Na MWANDISHI WETU
SERIKALI ya awamu ya tano iliingia madarakani chini ya kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na hadi sasa tumeshashuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali.
Kupitia taasisi zake, imehakikisha kwamba malengo na mipango iliyojiwekea inafanyika kwa ufanisi na kwa wakati na hivyo kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa huduma mbalimbali wanazozipata.
Miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotoa huduma kwa wananchi ni pamoja na Shirika la Bima la Taifa (NIC), ambalo ni kongwe hapa nchini, likiwa limeanzishwa mwaka 1963.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Sam Kamanga, anasema katika kipindi hiki cha awamu ya tano, wamepata mafanikio makubwa wakiongozwa na kauli mbiu ya ‘Bima Mpya Inawezekana.’
“Kitendo cha kuaminika kwa wateja wetu ni moja ya mafanikio, Shirika letu ni la Kitanzania na hapa ni nyumbani, kwa hiyo tunajivunia mno kukubalika nyumbani,” anasema.
Anasema kitendo cha Serikali kuzihamasisha taasisi zake mbalimbali kukata bima na NIC ni jambo kubwa ambalo shirika lake linaona ni mafanikio katika kipindi hiki cha awamu ya tano.
“Rais mstaafu Jakaya Kikwete alitangaza azimio linalozitaka taasisi za umma kukata bima kwetu hususan bima za magari, sasa ilivyoingia madarakani Serikali ya awamu ya tano, azimio hilo limeingia katika utekelezaji, kwa hiyo kwetu sisi awamu hii imekuja na mafanikio makubwa mno,” anasema.
Anasema baada ya Serikali kuhakikisha shirika linakuwa na nguvu za kiuchumi nao wamedhamiria kuchapa kazi.
“Kwa kweli hapa ni kazi tu, tumeamua na tumedhamiria kuchapa kazi tu ili kuhakikisha tunafikia mafanikio ambayo tumekusudia ikiwamo Serikali kupata gawio kutoka kwetu,” anasema.
Anafafanua kuwa shirika lake limetengeneza sera ili kuhakikisha kwamba wanatoa gawio ikiwa ni sehemu yake ya faida.
Anasema NIC ni shirika la umma linalofanya biashara ya kuhudumia umma wa Watanzania wote, ikiwamo sekta binafsi, kwa hiyo watahakikisha kwamba sehemu ya faida yao inakwenda serikalini ili kuchangia mapato.
Anaongeza kuwa ili kuhakikisha malengo hayo yanatimia, akiwa kiongozi mkuu wa shirika amewataka wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kutambua umuhimu wa mchango wao kama watumishi na wazalendo wa nchi hii.
“Tukitaka kwenda mbele tuchape kazi kwa bidii na maarifa, hapo tutakwenda mbele na shirika litazidi kukua hatimaye kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu,” anasema na kuongeza:
“Katika suala la uwajibikaji mimi sina mzaha, yule ambaye haendani na kasi yangu atupishe… sina mchezo na kazi, ni lazima tufanye kazi kwa bidii ili kuleta tija katika shirika letu,” anasema.
Anaongeza kuwa kwa sasa umma wa Watanzania unapaswa kuliamini shirika lake na kupata huduma mbalimbali za bima kutoka kwao.
“Nawaomba mno Watanzania watambue kwamba hili ni shirika lao, liko hapa nchini na litaendelea kuwapo… kupitia wao wataliwezesha shirika kuwa na nguvu kubwa sokoni, kiuchumi na hatimaye kuliwezesha kutoa gawio kubwa kwa Serikali, ambalo litasaidia katika kuiwezesha kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa umma,” anasema.
Anazitaja aina za bima zinazotolewa na shirika hilo kuwa ni bima ya mali na ajali, bima za maisha na bima za matibabu.
Mkurugenzi huyo anawatoa hofu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kuhusu ulipaji wa fidia mbalimbali zinazotokana na bima walizokata, akisema kuwa wanalipa kwa haraka.
“Sisi ni miongoni mwa kampuni tatu zinazolipa fidia kwa haraka, tunajivunia hilo na tunawaomba wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya hilo,” anasema.
Kuhusu mtandao wa shirika lake hapa nchini, anasema ofisi za shirika lake zipo nchi nzima na kwamba ni pekee lililosambaa maeneo mengi nchini.
Kuhusu ushindani, anabainisha kwamba wao wanahakikisha wanashindana sokoni ili kushinda na kuendelea kuwapo sokoni.
Anafafanua zaidi kuwa NIC inazidi kuboresha huduma zake kila kukicha na kwamba kwa sasa huduma zao zote zimewekwa kwenye mfumo wa kompyuta ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja.
“Katika hilo tuko vizuri, kila kitu kipo kwenye mtandao, kwa dunia ya sasa moja ya sifa ya kukufanya udumu sokoni ni teknolojia,” anasema.
Kuhusu mipango ya baadaye ya NIC, anasema wanazidi kuboresha huduma zao ili ziweze kukidhi matakwa ya wananchi.
Anasema hati ya bima ya maisha imeweza kuwasaidia wananchi kiuchumi kwa kuifanya iwe dhamana ya mikopo wanayochukua kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha.
Anabainisha kuwa wana mpango wa kuanzisha Bima ya Kilimo, lengo likiwa ni kuboresha huduma za sekta hiyo ambayo imeajiri Watanzania wengi, ambapo takribani asilimia 75 wanajihusisha na shughuli za kilimo.
“Kwahiyo, ni matumaini yetu kwamba bima hiyo itasaidia kuinua sekta ya kilimo,” anasema. Anaongeza kuwa NIC imedhamiria kurejesha imani ya Watanzania kwa shirika hilo ili liweze kuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa hili.
Kuhusu historia ya shirika hilo, anasema lilianzishwa mwaka 1963 likimilikiwa kwa ubia kati ya sekta binafsi na Serikali.
Anasema baada ya Serikali kutaifisha mashirika mbalimbali, likawa likimilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 huku likiwa shirika la umma pekee linalotoa huduma za bima Tanzania Bara.
Kamanga anaongeza kuwa hali hiyo iliendelea hadi miaka ya 1990 wakati Serikali ilipoanzisha mpango wa kurekebisha uchumi na kuruhusu kampuni binafsi za bima kuingia sokoni.
Anasema baada ya Serikali kuanza kubinafsisha mashirika, NIC ilikuwa kwenye orodha ya kubinafsishwa lakini baadaye likaachwa kufuatia uamuzi wa Serikali kufuta uamuzi huo na badala yake ikaweka mikakati ya kuliboresha.
Anabainisha kuwa kutokana na kampuni binafsi kuamua ‘kulipaka matope’ kwamba lina tabia ya kuchelewesha ulipaji wa madai, baadhi ya wateja walikimbia.
“Lakini katika kipindi hicho cha changamoto, tuliamua kusimama imara, kupambana na hali hiyo hadi tulipofikia sasa. Jambo jema ni kwamba pamoja na changamoto zote hizo zilizolikabili shirika, hatukuchukua ruzuku serikalini, tulisimama wenyewe,” anasema.
Kamanga anasema katika kipindi hicho waliathirika vibaya kwa kupoteza wateja na sekta binafsi ikatumia fursa hiyo kupata wateja wengi.
“Kwa sasa tuko imara kabisa sokoni na tupo tayari kushindana na kuleta changamoto ya uboreshaji wa huduma kwani soko likiwa na ushindani ni dhahiri kwamba wanaonufaika ni wateja,” anasema.
“Mwaka 2010 Serikali ilianzisha mageuzi kabambe ya kuliwezesha shirika kukabiliana na ushindani sokoni, moja ya mikakati hiyo ni kuanzisha timu maalumu ya kuongoza mageuzi hayo.
“Hadi sasa tuko kwenye mageuzi hayo ya kuliboresha shirika liweze kukabiliana na ushindani na kudumu sokoni, bima mpya na imara inawezekana,” anasema.
Baadhi ya wananchi wamelipongeza shirika hilo kwa kukabiliana na misukosuko ya kibiashara, hatimaye kusimama tena na kumudu ushindani.
“Kwa kweli ninalipongeza shirika letu la bima kwa kuhimili misukosuko hiyo na kudumu sokoni,” anasema Beatus Michael, Mchumi Mwandamizi na Mkazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Anatoa wito kwa Watanzania kukata bima zao kwenye shirika hilo kwa hoja kwamba ni la kwao na litaendelea kuwapo kwa masilahi ya umma wa Tanzania.