25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

LISTI YA MASTAA WALIOACHA MUZIKI WA KIDUNIA YAONGEZEKA

Na JOSEPH SHALUWA

HIVI karibuni mwanamuziki mahiri Bongo ambaye alikuwa akiimba muziki wa Taarab akiwa na Bendi ya Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf aliachana na muziki huo na kutangaza kumgeukia Muumba.

Kwa uamuzi huo, alisema hataimba kabisa muziki wa Taarab na akawataka mashabiki wake kuacha kumwita kwa jina lake maarufu la Mfalme, akisema Mfalme ni mmoja tu na siyo yeye.

Msanii huyo aliyekuwa tishio kwenye muziki huo kwa sasa ameanza kuimba Kaswida na hivyo kufuta kabisa ndoto za waliokuwa wakifikiri huenda angerejea jahazini.

Tukio la Mzee Yusuf likiwa halijapoa, msanii mwingine aliyeanza kuja juu hivi karibuni kwenye muziki wa Bongo Fleva, Khadija Maige ‘Khadija Nito’ akitokea Jumba la Vipaji Tanzania (THT) ametangaza kuokoka na kuachana na Bongo Fleva.

Pamoja na kuokoka pia amebadili jina lake ambapo kwa sasa anajulikana kama Natasha Maige Lisimo na tayari ameachia kibao chake cha kwanza kiitwacho Ufunguo akimshirikisha Bahati Bukuku.

Natasha (Khadija) amebadilika kila kitu, kuanzia mavazi na hata namna anavyoimba. Kabla ya kuokoka nyimbo zilizoanza kumpa umaarufu ni pamoja na Si Ulisema, Sina Maringo na Nifanye Nini.

Sasa cheki listi ya waliotangulia kuachana na muziki wa kidunia na kugeukia dini.

 

 

CHIDUMULE

Mwanamuziki wa muda mrefu Cosmas Chidumule kwa muda mrefu sasa ameokoka. Baada ya kuokoka tu aliachia wimbo wa Yesu ni Bwana ambao mpaka sasa bado unatamba.

Mbali na wimbo huo wa Injili, anao mwingine uitwao Hosiana ambao ameshirikiana na mwimbaji mwingine aitwaye Mwansasu – nao unafanya vizuri kama ilivyo Yesu ni Bwana.

Amepitia bendi nyingi na ameimba vibao mbalimbali maarufu kikiwemo kile cha Neema kilichovuma miaka ya nyuma huku kikiendelea kukubalika mpaka sasa.

 

K BASIL

Anaitwa Basil Kashumba ‘K Basil’ ambaye ni msanii mkongwe kwenye muziki wa kizazi kipya. Alikuwepo enzi akina Bob Rudala, Bizman, Mr. Paul, Stara Thomas na wengineo wakitamba kwenye Bongo Fleva.

Kibao chake maarufu hadi anaacha muziki miaka kadhaa iliyopita kilikuwa ni Riziki. Basil ni msomi wa Chuo Kikuu akiwa na Shahada ya Kwanza ya Jiografia na Mazingira.

K Bazil ameokoka muda mrefu na ameshatoa albamu moja ya Injili iitwayo Yesu Ananipenda ikiwa na nyimbo kama Namjua, Wakati na Bahati, Wewe ni Baba, Rudisha, Utukuzwe, Moyo, Tunasonga Mbele, Mama na Asante Yesu.

Mpaka sasa ni miongoni wa watumishi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam, chini ya Askofu Josephat Gwajima.

 

RENEE LAMIRA

Juhudi zake kwenye muziki ni kubwa kwani kupitia muziki wake alishawahi kutia maguu mpaka kwenye Tuzo za Kora. Wimbo wake maarufu uliompa mafanikio hayo ni Ngoma ya Kwetu wenye mahadhi ya asili na kitamaduni.

Mbali na Ngoma ya Kwetu ambayo ndiyo jina la albamu pekee aliyopata kutoa, Lamira alitamba pia na nyimbo kama Fitina na Ondoka.

Msanii huyu kwa miaka mingi sasa ameamua kuachana na muziki na kumrudia Mungu. Hadi anaamua kuokoka wakati huo alikuwa akisali katika Kanisa la Living Water chini ya Mtume Onesmo Ndegi.

 

STARA THOMAS

Mwanadada mwenye sauti tamu, Stara Thomas naye alitangaza kuokoka zaidi ya miaka mitano iliyopita na kugeukia muziki wa Injili. Ana nyimbo nyingi nzuri alizopata kuimba zikiwemo Mimi na Wewe, Sogea Karibu na Nipigie alioshirikishwa na msanii AT.

Akiwa ameokoka ametoa nyimbo kadhaa ukiwemo Nani Mshamba na Uwezeshwaji Mwanamke ambao aliutoa maalumu kwa siku ya mama.

 

Q JAY

Kijana huyu mwenye sauti tamu alikuwa ndani ya Kundi la Wakali Kwanza akiwa na wasanii wenzake, Makamua na Joseline. Q Jay yeye aliamua kujitenga na wenzake na kuokoka kisha kuanza kuimba muziki wa Injili ingawa hatambi kwenye muziki huo.

Akiwa na Wakali Kwanza alipata kutamba na Sifai, Nimebaki Lonely, Natamani na Kitu Gani.

 

DOKII

Dokii ambaye jina lake halisi ni Ummy Wenceslaus naye alipata kutangaza kuokoka na kuimba muziki wa Injili. Awali Dokii alikuwa msanii wa filamu lakini baadaye akaingia kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Kati ya nyimbo zake za Gospo ambazo hata hivyo hazijapata umaarufu mkubwa ni Nani wa Kumwabudu. Mbali na Gospo, Dokii anaimba nyimbo za kawaida (lakini siyo za kidunia) ambapo alipata kuimba wimbo maalum wa kumkaribisha aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama ‘Obama Welcome Tanzania’ wakati wa ujio wake nchini Julai, 2013 chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Hivi karibuni aliimba wimbo wa Uhuru Kenyatta ambao ulikuwa ukisifia utendaji kazi wa Rais huyo wa Kenya ambaye ameshinda kuongoza mhula mwingine katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.

Kwa sasa pamoja na mambo mengine, anatangaza kwenye kituo cha Redio E FM cha jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles