Na Fredy Azzah,
GWIJI na mwalimu wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, juzi alipimana ubavu wa kujenga hoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwa zaidi ya dakika 20.
Wawili hao walikuwa wakijenga hoja juzi jioni wakati wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, ambapo walikuwa wakibishania usahihi wa nafasi ya Jaji Mkuu kukaimiwa kwa muda mrefu.
Mbali na ilivyozoeleka kwamba Lissu hujenga hoja zake huku akitumia maneno ya kejeli, juzi alijikuta akimwomba radhi, Profesa Kabudi pale alipojikuta ametumia kauli kama hizo kwa Profesa huyo ambaye ni mwalimu wake.
“Katiba yetu ilisema katika maoni yangu kuna sababu kwa nini huyu anaitwa Kaimu Jaji Mkuu, kuna sababu na kuna sababu ya ibara ya 118 (1), inayosema ‘Jaji Mkuu’ kuna tofauti kati ya Jaji Mkuu na Kaimu Jaji Mkuu, na hoja yangu ni kwamba ukishasema acting, kaimu ni interlocutory ni ya muda, haiwezi ikawa haina ukomo, ndiyo maana inaitwa kaimu, ndiyo maana inaitwa ya muda, pending substantive appointment.
“Sasa Profesa anataka kutuaminisha kwamba kunaweza kukawa na Kaimu Jaji Mkuu miaka yote, haiwezekani, siyo kwa katiba hii, nasema mheshimiwa natoa shilingi (kwenye mshahara wa waziri ) tujadiliane,” alisema.
Baada ya maelezo hayo ya Lissu, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyekuwa akiendesha kikao cha juzi, alimpa nafasi, Profesa Kabudi kujibu hoja zilizotolewa.
“Nirudie yale yale niliyoyasema kwamba, nafasi ya kaimu jaji mkuu kama nilivyosema, ni pale (inapokoma) kwa mujibu wa ibara ya 118, Rais atakapomteua Jaji Mkuu, au Jaji Mkuu atakaporejea nchini, ama kama alikuwa hawezi kufanya kazi anaumwa, atakapokuwa amerudi kazini, huo ndiyo ukomo.
“Sasa lini Rais atamteua jaji mwingine ili Kaimu Jaji Mkuu aache kuwa Kaimu Jaji Mkuu, hilo ndilo nililosema halijawekewa muda, hajaambiwa miezi sita, miezi mitano, hajawekewa, lakini mara akimteua huo ndiyo ukomo wa Kaimu Jaji Mkuu.
“Na nilichokisema ukija kwenye function (kazi) zake ndiyo maana ukienda kwenye Ibara ya 151 pale, function zake ni zile zile za Jaji Mkuu ana-enjoy mamlaka yote ya Jaji Mkuu, na ana enjoy security of tenure, ambayo tayari ana- enjoy kwa sababu ni jaji wa Mahakama ya Rufani.
“Na katika majukumu yake haingiliwi na yeye hawaingilii majaji wengine hata hakimu wa mahakama ya mwanzo, tangu ateuliwe (Kaimu Jaji Mkuu) ni takribani miezi mitatu, sasa Mheshimiwa Tundu Lissu ni mdogo wangu, nilisihi na ninaendelea kusihi.
“Unajua mahakimu na majaji wanasimama nafasi ya Mwenyezi Mungu, ni Mwenyezi Mungu peke yake mwenye hukumu ya haki, na ndiyo maana hukumu hiyo ya mwenyezi Mungu haina rufaa na sisi wote binadamu tunajitahidi, ndiyo maana kuna madaraja ya rufaa.
“Sasa watu ambao Nabii Daudi kwenye Zaburi ya 15 anawaita ni manabii wa Mungu, kwa sababu wanafanya kazi ambayo yeye peke yake ndiye mtenda haki tuwaheshimu kidogo.
Baada ya maelezo hayo ya Profesa Kabudi, Lissu alipewa tena nafasi ambapo alisema. “Mheshimiwa mwenyekiti shilingi yangu hairudi, hili jambo tulijadili.
“Spika wa Bunge na Mwenyekiti wa Bunge, wewe mwenyekiti (Chenge), unapokuwa hapo kazi zako ziko sawa na za Spika, wewe ni Spika? Wewe ni Spika? Sasa mwalimu wangu Profesa Kabudi anasema kwa vile kazi za Chief Justice (Jaji Mkuu), zinafanana na kazi za Acting Chief Justice (Kaimu Jaji Mkuu), then the acting Chief Justice is Chief Justice.
“Tafadhali, mheshimiwa mwenyekiti kuna kitu amekisema Profesa Kabudi kizuri sana, nchi zinaishi kwa mila na desturi, za kikatiba na kisiasa.
“Imetokea kwa Jaji Othuman Chande, utafikiri hamkujua kwamba, Chande Othuman atastaafu mkajipanga, utafikiri hamkujua, it was well known (ilikuwa inajulikana sana).
“Kwanini mnavunja Katiba na desturi yetu ya Mahakama, tumekuwa na majaji wakuu miaka yote why now (kwa nini sasa), kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti hili suala lijadiliwe, nimeondoa shilingi na hairudi,” alisema.
Ali Saleh
Baada ya maelezo hayo, nafasi ilitolewa kwa wabunge kuchangia hoja hiyo ambapo, Mbunge wa Malindi, Ali Saleh (CUF), alisema kwa sasa nchi inatengeneza utamaduni mpya kabisa.
Alisema hali iliyopo sasa inaonyesha nchi haipo imara na ni jambo ambalo linatishia hata wawekezaji.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Angelah Kairuki, alisema hajaona ubaya wowote wa kuwa na Kaimu Jaji Mkuu kwani kuna ufanisi wa mahakama.
Mnyika
Naye Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), alisema kama Kairuki haoni tatizo lolote tangu Kaimu Jaji Mkuu akaimu nafasi hiyo, kwa nini haoni sababu ya kukubali maoni ya Kambi ya Upinzani kwamba, Rais amthibitishe Kaimu Jaji Mkuu kushika rasmi nafasi hiyo.
AG
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema kambi ya upinzani imetoa hoja ya kutaka Rais amthibitishe Kaimu Jaji Mkuu kitu ambacho alisema ni kinyume na Ibara ya 37 ya Katiba.
Alisema Ibara hiyo inasema. “Mbali na kuzingatia masharti yaliyo katika Katiba hii na sheria nyingine za Jamuhuri ya Muungano, Rais atakuwa huru na hatolazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu wa mamlaka yoyote” alisema.
Lissu alipopewa nafasi ya kuhitimisha hoja yake, alisema kuna hoja inajengwa kwamba, wanaotaka Jaji Mkuu ateuliwe ni kuidharau mahakama, jambo alilosema si sahihi.
“Unaidharau mahakama kwa kutofanya mahakama iwe na kiongozi wake kamili, hiyo ndiyo dharau ya mahakama, siyo wale wanaohoji kwa nini haina kiongozi wake mkuu, ni nyie ambao mnasababisha isiwe naye.
Pili kuna hoja kwamba halijaharibika neno, limeharibika neno vibaya sana, mahakama ni muhimili wa dola, unaongozwa na Jaji Mkuu, Katiba imesema ndiye Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ukimfanya anakaimu hana uhakika kama kesho atathibitishwa hana hakika kama kesho ataondolewa, manake ni namna ya kuvuruga uhuru wa mahakama.
Baada ya hoja hiyo, Chenge alihoji Bunge juu ya wanaoafiki na wasioafiki, shilingi ya waziri iondolewe na kisha akasema wasioafiki wameshinda.