Na MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwingine mkubwa.
Upasuaji huo utahusu mguu wake ulioshambuliwa kwa risasi na utakuwa mkubwa zaidi na wa mwisho.
Taarifa za ndani ambazo gazeti hili limezipata kutoka Nairobi, Kenya, ambako Lissu anapatiwa matibabu zinaeleza kuwa alitakiwa kufanyiwa upasuaji huo tangu juzi lakini ulishindikana kutokana na hali ya majeraha aliyokuwa nayo.
Endapo upasuaji huo utafanyika kama ulivyopangwa utakuwa ni wa mara ya zaidi ya nne tangu ashambuliwe kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7 mwaka huu.
Jana gazeti hili lilijaribu kumtafuta Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye amemsindikiza Lissu kwenye matibabu ili azungumzie suala hilo lakini hakupatikana.
Itakumbukwa upasuaji wa kwanza wa kumuweka sawa ulifanyika katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma saa chache baada ya kushambuliwa, na nyingine zilifanyika katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakoendelea na matibabu.
Wakati hayo yakijiri, MTANZANIA Jumamosi limebaini kuwapo kwa kauli tata au zenye kuacha nyufa mbalimbali kuhusiana na tukio la kushambuliwa kwake.
Kauli hizo si tu kwamba zimetolewa na viongozi wa Serikali hata wanasiasa hususani wa Chadema na hivyo kuibua maswali mengi katika jamii.
Miongoni mwa kauli zilizoacha nyufa katika jamii ni zile zilizotolewa hivi karibuni kabisa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kuhusiana na uchunguzi dhidi ya watu waliohusika katika tukio la kushambuliwa Lissu.
Katika mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Clouds yaliyofanyika juzi, Mwigulu alisema gari ambalo Lissu alidai lilikuwa likimfuatilia wakati akiwa Dar es Salaam lipo mkoani Arusha na halijawahi kufanya mizunguko ya aina yoyote jijini Dar es Salaam.
“Utoaji wa taarifa na wenyewe haukuwa rasmi kwa mfano Lissu aliposema kuna gari inamfuatilia, nilielekeza polisi wakaifuatilia ikakutwa Arusha, kuna gari ndogo ya namba hizo hizo, kwa hiyo kuna moja iliweka namba batili.”
Kilichozua maswali katika kauli hiyo ya Mwigulu ni pale aliposhindwa kuelezea njia waliyotumia polisi kuipata gari hiyo na kujiridhisha kama haijawahi kufanya mizunguko Dar es Salaam.
Hoja hiyo inatiliwa mkazo na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliyezungumza na MTANZANIA juzi akihoji njia walizotumia polisi kujiridhisha na jambo hili hasa ikizingatiwa kuwa nchi haina kamera barabarani wala kwenye mitaa.
Watu waliofuatilia mahojiano ya Mwigulu na kituo hicho wanasema utata mwingine aliouibua ni pale alipoeleza uamuzi wa Jeshi la Polisi kukamata magari 10 yanayofanana na lile linalodaiwa kuwabeba wahalifu waliomshambulia Lissu, huku likikaa kimya kuhusu wamiliki wake.
Mwigulu ambaye alitafutwa kwa njia ya simu jana ili kujibu maswali yote hayo lakini hakupatikana, pia inaelezwa kwamba hakufafanua wanachokisema wamiliki wa magari hayo, jambo ambalo limeacha pia maswali kuhusiana na uchunguzi unaoendelea dhidi ya tukio hilo.
Ukiachana na kauli hizo, jambo lingine linaloonekana kuzua utata katika jamii tangu Lissu ashambuliwe ni ushiriki wa Serikali katika matibabu yake.
Itakumbukwa jinsi jambo hilo lilivyozua maswali kiasi cha Serikali kulazimika kujitokeza hadharani na kueleza kuwa ipo tayari endapo itapelekewa maombi na familia ya Lissu.
Hoja hiyo ilionekana kuleta mvutano na familia ambayo ilieleza bayana kwamba iliandika barua ya maombi.
Si tu serikali hoja kama hiyo haikuliacha Bunge ambalo awali lilieleza utaratibu wake kuhusu kumtibu Lissu kuanzia hospitali ya Dodoma, Muhimbili na kisha nchini India kutegemeana na ushauri wa madaktari.
Ingawa tayari Bunge limeshatuma fedha zilizotokana na posho ya siku moja ya wabunge lakini hatua yake ya kumchagulia hospitali Lissu tofauti na wanavyofanyiwa wabunge wengine imelalamikiwa vikali na Chadema.
Mbali na Bunge, hoja kama hiyo pia imeigusa Chadema yenyewe kwani wapo wanaohoji ushiriki wake katika kusaidia matibabu ya Lissu.
Kwamba kwanini hadi sasa Chadema imeshindwa kutanguliza mbele fedha zake hususani zile za ruzuku kusimamia matibabu ya Lissu kabla kutafuta michango kutoka kwa wananchi kama ilivyofanya.
Jambo jingine ambalo linaonekana kuzua maswali mengi hadi sasa na ambayo hayajapata majibu yanayojitosheleza ni mazingira ya tukio lenyewe kwamba ilikuwaje dereva wa Lissu asipatwe na risasi wakati wa shambulio hilo?
Siku chache baada ya Lissu kushambuliwa, dereva huyo alikaririwa na gazeti moja (Si Mtanzania) akisimulia jinsi alivyojinusuru kushambuliwa na wahalifu hao wasiojulikana.
Katika maelezo yake alisema baada ya wahalifu hao kuanza kuwashambulia kwa risasi, aliamua kumlaza Lissu kwenye kiti cha dereva kisha yeye akaruka nje ya gari na kujificha uvunguni mwa gari jingine lililokuwa limeegeshwa jirani na mahali walipokuwapo.
“Ghafla yule bwana akashuka na bunduki aina ya SMG ambayo niliiona wakati anafungua mlango. Akaanza kumimina risasi kwenye gari letu. Nilichokifanya, ni kumlaza Lissu kwenye kiti cha dereva na mimi kuruka nje ya gari na kujificha uvunguni mwa gari jingine lililokuwa limeegeshwa kwenye uwanja wa nyumba za wabunge.
“Nilimwona kabisa huyu mtu aliyekuwa anarusha risasi; ninamfahamu. Alikuwa amevaa kapero na miwani nyeusi na kizubao…Ni yule yule niliyekuwa nimekutana naye jijini Dar es Salaam,” alikaririwa dereva huyo.
Katika mkutano na vyombo vya habari alioufanya wiki iliyopita, Mbowe alidai kwamba watu wasiojulikana walitumia magari matatu kulizingira gari la Lissu na kushambulia.
Si hilo tu pia zipo hoja dhidi ya Jeshi la Polisi kuhusu kitendo chake cha kutomkamata dereva huyo wakati wote baada ya kutokea tukio lile na hata sasa akiwa nchini Kenya.
Gazeti hili linazo taarifa kuwa, dereva huyo alisafiri kwa njia tofauti na ile aliyopitia Lissu na aligongewa mihuri nyaraka zake zote za kusafiria na maofisa wa uhamiaji, kitendo ambacho kimezua maswali na kutoa taswira ya kutokuwapo kwa mawasiliano baina ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Ukiacha hilo la dereva, ufa mwingine unaojitokeza sasa baada ya tukio la Lissu, ni kitendo cha Chadema kutompa ulinzi licha ya kufahamu wazi alivyokuwa akitishiwa maisha.
Wapo wanaoamini kuwa kabla Jeshi la Polisi halijawajibika na usalama wa Lissu, Chadema wao walipaswa kulitazama jambo hilo mapema zaidi kwa kumwongezea ulinzi.