchini Libya utafanyika baadaye mwezi huu chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa. Tangu kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi, nchi hiyo imegawanyika katika serikali; mbili ya mashariki na ya magharibi, pamoja na makundi mbalimbali ya wanamgambo.

Wakati huo wapiganaji 100 wa Jenerali Haftar wamekamatwa na wanamgambo wa magharibi mwa Libya pamoja na kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya moja ya kambi zake, ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo wa uasi kutangaza mashambulizi ya kutaka kuidhibiti Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Mashambulizi hayo yametokea juzi huku Guterres akiwa anamaliza ziara yake nchini humo, iliyokuwa na lengo la kuzuia kupanuka kwa mgogoro huo.

 Guterres amesema ameondoka Libya moyo wake ukiwa mzito, huku akiwa na wasiwasi mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles