MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amewataka wananchi wa Morogoro kutafakari iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinastahili kupewa miaka mingine mitano.
Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, alitoa kauli hiyo jana wakati akiwatubia wananchi wa Morogoro Mjini katika mkutano wake wa kampeni.
Pamoja na mambo mengine, Lissu alisema katika historia ya nchi hii haijapata kutokea wakati wa uchaguzi wagombea ubunge na udiwani wa upinzani wakaenguliwa kwa kiwango kama cha sasa.
“Ndugu zangu wa Morogoro naomba tutafakari kwa pamoja kama tuna sababu yoyote ya kumwongezea Rais Dk. John Magufuli miaka mitano mingine naomba tutafakari mambo ambayo yamefanyika katika kipindi hiki cha miaka mitano ili tuweze kuamua yeye na chama chake kama wanastahili kupatiwa miaka mingine mitano.
“Mfano tunakwenda kwenye uchaguzi wakati hakuna ushindani mfano mgombea ubunge wa Chadema eneo hili (Devotha Minja) amenyimwa haki ya kugombea ubunge. Tutafakari hili kwamba hatuna mgombea si kwa sababu hakujitokeza lakini ni kwa sababu tume wamemzuia kuwasilisha fomu za uteuzi,”alisema Lissu.
Vilvile alisema katika jimbo hilo la Morogoro Mjini, chama hicho kikuu cha upinzani nchini hakina wagombea udiwani kwa kata 16 kati ya 29 kwa sababu wameuziwa na wengine kuenguliwa kwa sababu zisizokuwepo.
Alisema kati ya majimbo 11 ya Mkoa wa Morogoro, majimbo nane hakuna wagombea wa Chadema kwa sababu wamezuiwa kuwasilisha fomu za uteuzi.
Aidha alisema katika kata 214 ya Mkoa wa Morogoro, Chadema hakina wagombea udiwani kwa kata 109 kwa sababu walienguliwa.
“Tunafanya uchaguzi katika mazingira ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii. Mwaka 2015 hatukuwahi kuyaona haya na Morogoro tukashinda majimbo matatu.
“Hatukuyaona haya mwaka 2010 wakati Jakaya Kikwete anagombea kwa mara ya pili, hatukuyaona haya mwaka 2005 wakati Benjamin Mkapa akiwa Rais, mwaka 2000 hatukuyaona na mwaka 1995 hatukuyaona haya lakini sasa tumeyaona mwaka huu 2020 Magufuli akiwa rais.
“Sasa hii ni uchaguzi tu fikiria haya mengine ya miaka mitano tumepigwa marufuku kujihusisha na siasa. Wanapenda kutuambia tutii sheria bila shuruti lakini wao wamekuwa wakivunja sheria wazi wazi.
“Watu wamefunguliwa kesi zisizokuwa na dhamana, imekuwa miaka mitano ya kututia umasikini. Nimesema tutafakari ndugu zangu wa Morogoro. Tangu tumepata uhuru ni lini kiongozi akapigwa risasi halafu hakuna hata mmoja ambaye anashukiwa.
“Mkayatafakari haya niliyoyasema leo ninyi na marafiki na familia zenu kama kuna haja ya kuendelea kuwa na uongozi huu kwa miaka mitano mingine.
“Imeandikwa katika vitabu vya dini kuwa haki huinua taifa. Nataka tushinde uchaguzi huu ili tutende haki kwa sababu maovu yakitawala watu huogopa,”alisema Lissu.
Kampeni za uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, zinaendelea kwa vyama kunadi ilani kwa Watanzania na zitahitimishwa Oktoba 27 mwaka huu.
Wagombea urais wanaoshiriki katika uchaguzi huu ni 15 ambapo mbali na Lissu na Dk. Magufuli, wengine ni Queen Cuthbert Sendiga (ADC), Bernard Membe (ACT-Wazalendo), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Cecilia Mwanga (Demokrasia Makini), Hashimu Rungwe (Chaumma) na Seif Maalim Seif (AAFP).
Pia wamo, John Shibuda (Ada-Tadea), Yeremia Kulwa Maganja (NCCR-Mageuzi), Philipo Fumbo (DP), Leopard Mahona (NRA), Mutamwega Magaywa (SAU), Twalib Kadege (UPDP) na Maisha Mapya Muchunguzi wa NLD.